BARABARA YA KIBIRIZI-KALALANGABO YANUFAISHA WANANCHI WILAYANI KIGOMA

Kigoma

Wananchi katika halmashauri ya wilaya ya Kigoma mkoani Kigoma wameeleza kunufaishwa na ujenzi wa barabara ya Kibirizi-Kalalangabo yenye urefu wa Km. 2.5 inayojengwa na Wakala ya Barabara za Vijiiini na Mijini (TARURA) ambayo imerahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji.

Bi. Pemacho Omari mkazi wa Kalalangago amesema kuwa, hapo awali shughuli za uvuvi na biashara kwa ujumla zilikwama hasa kipindi cha masika kutokana na ubovu wa barabara lakini sasa anaishukuru serikali kupitia TARURA kwa matengenezo ya barabara hiyo ambapo sasa wanafanya biashara bila wasiwasi.

“Awali tulikuwa tukitoka hapa mwaloni Kalalangago kwenda Katonga kwasababu ya urahisi wa kwenda sokoni, lakini sasa tunaishukuru serikali baada ya hii barabara pikipiki, gari zinafika na tunapata wateja kutoka sehemu mbalimbali tunafanya biashara hapa hapa bila wasiwasi kwasababu barabara ni nzuri”, amesema.

Naye, mkazi wa kijiji cha Tigali, Bw. Shaban Adam ameishukuru serikali kwa barabara hiyo kwani sasa wanapata wateja wa kila siku na biashara zinaenda vizuri kwasababu ya miundombinu ya barabara waliyotengenezewa.

Kwa upande wake, Mhandisi wa TARURA wilaya ya Kigoma, Jumanne Kamwangile amesema kuwa barabara hiyo imejengwa kupitia mradi wa RISE sehemu ya uondoaji vikwazo katika barabara ambapo mradi umehusisha ujenzi wa barabara Km. 2.5 kwa kiwango cha changarawe na ujenzi wa mifereji Km. 1 ambapo mradi umekamilika kwa 100% na upo katika kipindi cha matazamio.

“Tunaishukuru serikali kwa kutuletea fedha za ujenzi wa barabara hii ambayo hapo awali ilikuwa haipitiki hata kwa pikipiki, lakini sasa hivi vyombo vya moto vinapita ikiwemo pikipiki mpaka magari yanafika hapa Mwaloni kwaajili ya ubebaji mazao yanayotoka ziwani kama vile samaki na dagaa na kupeleka sokoni”, amesema.

 

Related Posts