Balozi Kombo: Diaspora leteni fursa nyumbani, Serikali itawaunga mkono

Dar es Salaam. Serikali imewahimiza Watanzania waishio ughaibuni kwenye mataifa mbalimbali kuchangamkia fursa zilizoko kwenye maeneo yao na kwamba, Serikali itawaunga mkono pale inapohitajika.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo Ijumaa Machi 14, 2025 wakati akifungua mafunzo ya ujasiriamali na uendeshaji wa biashara ya kimataifa kwa Watanzania waishio nchini Comoro.

Balozi Kombo amewaeleza Watanzania hao kuwa Serikali ipo karibu zaidi na Diaspora na kwamba, Sera ya Mambo ya Nje inawatambua rasmi na hivi karibuni utaratibu wa hadhi maalumu utakamilika kwa manufaa yao zaidi.

Awali, Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Said Yakubu amemweleza Balozi Kombo kuwa biashara kati ya mataifa hayo mawili imefikia Sh148 bilioni kwa mwaka, ikiwa ni wastani wa Sh405 milioni kwa siku huku kasi ya kuongeza ikiwa juu zaidi.

Hata hivyo mchango halisi wa ushirikiano wa Tanzania na Comoro kwa sasa ni Sh500 bilioni kwa mwaka kwa sekta zote za huduma.

Mafunzo hayo ya siku tatu yanaendeshwa na wataalamu wa masuala ya fedha na biashara kutoka Chuo cha Uhasibu Arusha chini ya usimamizi wa Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Eliamani Sedoyeka. Hafla hiyo ya ufunguzi imehudhuriwa pia na Mkuu wa Kitengo cha Diaspora kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, Salvatory Mbilinyi.

Endelea kufuatilia Mwananchi.

Related Posts