Dar es Salaam. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman amesema kitendo cha kuzuiliwa kwa saa nane na mamlaka za Angola ni cha aibu kidiplomasia.
Hata hivyo, ameeleza msimamo wakekuwa, licha ya kukerwa na tukio hilo hana kinyongo na wananchi wa Angola.
Katika taarifa yake leo Machi 14, 2025, Othman amesema yeye pamoja na viongiozi wengine walizuiliwa bila sababu yoyote na mamlaka za Angola alikokwenda kushiriki Jukwaa la Demokrasia Afrika.
“Hatimaye majira ya saa nne usiku tuliachiliwa huru na kupelekwa katika hoteli ambazo tulipangiwa, huku tukiwa na uchofu,” amesema Othman ambaye alikuwa amembatana na viongozi kadhaa.
Wakati anazuiwa jana Jumatano Machi 13, 2025, Othman amesema alikuwa ameambatana na Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Luteni Jenerali Matthew Edward Mkingule, ambaye pia anaiwakilisha Tanzania nchini Angola.
Wengine waliokuwa kwenye msafara wake ni Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu, Waziri kivuli wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk Nasra Nassor Omar na maofisa wengine wa chama hicho.
Vilevile, Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu ambaye pia alikuwa anaenda kuhudhuria mkutano huo wa Jukwaa la Demokrasia Afrika (PAD), naye alizuiwa kuingia nchini humo.
“Hiki ni kitendo cha aibu kidiplomasia kilichotekelezwa na mamlaka za Angola, na kimetia doa dhana ya Umoja wa Afrika (AU), hasa wakati huu ambapo Rais wa Angola ndiye Mwenyekiti wa AU,” amesema Othman katika ukurasa wake wa Mtandao wa X.
Othman amesema viongozi wengine wa kimataifa waliokwama pamoja naye, ni marais Wastaafu wa Botswana na Colombia, Waziri Mkuu Mstaafu wa Lesotho, pamoja na wakuu wa vyama vya siasa kutoka mataifa mbalimbali, waliozuiliwa kwa saa nane katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Quatro de Fevereiro, Luanda, Angola.
Ameeleza kuwa licha ya kusikitishwa na tukio hilo, hana kinyongo na wananchi wa Angola, akibainisha kuwa Tanzania na Angola zimekuwa na uhusiano wa kihistoria kwa muda mrefu.
Kutokana na tukio hilo, amesema ametafakari na kuamua asishiriki mkutano wa Jukwaa la Demokrasia Afrika ambao alikuwa amealikwa, na badala yake anarejea Tanzania kwa ajili ya kufanya tafakuri kuhusu tukio hilo.
“Naamini nahitaji muda wa kufanya tathmini ya kina kuhusu shambulio hili dhidi ya diplomasia na demokrasia barani Afrika,” amesema.