BEKI wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Nurdin Bakari amesema amekuwa akiifuatilia kwa ukaribu Ligi Kuu ya msimu huu na kubaini kuna uwezekano mkubwa yale yaliyojitokeza msimu wa 2016-2017 yakajirudia kwa bingwa kuchukua ubingwa kwa tofauti ya uwiano wa mabao.
Nurdin aliliambia Mwanaspoti kwamba hadi sasa ni ngumu kutabiri timu ipi itabeba ubingwa wa msimu huu, kutokana na timu zinazofukuzia ubingwa kwa ukaribu, Simba na Yanga kutotofautiana sana pointi, kitu anachohisi kinaweza kutokea cha 2016-2017 timu zilipomaliza kila moja na pointi 68.
Alisema anakumbuka Yanga ilibeba ubingwa kwa sababu ya uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa kulingana na watani wao Simba na kuleta mvutano mkubwa mapema kabla ya Shirikisho la Soka na Bidi la Ligi kutoa ufafanuzi kulingana na kanuni.
Katika msimu huo Yanga katika mechi 30, ilishinda 21, sare tano na kupoteza nne kama ilivyokuwa kwa Simba, ila ilifunga mabao 57 na kufungwa 14, wakati Simba ilifunga 50 na kufungwa 17 na tofauti na mabao Yanga ikawa na 43 dhidi ya 33 ya Simba na kutangazwa bingwa.
Nurdin aliyeitumikia Simba kati ya 2004-2007 kabla ya kutua Yanga na kuichezea kuanzia 2007-2013, alisema klabu hizo kongwe zimepishana pointi chache na katika mechi zilizosalia kwa kila mmoja, lolote linaweza likatokea, jambo linalofanya wachezaji na mabenchi ya ufundi wawe na kazi ya ziada.
Kwa sasa Yanga inaongoza msimamo ikiwa na pointi 58 kupitia mechi mechi 22, imeshinda 19, sare moja na kupoteza mara mbili, huku ikifunga mabao 58 na kufungwa tisa, wakati Simba katika mechi 21 ilizocheza ina pointi 54, imeshinda mechi 17, sare tatu na kupoteza moja ikifunga mabao 46 na kufungwa manane tu.
“Ukiutazama msimamo wa ligi unauona ugumu.”
“Ni ngumu kwa timu mojawapo kujihakikishia ubingwa mapema, ukizingatia timu zinazocheza nazo zinaonyesha ushindani, zipo zile zinazojikwamua kushuka daraja, hivyo si kazi rahisi kupata matokeo,” alisema mkongwe huyo na kuongeza;
“Hata zingecheza dabi isingetosha kwa timu ambayo ingeshinda kuona ina uhakika wa ubingwa, hivyo makocha na mabenchi yao ya ufundi wana kazi ya kupiga hesabu sawa sawa za kushinda mechi zao, la sivyo, tunaweza kushuhudia ya msimu wa 2016-17 bingwa kupatikana kwa tofauti na mabao.”
Yanga imebakiwa na mechi nane, huku Simba mechi tisa, ikiwamo baina yao na saba dhidi ya timu nyingine ambapo kila moja ikishinda zote, Yanga inaweza kumaliza msimu na pointi 79 wakati Simba itafikisha 78 (bila ya kujumuisha mechi yao ya dabi iliyoahirishwa kiutata).
Lakini kama timu hizo zitadondosha pointi katika mechi zilizosalia huenda zikaja kulingana pointi na hapo ndipo kanuni zinarejea uwiano wa mabao au zilipokutana zenyewe kwa zenyewe ili kumtangaza bingwa wa msimu huu, kitu ambacho hutokea nadra katika soka la Tanzania.