Tanzania imejiweka kimkakati soko la nishati Afrika

Dar es Salaam. Tanzania imekuwa mdau muhimu katika mijadala ya nishati duniani, ikitumia mipango yake ya kimkakati na rasilimali zake nyingi kuendeleza sekta hiyo kwa kiwango kikubwa.

Hatua hii inaifanya nchi hii kujipambanua kama kinara katika mchakato wa mpito wa nishati barani Afrika, baada ya kuwa mwenyeji wa mikutano mikubwa minne ya nishati ndani ya miezi mitatu.

Tanzania ilikuwa mwenyeji wa Mkutano wa Energy Connect Conference & Exhibition na Mkutano wa tisa wa Africa Energy Market Place (AEMP) Oktoba 2024. Mnamo Januari 2025, pia ilikuwa mwenyeji wa Mkutano wa Afrika (Mission 300).

Kuanzia Machi 4-7, Dar es Salaam iliandaa Mkutano wa 11 wa Mafuta na Gesi wa Afrika Mashariki (EAPCE’25).

Mikutano yote hii iliwavutia wakuu wa nchi, watunga sera, viongozi wa sekta na wataalamu wa nishati kutoka kote duniani, ambao kwa pamoja walitangaza mikakati ya kuongoza ajenda ya nishati kwa ukanda huu.

Hii ina maana gani kwa ajenda ya mpito wa nishati wa Tanzania, ukuaji wa uchumi wa nchi na malengo ya nishati barani Afrika.

Wakati wa mkutano wa Mission 300, ambao ulijikita katika kushughulikia changamoto za nishati barani Afrika, Tanzania iliahidi kuongeza uwezo wake wa kuzalisha nishati kufikia megawati 4,000 ifikapo mwisho wa mwaka, ambapo asilimia 61 ya nishati hiyo inatarajiwa kutoka vyanzo vya nishati jadidifu.

Katika Mkutano wa Kimataifa wa Nishati Endelevu uliofanyika Barbados, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati wa Tanzania, Dk Doto Biteko, alieleza hatua madhubuti ambazo nchi imepiga kuelekea mustakabali endelevu wa nishati huku pia akihimiza umuhimu wa suluhisho endelevu.

Wataalamu wameangazia umuhimu wa Tanzania kuwa mwenyeji wa mikutano mikubwa ya kimataifa, wakiamini kuwa hii ni nafasi nyingine ambayo nchi, inayojulikana kwa uwezo wake wa kuwaunganisha Waafrika, inatumia kujijengea jina jipya.

“Hii inaonyesha jinsi Tanzania inavyoaminika sasa na jinsi watu wanavyotambua juhudi za Serikali katika kuongoza mapinduzi ya nishati barani,” alisema mtaalamu wa nishati, Emmanuel Nyanda.

Aliongeza kuwa, “nafasi hii inatoa fursa kubwa kwa Tanzania kufanikisha malengo yake ya nishati kutokana na imani ambayo imejijengea duniani kote.”

Utambuzi wa kipekee wa Rais Samia Suluhu Hassan kama kinara wa juhudi za nishati safi ya kupikia, unaifanya Tanzania kuwa kitovu cha nishati barani Afrika.

Katika Mkutano wa COP28, Rais Samia alizindua mpango wa kusaidia wanawake barani Afrika kupata nishati safi ya kupikia (AWCCSP), akilifanya suala hilo ajenda ya bara zima.

Alisisitiza kuwa takriban asilimia 80 ya kaya za kusini mwa Jangwa la Sahara zinategemea nishati ya kuni kwa kupikia, hali inayopelekea ukataji miti na athari za kiafya.

Alitoa wito wa kusaka Dola za Marekani 12 bilioni (Sh32 trilioni) kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Afrika, akionyesha dhamira ya Tanzania kuhakikisha upatikanaji wa fedha kwa suluhisho za nishati safi katika ukanda huu.

Mtaalamu kutoka Uganda, Dk Sospeter Munyoro, aliyeshiriki mikutano yote ya nishati iliyofanyika Dar es Salaam, alisema Tanzania ni mfano wa kuigwa hasa katika juhudi za nishati safi ya kupikia barani Afrika.

“Tanzania iko katika nafasi nzuri kusaidia Afrika kufanikisha Mission 300 na malengo ya nishati safi. Si kwa sababu tayari imefanikiwa kitaifa, bali kutokana na ushawishi na uaminifu iliojijengea kimataifa, hasa katika masuala ya nishati.

Iwapo mataifa mengine ya Afrika yataungana na Tanzania katika kuunga mkono ajenda hii, tunaweza kufanikisha malengo kabla ya mwaka 2030 uliowekwa kama tarehe ya mwisho kwa mpito wa kupikia nishati safi.”

Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zitakazonufaika na ahadi ya Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ya kutoa dola bilioni 2 kwa miaka 10 kwa ajili ya suluhisho za kupikia safi barani Afrika.

Ahadi hiyo, iliyotolewa wakati wa Mission 300, ni mchango muhimu kwa mahitaji ya dola bilioni 4 kwa mwaka zinazohitajika ili kuwezesha familia za Kiafrika kupata upatikanaji wa kupikia safi ifikapo 2030.

Uwekezaji wa sekta binafsi pia unazidi kukua. Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na washirika wa kimataifa wamesaini makubaliano yenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 2 (Sh5.3 trilioni) kwa ajili ya kuendeleza miundombinu ya gesi itakayosaidia matumizi ya ndani na usafirishaji nje ya nchi.

Serikali inaendelea kufanya mazungumzo na makampuni makubwa ya nishati, yakiwemo Equinor na Shell, kukamilisha mradi wa gesi asilia iliyosindikwa (LNG) wenye thamani ya dola 42 bilioni (Sh11.7 trilioni).

Mkakati wa Taifa wa nishati safi ya kupikia Tanzania wa 2024-2034 umeweka malengo madhubuti ya kuunganisha nishati safi katika mchanganyiko wa nishati wa nchi.

Hii ni pamoja na kuongeza upatikanaji wa LPG, ethanoli na suluhisho za kupikia zinazotumia umeme. Serikali pia inafanya kazi ya kuunganisha upangaji wa nishati kati ya kupikia ili kuhakikisha ufanisi na uendelevu.

Mpaka sasa, Tanzania imegundua takriban futi za ujazo trilioni 57.54 za gesi asilia. Kati ya hizo, futi trilioni 1.16 za ujazo zimethibitishwa na zimeanza kutumika tangu 2004 kwa ajili ya uzalishaji wa umeme.

Related Posts