Ukiwa na kisukari si hukumu ya kifo, bali ni hali ya kiafya inayohitaji usimamizi wa makini ili kuendelea kuishi maisha yenye afya na furaha.
Wagonjwa wa kisukari wanaweza kudhibiti ugonjwa huu na kuishi vizuri kwa kufuata mtindo sahihi wa maisha, kutumia dawa ipasavyo na kupata elimu sahihi kuhusu hali yao.
Ukigundulika kuwa una ugonjwa wa kisukari, ni muhimu kujua ni aina gani ya kisukari, kwani hilo husaidia kuchukua hatua sahihi za kudhibiti afya yako.
Kuna aina kuu tatu za kisukari: kisukari aina ya kwanza inayotokea pale kongosho linaposhindwa kuzalisha insulini kabisa. Wagonjwa wa aina hii wanahitaji insulini kila siku kwa maisha yao yote na hugundulika katika umri mdogo.
Kisukari aina ya pili. Hapa mwili hauzalishi insulini ya kutosha na mara nyingi hudhibitiwa kwa lishe bora, mazoezi, na dawa.
Kisukari cha mimba. Hiki hutokea wakati wa ujauzito na huisha baada ya kujifungua, lakini kinaweza kuongeza hatari ya kupata kisukari aina ya pili baadaye.
Kudhibiti viwango vya sukari ni jambo muhimu kwa mgonjwa wa kisukari. Njia bora za kufanya hivyo ni kupima sukari mara kwa mara ili kufuatilia mwenendo wake, kula mlo sahihi. Epuka wanga zisizo na nyuzinyuzi, tumia vyakula vya asili kama mboga, matunda na nafaka zisizokobolewa, kufanya mazoezi mara kwa mara.
Fuata ratiba ya dawa. Ikiwa unatumia insulini au dawa zingine, hakikisha unazifuata kama inavyoelekezwa na daktari.
Kisukari kisipodhibitiwa vizuri kinaweza kusababisha madhara kama upofu, matatizo ya figo, shinikizo la damu au vidonda visivyopona. Njia za kuzuia madhara haya ni kupima shinikizo la damu na lehemu mara kwa mara. Kuhakikisha miguu ni safi na kavu kila siku, kuepuka majeraha madogo ambayo yanaweza kuwa makubwa, kufanya uchunguzi wa macho na figo mara kwa mara ili kugundua matatizo mapema.
Kisukari sio tu ugonjwa wa mwili, Unaweza pia kuathiri hisia na hali ya kisaikolojia. Ni muhimu kuwa na mtazamo chanya, kujiunga na vikundi vya usaidizi, kukutana na watu wenye hali kama yako huongeza motisha na maarifa.
Shirikiana na familia na marafiki na wafahamishe rafiki na ndugu kuhusu hali yako ili wakusaidie vyema.
Epuka msongo wa mawazo, kwani unaweza kukufanya kushindwa kudhibiti viwango vya sukari. Hivyo ni muhimu kutafuta njia za kupunguza hali hii kwa kusali, kusikiliza muziki au kufanya mazoezi.
Kuishi na kisukari si jambo gumu iwapo utachukua hatua sahihi za kudhibiti afya yako. Ukifuata lishe bora, kufanya mazoezi, kudhibiti viwango vya sukari, na kupata usaidizi wa kimwili na kisaikolojia, unaweza kuishi maisha marefu na yenye afya.