Wakati chama cha ACT Wazalendo, kikisusia kikao cha Baraza la Vyama vya Siasa, baadhi ya vyama vilivyoshiriki mkutano huo vimesema chama hicho, hakipaswi kudharau chombo hicho chenye dhamana ya kuimarisha mazingira ya siasa.
Wameeleza hayo Alhamisi Machi 13, 2025 wakati wakizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kumalizika kwa kikao cha siku cha Baraza la Vyama vya Siasa, kilichofanyika mkoani Morogoro.
Machi 11, 2025 siku moja ya kuanza kwa kikao hicho, ACT Wazalendo kupitia Katibu Mkuu wake Ado Shaibu kiliweka msimamo wa kutoshiriki mkutano kwa madai baraza hilo limekosa uhalali.
Mbali na hilo, Ado alidai uamuzi huo umefikiwa na kikao cha Kamati ya Uongozi Taifa cha ACT Wazalendo, kilichoketi Machi 10, 2025.
“Baraza la Vyama vya Siasa linaloratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini limepoteza uhalali baada ya kushindwa kuwa jukwaa huru la majadiliano,” alisema Ado.
Hata hivyo, wajumbe wa baraza hilo, jana wamekishukia ACT Wazalendo wakikitaka kuheshimu na kutambua umuhimu wa baraza hilo katika kusimamia amani, utulivu na demokrasia.
Katibu Mkuu wa NLD, Hassan Doyo, amesema baraza hilo lina nafasi muhimu katika kusimamia amani na utulivu hasa wakati huu wa kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba, 2025.
“Tunalitazama baraza hili kama chombo cha majadiliano kwa mustakabali wa kisiasa wa nchi yetu. Vyama vinavyopuuza harakati za baraza hili vinapaswa kuelekezwa ili vitambue umuhimu wake,” amesema Doyo.

Aidha, Katibu Mkuu wa DP, Abdul Mluya na Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa na Bunge wa baraza hilo, amesema taasisi hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha mazingira ya kisiasa.
“Baraza limekuwa likihakikisha vyama vya siasa vinapata fursa ya kufanya mikutano ya hadhara na vikao vya ndani, ambavyo awali vilikuwa na vizuizi.
“ACT Wazalendo wanapaswa kutambua kuwa baraza hili ndilo lililopelekea uwepo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, si sahihi kuonyesha dharau kwa baraza na wanachama wake,” amesema Mluya.
Awali, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Ally Khatibu, akisoma maazimio ya kikao hicho amesema ni muhimu kwa vyama vyote kuheshimiwa baraza hilo ambalo lipo kikatiba.
Amesema wakati huu wa kuelekea Uchaguzi Mkuu Baraza lina wajibu mkubwa katika kuhakikisha vyama vinatekeleza wajibu wake kwa Watanzania.
“Tunapokaribia Uchaguzi, ni muhimu kuhakikisha kuwa hotuba na kampeni za kisiasa zinafuata misingi ya staha, bila matusi, kejeli au kashfa,” amesema Khatibu.
Pia, Khatibu amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake katika kuimarisha haki za wanawake na kuwawezesha kiuchumi, kielimu, na katika nafasi za uongozi.