NYOTA wa kimataifa wa Tanzania anayeshikilia rekodi ya kucheza mechi nyingi akiwa na timu ya taifa, Taifa Stars, Erasto Nyoni anayeitumikia Namungo kwa sasa, amekataa kushuka na timu hiyo akisema licha ya kuwa na hali mbaya msimu huu, lakini bado wana nafasi ya kujisahihisha.
Namungo iliyopanda daraja msimu wa 2019-2020 kwa sasa ipo nafasi ya 12 katika msimamo baada ya kucheza mechi 23 ikikusanya pointi 23 ni wastani wa kukusanya pointi moja moja katika kila mchezo imefunga mabao 16 ikiruhusu nyavu zao kutikiswa mara 28.
Akizungumza na Mwanaspoti, Nyoni alikiri ni kweli wana kibarua kigumu cha kuipigania Namungo ili kujihakikishia kucheza msimu ujao baada ya kuondolewa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho (FA) kwa kufungwa mabao 3-0 na Kagera Sugar mapema wiki hii, ila bado haoni kama wanashuka.
“Tumepoteza nafasi moja ya kucheza Kombe la Shirikisho, hivyo kwa sasa nguvu zote tunazihamishia Ligi Kuu ambayo nakiri tumekuwa na msimu mgumu sana na hatupo kwenye nafasi nzuri tunahitaji kupambana zaidi ili kujihakikishia kucheza ligi msimu ujao,” alisema Nyoni na kuongeza;
“Licha ya changamoto kubwa iliyo mbele yetu ya kukabiliana na ugumu wa wapinzani, tumejipanga vya kutosha kuipambania Namungo ifikie malengo ya kubaki Ligi Kuu msimu ujao.”
Nyoni alisema kwamba wanaamini wamekuwa kwenye hali mbaya kutokana na ugumu wa ligi ya msimu huu, lakini wanajipanga kusaka matokeo mazuri kwa mechi saba zilizosalia kabla pazia halijafungwa.
“Unajua hii michezo ya mwishoni ndiyo imetukwamisha, tulipanga kupata matokeo mazuri, lakini ndiyo hivyo wapinzani nao wameonyesha ugumu wao, ligi imekuwa ngumu msimu huu, kila timu inataka kufanya vizuri.
“Lakini tunaamini tutasalia katika Ligi kwa msimu ujao, hatuna hofu kuhusiana na hilo, tunapambana, tunajipanga, tunaweka sawa kikosi kuhakikisha hatupotezi mchezo kwenye mechi zilizobaki na tunaamini msimu ujao tutaendelea kuwepo,” alisema Nyoni aliyewahi kuwika Rolling Store, kisha kusajiliwa Vital’O ya Burundi kabla ya kutamba na Azam na Simba, huku akishikilia rekodi ya kuitumikia Taifa Stars katika mechi 107 tangu 2006-2021 akiwa kinara wa kuitumikia Tanzania kwa mechi nyingi zaidi kwa miaka 15.