Dar es Salaam. Watumiaji wa bidhaa wana haki ya kudai na kufungua shauri la kudai fidia wanapobaini zile walizopatiwa haziendani na walichoahidiwa, huku wakiwa na wajibu wa kupata maelezo ya awali kuzihusu.
Hayo yameelezwa kwa nyakati tofauti leo Machi 13, 2025 na wadau wa mabaraza ya watumiaji wa huduma katika mjadala wa Mwananchi X Space ulioandaliwa na Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa kushirikiana na Jukwaa la Watumiaji Tanzania, ikiwa ni sehemu ya kuelekea maadhimisho ya siku ya haki ya watumiaji, ukijadili mada isemayo: “Wajibu wa wadau katika kuimarisha haki za mtumiaji kwa maisha endelevu.”
Maadhimisho hayo yatafanyika machi 15, 2025.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Watumiaji wa Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA CCC), Innocent Kyara amesema ziko kanuni zinazoonyesha ni kwa namna gani abiria anaweza kufidiwa ikiwa ndege itachelewa kufanya safari na kusababisha hasara kwake moja kwa moja.
“Niwaombe abiria kuanza kuchukua hatua ikiwa wameathirika kwa namna yoyote kwa sababu taratibu zipo ikiwamo kudai fidia. Kudai fidia inaweza kuwa chachu ya mashirika kuboresha huduma ili kukwepa kulipa fidia kwa abiria wao kila mara,” amesema.
Amesema kudai fidia si kwa kuchelewa kwa ndege pekee, hata begi likiharibika au vitu kupotea abiria anapaswa kudai fidia ili kurejesha hali iliyokuwapo kabla mtumiaji hajapata madhara hayo.
Kyara amesema wakati mwingine kuchelewa kwa safati za ndege huwa na sababu mbalimbali, ikiwamo suala la usalama. Ametoa mfano endapo ikibainika ndege haiko salama kuruka kutakuwa na ucheleweshaji na hilo likitokea kwa ndege moja itasababisha kuvurugika kwa ratiba nzima ya shirika.
“Tunachopigania zaidi ni namna mashirika ya ndege yanavyohudumia wateja hili linapotokea, wakati mwingine kuchelewa kwa ndege hakuepukiki, hivyo ni lazima mashirika haya yahudumie vizuri abiria wake ikiwemo kutoa taarifa kuwa hilo litakuwa kwa muda gani na taarifa zina ukweli gani na si kusema kwa dakika 30 zikifika unaongeza tena na tena,” amesema.
Awali, Mhariri wa Uchumi wa Mwananchi, Ephraim Bahemu amesema mtumiaji ana haki ya kudai na kufungua shauri la kudai fidia pindi bidhaa aliyopewa haiendani na kile alichoahidiwa.
Amesema mtumiaji pia ana wajibu wa kupata maelezo ya awali kuhusu bidhaa.
“Katika hili suala la kutoa elimu ni muhimu kwa sababu siyo jamii kubwa inajua haki zake, katika nchi yetu bado kuna tabaka halijui haki zake na wapi pa kuzipata, lakini wengine hawana nia ya kuzifuatalia hadi pale wanapopata shida.”
“Ni muhimu wadau kutoa elimu kuwaeleza watumiaji au wananchi kujenga utamaduni wa kufuatilia haki zao na kutimiza wajibu pindi wanapopata huduma fulani. Hili ni muhimu kwa sababu itapunguza migogoro na sintofahamu na kuleta maisha endelevu,” amesema.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduna za Maji na Mafuta (Ewura CCC), Stella Lupimo amesema ucheleweshaji wa kuunganishiwa umeme wateja wapya ni moja ya changamoto inayolalamikiwa na wengi wanaohitaji huduna hiyo.
Hilo ni kutokana na huduma kuchukua muda mrefu tofauti na mkataba wa uhudumiaji wateja unavyotaka.
Amesema kwa kawaida mtu anayetaka kuunganishiwa umeme anatakiwa kupata mkataba wa huduma kwa wateja ili ajue haki zake ni zipi, lakini mara zote mtu anapohitaji huduma hiyo anakuwa na hamu ya kuunganishwa umeme pekee.
“Mara zote tumekuwa tukiwashauri wawasiliane na Tanesco (Shirika la Umeme Tanzania) ili kujua changamoto inayowakabili hadi mteja kucheleweshewa kuunganishiwa umeme,” amesema.
Kukatika umeme bila taarifa ni changamoto nyingine inayoripotiwa zaidi na wateja, ikiwa ni dharura au kwa kupangwa, huku wakitaka taarifa zitolewe. Amesema suala hilo angalau siku hizi linafanyiwa kazi.
“Changamoto nyingine katika umeme ni wateja kuhamishwa madaraja bila taarifa, mtu anatolewa daraja labda la D1 kwenda T1, baraza limekuwa likielimisha watu ni kwa kipindi gani mtu anaweza kuhamishwa daraja hilo,” amesema.
Katika eneo la mafuta, Stella amesema wakati mwingine inapofika muda wa kutangaza bei mpya wauzaji wamekuwa wakitengeneza uhaba wa makusudi ili kujinuifaisha jambo ambalo limekuwa likishughulikiwa kwa wakati.
Katibu Mtendaji wa Latra CCC, Daudi Daudi amesema moja ya changamoto inayolalamikiwa na watumiaji wa daladala ni watoa huduma kukatisha safari, hasa muda ambao kuna uhitaji mkubwa wa usafiri.
Jambo hilo amesema lilikwenda sambamba na baadhi ya watoa huduma kulipisha nauli zaidi ya ile iliyowekwa na mamlaka husika.
“Pia, malalamiko mengi yanakuja wakati ambao mtu anapotaka kusafiri anapata daladala usiku sana lakini akiingia wanatoza nauli ambazo wameamua wao uhalisia ni Sh700 wao wanatoza Sh1,000, hivyo hili kila linapowasilishwa tunalipeleka kwa mamlaka husika. Tunashukuru wamekuwa wepesi wa kufanyia maamuzi na muhusika amepewa stahiki zake,” amesema.
Malalamiko mengine amesema yalikuwa ya watumiaji wa Reli ya Kisasa (SGR) ambao upya wa huduma ulifanya wengi kulalamika kwa sababu walikuwa wakikutana na makatazo ambayo hawayafahamu au kuwa na vitu ambavyo vinatakiwa.
“Hili pia, tulikutana na watoa huduma katika kikao cha ndani walizichukua na kuongeza matangazo juu ya namna gani mtu anapaswa kusafiri na katika namna gani,” amesema.
Amesema moja ya jukumu wanalolifanya ni kutoa elimu kwa watumiaji wa usafiri wa ardhini kuhusu kulinda mazingira.
“Huu ni wajibu wanapokuwa safarini, ni wajibu wao wa kutunza mazingira ndani na nje ya chombo, pamoja na maeneo yote yanayozunguka mnyororo mzima wa safari. Hapa ninamaanisha watakapofika vituoni kutunza mazingira au watakapokuwa njiani kutunza mazingira,” amesema.
Amesema hilo pia linawahusu watoa huduma wanaotakiwa kuhakikisha chombo wanachotumia kinapopata hitilafu njiani ni jukumu lao kulinda mazingira.
“Kumwaga kemikali kama mafuta ni uharibifu wa mazingira badala yake wanatakiwa watumie sehemu maalumu zilizotengwa kwa ufundi,” amesema.
Amewataka wasafiri ‘kutokuchimba dawa’ porini wakiwa safari kwa sababu huo ni uharibifu wa mazingira, badala yake wanapaswa kufuata utaratibu uliowekwa wa maeneo maalumu yaliyoanishwa kupata huduma za kijamii.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Mawasiliano Tanzania (TCRA CCC), Mary Msuya amesema baraza hilo limekuwa mstari wa mbele kutoa elimu kwa watumiaji ili kukabiliana changamoto mbalimbali, ikiwemo utapeli wa mitandao.
Msuya amesema watumiaji wamekuwa wakikumbana na utapeli katika simu hasa kutumiwa ujumbe wa kitapeli kupitia sms au barua pepe, lakini pia kuna changamoto nyingine ya uelewa wa watumiaji.
“Sekta inakua kwa haraka tofauti na uelewa wa watumiaji, hivi sasa kila siku simu za mkononi zinatoka mpya,” amesema.
Mwakilishi wa shirika lisilo la kiserikali la Foundation for Civil Society (FSC), Sarah Masenga amesema malengo ya taasisi hiyo ni kuhakikisha wadau na watumiaji wanapata haki zao ili kuboresha maisha yao.
FSC ni asasi ya kiraia inayojishughulisha na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa miaka 20 kwa kutatua changamoto za wananchi.
Amesema katika kipindi cha miaka 20 ya utekelezaji wa miradi wamewafikia wananchi milioni 31 katika miradi ya kupinga ukatili wa kijinsia, uwezeshaji wa kiuchumi wanawake na watu wenye ulemavu, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
“Kwa ufadhili wa Trademark Afrika, tunatekeleza mradi wa miaka mitatu wenye lengo la kutoa elimu kwa mlaji, kupitia ufadhili tumeona ni vyema tukashirikiana na mabaraza ya watumiaji, kutoa elimu kwa wananchi na asasi za kiraia.
“Kikubwa tunachotaka kuona watu wakijua haki zao, wanaweza kujua mfumo wa kutoa malalamiko katika mabaraza na majukwaa. Wanaweza kutoa malalamiko yao kuhusu huduma au changamoto kuhusu mawasiliano na usafiri,” amesema.
Masenga amesema mkakati wao ni kuwafikia watumiaji angalau asilimia 60 katika mradi hadi utakapofika mwisho ili wananchi waelewe na kuyafanyia kazi.