Mwanza. Wakati kukiwa na kundi la vijana linalojihusisha na michezo ya kubashiri, kudekezwa kwenye familia, kufuata mkumbo na kuchagua kazi baada ya kuhitimu masomo ni miongoni mwa sababu zinazotajwa kuchangia tatizo hilo.
Imeelezwa vijana wengi hujikuta wakiishia kucheza ‘Pool table’, michezo ya kubashiri, kukaa vijiweni na kusubiri wenzao wanaojishughulisha ili wawaombe kitu kidogo, maarufu kugongea.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, Neema Semaiko amesema hayo leo Machi 13, 2025 alipozungumza na wazazi na vijana 35 waliohitimu mafunzo ya stadi za maisha, elimu ya afya ya uzazi na malezi katika hafla ya kuwakabidhi wahitimu hao vyerehani 35 vilivyotolewa na Shirika la SOS Village, katika Kata ya Kayenze, wilayani Ilemela mkoani Mwanza.
“Niwape siri, usomi wa siku hizi hauna ajira, ajira ndiyo hizi kazi ambazo tunatakiwa tuwafundishe kuanzia nyumbani, sasa ukisema mwanangu amefika kidato cha sita hajazoea kazi, tabia hiyo tuache. Tujifunze kwa wazazi wetu waliotulea kwa kutufanyisha kazi,” amesema na kuongeza:
“Ndugu wazazi kubeti kunatuumizia watoto na kututia umaskini, wao wanafikiri kule wanapata fedha lakini hakuna anayetoa fedha ya bure. Atakufanya ufikiri unapata kumbe wewe ndio unampa fedha, yaani utafutaji wa pesa umekwenda kwa kiwango kingine zaidi cha kutapeli wengine ili wewe ule.”
Amewashauri wazazi kutokaa kimya wazungumze na watoto wao wawe wa tofauti, kwani hakuna kazi ya mwanamke au mwanaume, cha msingi iwe halali na mkono uende kinywani.
Amewataka wasifuate mkumbo kwani huwapoteza na kujikuta umri umekwenda na hawajafanya chochote cha maana, hivyo kubaki mzigo na mateso kwa wazazi.
Mkurugenzi huyo amewataka vijana 35 waliohitimu mafunzo kutobweteka na kuuza vyerehani walivyopewa, bali waungane kuanzisha kikundi wapate nguvu na uhalali wa kunufaika na mikopo ya asilimia 10 kwa vijana kutoka halmashauri, na kupata zabuni za kushona sare za taasisi mbalimbali za umma.
“Mikopo ya halmashauri ipo mnakaribishwa lakini muonyeshe kweli mna nia na kuna kitu mmeshaanza kukifanya, stadi za maisha mlizopata za kujiwekea akiba na nidhamu ya fedha zitumieni vyema tusije kufikia mahali tumekopa kwenye vicoba tukaweka cherehani rehani,” amesema.
Debora Fabian, muhitimu wa mafunzo hayo ya siku 90, amesema kutokana na kukosa kazi za kufanya wasichana wengi wanarubuniwa na kuzalishwa kisha kutelekezwa na kuwa mzigo kwa wazazi.
Amepongeza uwezeshaji uliofanywa akisema unawakomboa kutoka kwenye utegemezi.
“Baada ya kuhitimu masomo nilikosa kazi ya kufanya, hivyo kukosa mahitaji muhimu. Kutokana na vishawishi sasa nina watoto wawili ninaishi kwa wazazi, hivyo mafunzo haya na cherehani niliyopata vitanisaidia kujikimu kimaisha. Kwa sababu tumepata mwanga, tutaweza kulea watoto wetu na kujitegemea,” amesema.
Kijana pekee wa kiume aliyehitimu mafunzo hayo ya ushonaji, John Lucas amesema: “Serikali iendelee kubuni miradi na shughuli za kiuchumi kwa vijana ili kuwainua na kuwaepusha na vitendo vya utegemezi. Sisi tuliohitimu tunaomba tuwezeshwe mikopo ya halmashauri ili tusiishie njiani tukashindwa hata kulipa pango la biashara na wengine kujikuta wakiuza vyerehani.”
Kaimu Meneja Miradi wa Shirika la SOS Village Mkoa wa Mwanza, Elizabeth Swai amesema mafunzo hayo yalilenga kuwasaidia wahitimu kujiajiri, kutoka kwenye uduni wa maisha na utegemezi kwa kuondoa mzigo kwenye familia na kuwa wakombozi.
Amesema mradi huo umegharimu Sh26 milioni zikiwamo Sh15.2 milioni za kununua vyerehani 35.
“Nawasihi vifaa tunavyowawezesha tuvitumie kufikia malengo ya maendeleo, mkafanye kazi kwa malengo ili iwe sifa kwa kuchangia ajira kwa vijana. Tumieni ujuzi huu mlioupata kwa miezi mitatu muendelee kujifunza kuongeza maarifa na kukuza mitaji yenu,” amesema.