PIC yaridhishwa na utekelezaji wa mradi wa HEET Udom

Dodoma. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) imesema imeridhishwa na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa maabara za sayansi na madarasa ya masomo ya kada ya ardhi kwenye Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).

Mradi huo utakaowezesha kupanua wigo wa udahili wa wanafunzi kwenye chuo hicho, unatekelezwa chini ya Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).

HEET ni mradi unaotekelezwa kwa miaka mitano kuanzia Mei 2021 hadi Juni 2026, kwa fedha za mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia (WB) utakaotekelezwa kwa zaidi ya Sh972 bilioni.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Augustine Vuma ameyasema hayo leo Alhamisi Machi 13, 2025 baada ya wajumbe wa kamati yake kutembelea mradi huo.

“Tumekagua ujenzi wa majengo makubwa mawili kwa kweli tumeridhishwa na jinsi mradi unavyoendelea katika Chuo Kikuu cha Dodoma, usimamizi ni wa hali ya juu sana wa wizara pamoja na menejimenti ya chuo kikuu chenyewe,”amesema.

Amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutafuta fedha kwa ajili ya kuboresha na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na chuo kikuu kwa usimamizi wa karibu wa mradi huo.

Amesema wanaamini kukamilika kwa mradi huo kutaboresha kwa kiasi kikubwa elimu ya juu nchini Tanzania na hivyo kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga amesema Udom katika mradi huo imepata gawiwo la Dola za Marekani milioni 23.

Amesema fedha hizo zitatumika katika ujenzi wa maabara za kisasa za sayansi, madarasa ya kuanzisha mafunzo ya kada za ardhi na ujenzi wa kampasi mpya mkoani Njombe.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) wakitembelea mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).

Amesema miradi yote miwili ya ujenzi wa maabara na madarasa inatekelezwa kwa gharama ya zaidi ya Sh24 bilioni.

Makamu Mkuu wa Udom, Profesa Lughano Kusiluka amesema miradi hiyo ina tija kubwa kwao kwa sababu bado wanahitaji miundombinu mbalimbali kwa ajili ya kuongeza udahili na hasa katika maeneo ya sayansi na uhandisi.

“Miundombinu tuliyokuwa nayo ilikuwa haitoshi kutokana na ongezeko la wanafunzi chuoni, kwa hiyo tunaishukuru Serikali yetu chini ya uongozi wa Rais Samia kwa kuendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika chuo chetu,”amesema.

Amesema maabara zinatarajiwa kutanua wigo wa wanafunzi kujifunza ambapo kwa wakati mmoja zitachukua wanafunzi zaidi ya 2,000 kwenye madarasa yanayojengwa katika mradi huo utakaokamilika Desemba mwaka huu.

Related Posts