KONA YA WASTAAFU: Nyongeza ya Pensheni ya wastaafu inapooteshwa mbawa!

Oktoba 2024, iliyopita, siri-kali ilijikanyaga katika kile ilichookita ni kumsaidia mstaafu wake wa Kima cha Chizi kuweza kukabiliana na hali ngumu ya maisha iliyokuwa ikimkabili.

Ilimtangazia mstaafu huyo nyongeza ya pensheni ya Sh50,000 ambayo ukiongeza na ile laki moja kwa mwezi aliyokuwa akipata kwa miaka 21 nyuma, angekuwa sasa akipata Sh150,000.

Siri-kali haikulazimishwa na yoyote. Labda tu ni baada ya kilio cha miaka 21 cha wastaafu hao cha kuomba nyongeza ya pensheni na ushauri wa wananchi wengi waliokuwa wakiandika ujumbe wao hapa wakiitaka siri-kali iwasaidie kweli wastaafu kwa kuwaongeza pensheni yao ya mwezi maana ni ndogo,  hatimaye siri-kali kukubali kuwapoza wastaafu hao kwa Sh50,000!

Wastaafu tukadhani kama siri-kali ilikuwa ikiweza kumlipa mwakilishi wa wananchi shilingi…mama wee… milioni 14 kwa mwezi, rudia kwa mwezi, isingeshindwa kumlipa mstaafu wake wa kima cha chini cha mshahara pensheni japo Sh300,000 tu kwa mwezi kama kweli ilikuwa inataka kumuwezesha mstaafu huyo kukabiliana na hali ngumu ya maisha, akisubiri kuelekea Kinondoni ambako wote tutakwenda!

Mstaafu wetu anajikuta akiomba kimoyomoyo siri-kali ibadilishe mishahara kwa mwezi tu, wawakilishi walipwe Sh150 000 kwa mwezi kama wastaafu wanavyolipwa na wastaafu walipwe milioni 14 kwa mwezi isiyokatwa kodi, kama wawakilishi wanavyolipwa.

Anaamini kuwa hapo ndipo siri-kali itakapojua maana halisi ya kumuwezesha mstaafu huyu aliyeijenga nchi mpaka kufikia mahali pa watu kulipana Sh14 milioni kwa mwezi huku wastaafu wa nchi wakiambulia Sh110,000 kwa mwezi, huku wote wakitakiwa wagawane sawa bin sawa keki ya Taifa.

Mstaafu wetu anajikuta akilazimika kujiuliza hasa kama nchi hii ni maskini kweli au kuna kikundi cha watu kinafanya kila kiwezacho ili nchi ionekane maskini na zaidi uonekane kwa wastaafu tu huku nchi ikiweza kuwalipa wawakilishi.

Ndio, umaskini wa nchi hii ni wa kuchonga kwa wastaafu wa kima cha chini tu lakini siri-kali inaweza kununua ma v8 ya bei mbaya kwa mawaziri wake hadi wakuu wa wilaya wakati wangeweza  kununua Toyota ‘double cabin’ za bei  rahisi, huku wakiweza kuwalipa wenza wa waheshimiwa, wasiokuwa wastaafu, pensheni ya milioni kwa mwezi wakati Sh50,000 tu ya wastaafu inaelekea kuwa ‘santakarawe’ ya watu fulani.

Inashangaza na kumuumiza mno mstaafu. Amekaa miezi mitatu akitegemea kuwa mwisho wa Januari, kwa mujibu wa ahadi ya siri-kali, pensheni yake sasa itakuwa Sh150,000 badala ya Sh100,000 aliyokuwa akipokea kwa miaka 21 tangu yule Muungwana wa Msoga alipopandisha pensheni yao bila kuwataka wakae miezi mitatu kwanza kabla ya kuipata, kama hawa!

Mwisho wa Januari umefika na wastaafu wa kima cha chini wamejikuta wakipokea pensheni ‘mpya’ ya Sh110,000, badala ya Sh150,000 walizoahidiwa kwa mbwembwe na siri-kali miezi mitano iliyopita.

Inamuumiza mstaafu kuona kila mtu ameuchuna kimyaa, sio  waziri aliyetangaza nyongeza hiyo, sio wabunge, sio waheshimiwa wa vibubu vya akiba ya wafanyakazi sio wasemekanao kuwa wanaharakati wala sio vyama mbadala vya wananchi!

Wote wako kimya, kama vile mstaafu kuahidiwa na siri-kali kupata pensheni ya Sh150,000 baada ya miezi mitatu lakini akaishia kupata Sh110,000 ni jambo la kawaida tu! Hakuna anayehoji Sh40,000 imekwenda wapi?

Je imeunganishwa kwenda kununua ngombe 400 kutekeleza sera ya ubwabwa wakati mstaafu mwenyewe anapiga miayo? Je kuna ‘mbuzi’ mahali ameufanyia kazi ushauri wa kumtaka kila mbuzi kula urefu wa kamba yake mradi asizidishe?

Mstaafu wetu anajikuta akilazimika kusema ile nyongeza ya Sh50,000 waliyoahidiwa kwa mbwembwe na siri-kali miezi mitano iliyopita imeoteshwa, sio imeota yenyewe,  mbawa na kuelekezwa kule kwenye kuwa maneno ya kanga tu alikofia yule mwenzake wa ‘matibabu ya bure kwa wazee wa miaka 60 na zaidi.’

Mstaafu wetu anajiuliza sana, iwapo nchi yetu inashindwa kumlipa mstaafu nyongeza ya pensheni ya Sh50,000  tu iliyoahidi yenyewe, itaweza kweli kukubali kibubu kutoa ile huduma inachojifagilia nayo ya kutoa shilingi laki tano kama gharama za kumrejesha mavumbini mstaafu, na baadaye kutoa Sh5 milioni kuwapa warithi wake baada ya yeye kuwa mkazi wa kudumu wa Kinondoni?

Wastaafu tuamke. Kweli, tumeishazeeka na tunazidi kuzeeshwa na mambo ya dunia hii. Inawezekana mambo ya kuandamana hatuwezi tena, lakini mabadiliko yanatuhusu. Tuamke, nchi ni yetu sote na keki ya Taifa wote tuimung’unye!

                                                     

  0754 340606 / 0784 340606

Related Posts