Presha juu ugawaji majimbo | Mwananchi

Dar/ mikoani. Joto la Uchaguzi Mkuu mwaka huu limezidi kupanda na kukoleza maombi ya kugawa maeneo ya uchaguzi ambayo hadi sasa yameyagusa takriban majimbo 14.

Mchakato huo ni kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, inayoipa mamlaka Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) kugawa mipaka ya majimbo ya uchaguzi.

Presha hiyo ilianza kupanda ndani ya vyama, hasa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambako baadhi ya makada wake walianza kampeni za chini chini ama za kujipitisha kwenye majimbo yaliyopo na kusukuma ajenga za kuyagawa mengine ili wapate nafasi za kugombea.

Pia, wakati wa mkutano wa Bunge uliopita kulikuwa taarifa zisizo rasmi kwamba baadhi ya wabunge wako majimboni kuokoa nafasi zao kutokana na taarifa za kuwepo watu wengine wanaojipitisha.

Kwa upande mwingine, pia zipo taarifa zinazohusisha msukumo huo na ushindani baina ya vyama, hali inayotajwa kwa Mbeya Mjini, ambapo Mbunge wa sasa Spika Tulia Ackson anatazamiwa kuvaana na mbunge wa zamani na Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’.

Licha ya wengi wanaotaka majimbo yagawanywe kudai wamekidhi vigezo vya kiutawala, mchambuzi wa masuala ya utawala na utafiti, Donald Kasongi, amesema kinachoendelea kwenye ugawanywaji wa majimbo “ni utashi wa kisiasa zaidi kuliko sababu za kiutawala.”

Amesema kwa kuzingatia ukubwa wa maeneo na idadi ya watu, masuala ambayo ndiyo kigezo cha kugawa majimbo, inaweza isiwe sababu kwenye baadhi ya maeneo ila ni utashi wa kisiasa ambao si rahisi kuukwepa.

Mtafiti huyo amegusia pia  suala la kuiongezea Serikali mzigo wa kuwalipa wabunge ambao wataongezeka, huku baadhi yao wakiwa hawafanyi hiyo kazi ya kuwahudumia wananchi.

Februari 26, 2025 Mwenyekiti wa INEC Jaji Jacobs Mwambegele alitoa taarifa y tume hiyo kuanza kupokea maombi ya kugawa majimbo au kubadili majina kati ya Februari 27, 2025 na Machi 26, 2025.

Sambamba na tangazo hilo, alitaja vigezo vya kugawa majimbo ni idadi ya watu, akisema kwa majimbo ya mjini ni kuanzia wastani wa watu 600,000 na majimbo ya vijijini ni kuanzia wastani wa watu 400,000.

Vigezo vingine ni hali ya kiuchumi ya jimbo, ukubwa wa eneo, mipaka ya kiutawala, uwezo wa ukumbi wa Bunge, jimbo moja kutokuwa ndani ya wilaya au halmashauri mbili, mpangilio wa maeneo ya makazi ya watu yaliyopo, idadi ya wabunge wa viti maalumu wanawake na upatikanaji wa njia za mawasiliano na hali ya kijiografia ya eneo linalokusudiwa kugawanywa.

Baada ya kipenga cha kugawa majimbo kupulizwa, michakato ilianza mara moja katika halmashauri mbalimbali zinazoyagusa takriban majimbo 14, miongoni mwayo yapo ambayo yamehitimisha ngwe yake na kuwasilisha mapendekezo kwenye vikao vya ngazi inayofuata ya kamati za ushauri za mikoa.

Majimbo ambayo yamehusishwa kwenye mchakato huo yapo kwenye mikoa ya Mbeya, Kigoma, Mwanza, Tanga, Simiyu, Dodoma, Shinyanga na Mara.

Ugawaji wa majimbo hayo engapo utapishwa maana yake itakuwa ni kuongeza idadi ya wabunge kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka idadi ya sasa ya wabunge 393 na gharama zinazoendana na ongeko hilo zikiwamo za mishahara na posho.

Juzi gazeti hili liliandika taarifa za Halmashauri ya Jiji la Mbeya kuomba Jimbo la Mbeya Mjini ligawanywe na kuzaa Jimbo la Uyole.

Pia majimbo ya Mbeya Vijijini na Mbarali kila moja linapendekezwa kuzaa jingine jipya.

Hata hivyo, mchambuzi wa siasa za Jiji la Mbeya, Chifu Mwaihojo Mwambipile ameshauri hata kama majimbo yatagawanywa, wananchi wajiandae kuchagua kiongozi mwenye maono badala ya kuchagua chama.

Majimbo mengine ambayo yako kwenye mchakato kama huo ni pamoja na Dodoma Mjini ambalo tayari Baraza la Madiwani limetoa taarifa likibariki mapendekezo ya kugawanywa.

Ofisa uchaguzi wa Jiji la Dodoma, Albert Kasoga amesema mapendekezo yamezingatia mambo yote muhimu ili kutoathiri hali ya kiuchumi ya jimbo moja kutoka kwa linguine na majimbo hayo yaitwe Jimbo la Mtumba (Dodoma Mashariki) na Jimbo la Dodoma Mjini (Dodoma Magharibi).

Majimbo mengine ni Bariadi (Simiyu), Magu (Mwanza), Kilindi na Handeni (Tanga), Ushetu (Shinyanga), Kasulu Vijijini, Muhambwe, Kigoma Kusini na Kigoma Kaskazini (Kigoma); huku jimbo la Ilemela (Mwanza) maombi yake yakiwa wamepelekwa tangu awamu ya tano lakini hayakubaliwa wala kujibiwa.

Akizungumzia mchakati huo, Mkuu wa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, Simon Simalenga, amesema jimbo la Bariadi limekidhi vigezo vya kugawanywa kutokana na idadi ya watu kufikia 644,312 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, idadi inayozidi kiwango cha watu 400,000 kinachopendekezwa kwa jimbo moja la vijijini. 

 “Kwa sasa tunasubiri suala hili liingizwe kwenye kikao cha baraza la madiwani, licha ya kuwa hili suala lilishajadiliwa kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya wilaya, kabla ya huu utaratibu mpya kutangazwa,” amesema.

Kwa Mkoa wa Mara, kikao cha RCC kilichoketi wiki iliyopita kilipitisha ombi la Wilaya ya Serengeti la kutaka jimbo la Serengeti ligawanywe na kuwa majimbo mawili.

Katika kikao hicho kilichoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi pamoja na mambo mengine walikubaliana majimbo hayo yaitwe Serengeti Mashariki na Serengeti Magharibi.

Awali Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Charles Rutonesha alisema hoja za kugawa jimbo hilo zilipitishwa na vikao vya ngazi ya chini ikiwepo kikao cha DCC.

Alisema jimbo hilo lina wakazi zaidi ya 340,000, hali ambayo imekuwa ikileta changamoto za kiungozi kwa mbunge kulingana na jiografia ya jimbo.

Pia, kikao maalumu kilichofanyika katika ukumbi wa Kigoma Makao Makuu ya Halmashauri ya Kasulu, Baraza la Madiwani chini ya Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri, Laurent Poteza iliazimia kugawanywa kwa Jimbo la Kasulu Vijijini ili kuwe na majimbo mawili ya Buyonga na Makele.

Jimbo la Muhambwe wilayani Kibondo pia ilipendekezwa ligawanywe kuwa majimbo mawili ya Muhambwe Mashariki na Muhambwe Magharibi na kuwa makao makuu yakipendekezwa kuwa Kibondo Mjini kwa Jimbo la Muhambwe Mashariki na Kata ya Nyaruyoba kuwa makao makuu ya Jimbo la Muhambwe Magharibi.

Pia, Baraza la Madiwani katika Halmashauri ya Wilaya Kilindi limepitisha mapendekezo ya kuligawa Jimbo la Kilindi na kuzaa Songe na Kilindi.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Kilindi Hashim Mgandilwa alisema katika kupendekeza kikubwa ni kuangalia masilahi ya wananchi ambao ndiyo walengwa katika kupatiwa huduma mbalimbali za maendeleo.

Kwa halmashauri ya Wilaya ya Handeni Mwenyekiti wa Halmashauri, Mussa Mwanyumbu amesema wameshapitisha pendekezo la kupata jimbo la Handeni na kuzaliwa jimbo Jipya la Kabuku.

Baada ya mapendekezo hayo, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Tanga, Jonathan Bahweje amesema anaunga mkono ugawaji wa majimbo mapya, ila Serikali inapaswa kuhakikisha vigezo husika vinazingatiwa katika ugawaji huo, kuwa kuna maeneo ambayo licha ya kukidhi idadi ya watu ila geografia yake haikidhi.

Ametolea mfano wilayani Handeni akisema hakuna sababu ya kuigawa kuwa majimbo mawili na badala yake uangaliwe uwezekano wa jimbo ya Handeni vijijini baadhi ya kata zake zirudishwe Handeni Mjini, ambako wananchi wake wanapata huduma.

Kadhalika, amesema kama inawezekana kugawiwa Kilindi na Muheza yagawanywe kwa kuwa maeneo yake ni makubwa sana na wananchi wanachukua muda mrefu kutafuta huduma makao makuu.

Mwenyekiti wa Chama cha National League for Democracy (NLD), Doyo Hassan Doyo amesema ugawaji wa majimbo ni jambo zuri na linasaidia kusogeza huduma kwa wananchi karibu.

Jambo ambalo amesisitiza kufanyika ni kuzingatia maeneo yote ambayo wananchi wanatembea umbali mrefu kwenda kutafuta huduma makao makuu, uangaliwe utaratibu wa kusogezwa huduma hizo karibu.

“Mipaka ya utawala inachagiza maendeleo kwenye jamii, mfano mwananchi kutembea kilomita 75 kwenda kutafuta huduma sio sawa, hivyo ugawaji huo wa mipaka au majimbo utaweza kuchagiza maendeleo ya wananchi lakini pia kupata huduma karibu,” amesema Doyo.

Aidha, amesema ugawaji uzingatie majina ambayo ni asili kuliko kubuni mapya, kwani wapo watu, maeneo na viongozi maarufu ambao wanastahili kuenziwa kwa njia hiyo.

Related Posts