Baadhi ya watu wanafunga bila kuelewa hukumu zake, jambo linalowafanya waingie katika makosa kwa sababu ya kutokujua na hivyo kupunguza thawabu za Saumu zao au kuathiri ukamilifu wake.
Hivyo inampasa Muislamu anayetaka alipwe thawabu timilifu, ajifunze vizuri ibada yoyote kabla ya kuianza, ili aweze kumuabudu Allah Mtukufu kwa ujuzi, maarifa na ufahamu sahihi.
Mtume (Rehema na amani zimshukie) amesema: “Kuweni na haya (aibu) ya kweli kwa Allah.” Maswahaba wakauliza: “Ewe Mtume wa Allah! Sisi tunayo haya, na tunamshukuru Allah kwa hilo.” Akawaambia: “Sio hiyo, lakini haya ya kweli kwa Allah ni kuhifadhi kichwa na viungo vingine vilivyokuwa jirani na kichwa, kulihifadhi tumbo na viungo vingine vilivyokuwa jirani na tumbo…”
Mfungaji anapaswa kuuchunga ulimi wake na usengenyaji, fitna, uongo, kusingizia watu, uzushi, upuuzi na matusi.
Macho yanapaswa uyaepushe na kuangalia mambo aliyoyaharamisha Allah Mtukufu. Na ikiwa itatokea kwa bahati mbaya basi mtazamo wa kwanza utakuwa si wa makusudi, na mtazamo wa pili na kuendelea utakuwa wa kudhamiria.
Mtume amesema: “Na ulilinde tumbo.” Hii inamaanisha kuwa Muislamu ajiepushe na kula au kunywa vitu haramu, kama vile riba, kula mali za watu kwa njia isiyo halali, kula au kunywa kitu chochote cha haramu, tumbo linapaswa kuingiza tu kilicho halali.
Sehemu za siri zinapaswa kulindwa dhidi ya maovu kama vile: uzinifu, mapenzi ya jinsia mojai, kujichua au kwa kutazama picha chafu n.k.
Muislamu hapaswi kutumia miguu yake kwenda mahali penye maasi au kufanya kitendo chochote cha haramu.
Mikono inapaswa kutumika kwa mambo halali pekee, bila kudhulumu watu, kuandika au kufanya jambo lolote la haramu.
Moyo nao unapaswa kulindwa dhidi ya maradhi ya kiroho kama vile husuda (wivu wa chuki), chuki, uhasama, kiburi, kujiona, kutafuta umaarufu kwa nia ya kujikweza, choyo, ubinafsi, ubahili n.k.
Ubadhirifu na matumizi kupita kiasi
Ubadhirifu ni kupitiliza mipaka katika jambo lolote analofanya mtu, ingawa mara nyingi linahusiana na matumizi ya mali. Watu wengi huangukia katika ubadhirifu, hasa katika mwezi wa Ramadhani, kwa kutumia pesa nyingi katika chakula na vinywaji, na hatimaye kutupa kilichobaki majalalani au mitaani.
Katika Ramadhani, tabia hii ya israfu hujitokeza wazi, ambapo watu huandaa aina nyingi za vyakula, vinywaji, matunda na mboga, lakini baada ya kula, kilichobaki hutupwa majalalani na kuchanganyika na taka.
Uislamu umeweka mwongozo wa kula na kunywa kwa Muislamu. Mtume wa Allah amesema: ” Inatosha kwa mwanadamu kula kichache tu ili kuimarisha uti wa mgongo wake. Na ikiwa hawezi kuacha kula zaidi, basi (agawanye tumbo lake) sehemu tatu: Theluthi moja iwe ya chakula, theluthi moja ya kinywaji, na theluthi moja ya pumzi (asile hadi anashindwa kupumua)”
Wakati wa Ramadhani, baadhi ya wanaume huwafanya wake zao au wafanyakazi wao wa nyumbani wapike vyakula vingi na vinywaji kwa muda mrefu, kuanzia mchana hadi usiku.
Hili lina madhara ya mwanamke au mfanyakazi wa nyumbani hukosa muda wa kupumzika na kushindwa kufanya ibada nyingine za utiifu wa Mola wake kwa ufanisi, kama vile kuswali sala za faradhi kwa wakati na Tarawehe.
Baadhi ya watu hulala na kuiacha Swala ya Alfajiri, wengine huiswali kabla ya wakati wake, na wengine huiharakisha bila utulivu. Hali hii ni hatari kwa mtu aliyefunga, kwani huenda funga yake ikawa ni kushinda na njaa na kiu tu.
Kulala mchana kwa muda mrefu sana ni kinyume na kanuni za Allah Mtukufu, ambaye ameufanya usiku kwa ajili ya kupumzika na mchana kwa ajili ya shughuli za utafutaji maisha.
Mtu hupoteza thawabu za kufanya ibada katika mchana wa Ramadhani, ambao ni muda wenye thamani, kwa sababu hata kujitafutia kipato cha halili ni ibada.
Watu wengi hupoteza muda wao kwa: Mazungumzo ya upuuzi na yasiyo na manufaa vijiweni na katika baraza za kahawa.
Baadhi ya watu hujishughulisha na mambo yasiyo na manufaa na kupuuza kusoma Qur’an, jambo ambalo linawanyima fadhila zake.
Sababu kuu zinazowafanya waache kusoma Qur’an ni kulala kupita kiasi, kuingia katika mambo ya upuuzi na michezo isiyo na faida kama vile kucheza karata, zumna, bao, kete n.k.
Baadhi ya watu hawaombi dua wanapofuturu au wakiwa katika saumu, hali ya kuwa dua ni ibada yenye nafasi kubwa. Kupitia dua, mja huonesha unyenyekevu na unyonge wake kwa Allah Mtukufu,. Miongoni mwa nyakati bora za kukubaliwa kwa dua ni wakati wa saumu.
Mtume wa Allah amesema: “Dua za watu watatu hazirudishwi (patupu): kiongozi mwadilifu, mfungaji mpaka afuturu, na aliyedhulumiwa.”
Baadhi ya watu huchelewa kwenda msikitini kwa ajili ya kufuturu, jambo ambalo linawafanya wasali Magharibi kwa haraka au kwa kuchelewa. Mtume wa Allah alikuwa akifuturu kwa tende chache au maji kidogo kisha anaswali kabla ya kula chakula kingine.
Baadhi ya watu hawaendi kuswali Tarawehe msikitini baada ya Swala ya Isha, na wengine hata hawaswali nyumbani. Kuswali Tarawehe na imamu ni bora zaidi kuliko kuswali peke yako, kwani Mtume wa Allah aliiswali na maswahaba wake kwa siku tatu, kisha akaacha kutoka kuswali nao pamoja kwa hofu ya kuwajibishwa kwa Sala hiyo.
Baadhi ya maimamu huswali Tarawehe kwa haraka sana kiasi kwamba: Hawapatii rukuu na sijida utulivu unaostahiki. Wanakosa unyenyekevu. Wanasoma Qur’an kwa muunganiko wa haraka hadi kupoteza maana yake.Tabia hii inasababishwa na kuutaka kuimaliza Sala haraka ili wajiondoe kwenye jukumu.