Japan yaipa Tanzania msaada wa Sh27.3 bilioni

Dar es Salaam. Hospitali saba za rufaa nchini zinatarajiwa kunufaika na vifaatiba vipya kwa ajili ya kuimarisha huduma za mama na mtoto zinazotolewa.

Vifaa hivyo ni vile vitakavyonunuliwa kupitia Sh27.3 bilioni zilizotolewa na Serikali ya Japan kama msaada kwa ajili ya kuboresha huduma hizo katika hospitali za Dodoma, Tumbi (Pwani), Mount Meru (Arusha), Sekou-Toure (Mwanza), Songea (Ruvuma), Maweni (Kigoma) na ya Lumumba (Zanzibar).

Hili linafanyika wakati ambao Tanzania imefanikiwa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa asilimia 80 kutoka 556 mwaka 2016/2017 mpaka kufikia vifo 104 mwaka 2022 kwa kila vizazi hai 100,000.

 Akizungumza katika hafla ya kusaini mkataba huo, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dk Natu Mwamba amesema utekelezaji wa mradi huu utaboresha kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa huduma bora za afya hususani huduma ya mama na mtoto.

Hilo litafanyika kwa kupitia utoaji wa vifaatiba vya kisasa vitakavyoongeza uwezo wa kufanya uchunguzi na matibabu katika Hospitali saba za Rufaa.

“ Ufadhili huu unaendana na mpango wetu wa sasa wa maendeleo wa miaka mitano ambao pamoja na masuala mengine, unalenga kutatua changamoto za ubora katika utoaji huduma za afya nchini,” amesema.

Pia amesema ufadhili huo unaunga juhudi za Serikali kwenye sekta ya afya, zinazolenga kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana kwa wakati kwenye jamii.

Amesema kilichofanyika ni mwendelezo wa ushirikiano unaokuwa kati ya nchi hizo mbili kama inavyodhihirishwa na kuongezeka kwa namba ya miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na Serikali ya Japan kupitia misaada na mikopo nafuu.

“Ufadhili huu utasimamiwa Shirika la Maendeleo la Japan (Jica) kwa niaba ya Serikali ya Japan kupitia mkataba wa msaada tuliosaini leo na kwa upande wa Serikali ya Tanzania, mradi utatekelezwa na Wizara ya Afya,” amesema.

Dk Natu amesema ufadhili kama huu na mingine ambayo imekuwa ikitolewa na Serikali ya Japan imechangia kwa kiasi kikubwa kuchochea maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi na kuboresha maisha ya Watanzania.

“Kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, napenda kuchukua fursa hii kwa mara nyingine kuishukuru Serikali ya Japan kwa kuendelea kuisaidia Tanzania katika kuletea watu wetu maendeleo,” amesema Dk Natu na kuongeza

“Napenda kuwahakikishia kwamba Tanzania itachukua hatua zote muhimu kuhakikisha mradi huu unatekelezwa kwa ufanisi, ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Balozi wa Japan nchini, Yoichi Mikami amesema anaamini fedha hizi zitakwenda kuboresha zaidi huduma za mama na mtoto Tanzania.

“Kati ya hospitali zilizochaguliwa, sita zinatoka Tanzania Bara na moja inatoka Zanzibar tunaamini huu utakuwa mwendelezo wa kile ambacho kimefanywa na serikali katika kuboresha huduma za mama na mtoto,” amesema Mikami.

Related Posts