Dar es Salaam. Kutokana na utafiti kubaini wakazi wa mijini kuwa na unene kupita kiasi ikilinganishwa waishio vijijini, wataalamu wa lishe na afya ya binadamu wameeleza aina ya maisha wanayopaswa kuishi wakazi wa mijini.
Wataalamu hao wanaeleza hayo wakati uhalisia wa maisha ya wakazi wa mijini yakionyeshwa kwenye Ripoti ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria (TDHS) wa Mwaka 2022.
Utafiti huo unaonyesha asilimia 50 ya wanawake wanene wanaishi maeneo ya mijini huku asilimia 28 wakiwa vijijini.
Sio kwa wanawake tu bali kulingana na utafiti huo, kuna asilimia 26 ya wanaume wanene mijini ikiwa ni mara mbili ya wanaume wanene vijijini.
Ripoti hiyo imebaini wanawake hunenepa zaidi umri unavyozidi kuongezeka ikionyesha karibu nusu ya wanawake wenye miaka 40 hadi 49 ni wanene, wakati ni robo pekee wenye miaka 20 hadi 29 ndio wanene.
Mtaalamu wa lishe, Maria Samlongo anafafanua unene kupitia kiasi, hutokea pale uwiano wa uzito wa mtu na urefu (BMI) unapoanzia 25 na kuendelea.
“Mtu anapata unene kupita kiasi kutokana na kiasi kikubwa cha mafuta mwilini kinapoongezeka na hii inatokea pale kiasi kikubwa cha nishati lishe, kinapoingia mwilini kuliko kiasi ambacho mwili unahitaji.
Vyakula vyenye kiasi kikubwa cha nishati lishe ni vile vyenye asili ya wanga, sukari na mafuta,”anasema.
Maria anasema vyakula hivyo vikitumika bila kufuata kanuni za lishe bora, vinaweza kusababisha mtumiaji kuwa na uzito uliozidi kiasi au uliokithiri.
Maria anasema kwa watu wanaoishi mijini wanashauriwa kutumia vyakula aina mbalimbali kwa kuzingatia kazi wanayofanya, hali ya kiafya, umri na jinsia.
Kwa wanaoishi mjini, Maria anasema wanapaswa kuzingatia kanuni bora za lishe ikiwa ni pamoja na kuepuka matumizi ya sukari, kupunguza matumizi ya vyakula vilivyopikwa kwa mafuta mengi, kuepuka matumizi ya vilevi na tabia bwete.
Maria anasema ni muhimu kuongeza matumizi ya mboga za majani na matunda pamoja na mazoezi ya viungo vya mwili na kupunguza msongo wa mawazo.
“Kama utakula chakula kitokanacho na wanga kiendane na shughuli ambazo mtu anafanya, yule aliye ofisini hawezi kula sawa na mbeba mizigo sokoni,
Unapotumia kiasi kikubwa cha wanga kuliko mahitaji yako basi mwili hubadilisha nishati hiyo kuwa mafuta na kusababisha ongezeko la uzito uliozidi,”anasema.
Maria anasema mtu mnene kupita kiasi anatakiwa kupata ushauri kutoka kwa wataalamu wa lishe ili aweze kuchagua lishe bora na itakayomsaidia kuweza kupunguza uzito bila kupata matatizo.
Mtaalamu huyo wa lishe amesema mtu anapokuwa na uzito kupita kiasi anajiweka katika hatari ya kupata magonjwa hasa yale yasiyo ya kuambukiza mfano kisukari aina ya pili, shinikizo la juu la damu, kiharusi, mafuta mengi kwenye damu pamoja na kupunguza ufanisi katika utendaji kazi,
Kama utahitaji kupunguza uzito, Maria anasema inahitaji mtu kuwa na subra na sio kutaka matokeo ya haraka, pamoja na kutenga muda kwa ajili ya kufanya mazoezi ya viungo angalau dakika 30 kwa siku.
Daktari kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya Dk Ernest Winchislaus, anasema sababu ya watu kunenepa kupita kiasi, ni mfumo wa mwili wa kujilinda dhidi ya njaa.
“Mwili umeundwa kwa namna ambavyo utajilinda dhidi ya njaa,ukitaka kupunguza uzito mwili hujaribu kuhifadhi nishati kwa kupunguza kiwango cha metaboli, hali inayofanya iwe vigumu kupunguza na kudumisha uzito wa mwili.
Hii ndiyo sababu wengi wanaojinyima kula huishia kurejea kwenye uzito wa awali au hata kuongezeka zaidi,”anasema.
Mbali na hilo mtaalamu huyo anasema yapo baadhi ya ya matatizo ya akili kama vile mfadhaiko na msongo wa mawazo, ambayo husababisha kuongezeka kwa uzito.
Anasema mtu mwenye mfadhaiko anaweza kupata faraja kwa kula vyakula vyenye sukari nyingi na mafuta, hivyo kuongeza uzito wake bila kufahamu.
Pia mabadiliko ya kimwili Dk Winchislaus, anasema huchangia hali hiyo kwani maisha hupitia hatua mbalimbali kama vile ujauzito, utu uzima wa mapema, magonjwa na matumizi ya dawa ambazo husababisha kuongezeka kwa uzito.
“Wanawake hupata ongezeko la uzito wakati wa ujauzito na mara nyingine hupata ugumu wa kuupunguza baada ya kujifungua,”anasema.
Kulingana na tafiti, Dk Winchislaus anasema vinasaba huchangia kati ya asilimia 40 hadi 70 ya uwezekano wa mtu kupata unene kupita kiasi.
“Ikiwa mzazi mmoja au wote wawili ni wanene, kuna uwezekano mkubwa watoto wao pia watakuwa na tabia ya kuongezeka uzito haraka,”anasema.
Jambo lingine ni unyanyapaa na ubaguzi wa kijamii, Dk Winchislaus anasema watu wenye unene uliopitiliza mara nyingi hukumbwa na ubaguzi wa kijamii na unyanyapaa.
“Mtu mnene anaweza kusita kwenda kufanya mazoezi kwa sababu anaogopa kudhalilishwa, hali inayofanya iwe vigumu kwake kupunguza uzito,’’ anasema.
Dk Daud Emmanuel anasema mtu akipunguza asilimia tano pekee ya uzito wake, hupata matokeo ya haraka hivyo kwa mtu anayetaka kupunguza uzito, lazima azungumze na wataalamu.
“Mtu akitaka kupunguza uzito lazima azunguzme na wataalamu ndipo ashauriwe na kuweka malengo. Pia lazima afuatilie hali yake ya ulaji na ufanyaji wa mazoezi kama atakavyoshauriwa.
Dk Daud anasema kama kuna vitu humfanya mtu kula sana vyakula kama msongo wa mawazo, kujumuika na makundi mbalimbali yanayokula, ni lazima mhusika avidhibiti.
Mtaalamu huyo anasema watu huanza vyema kudhibiti unene wao, lakini baadaye hushindwa.