Usichokijua kuhusu kuachia chumba cha gesti saa 4 asubuhi

Dar/Mikoani. Umewahi kujiuliza ni kwa nini nyumba za kulala wageni muda wa kukabidhi chumba ni saa nne asubuhi, usipokabidhi inakuwaje?

Ni maswali magumu kuyajibu lakini mepesi kueleweka hasa kwa wanaosafiri kila mara, baadhi wakikabiliana na adha ya kuondolewa vyumbani muda huo unapowadia. Hata hivyo, si wahudumu wala wamiliki wa nyumba hizo wenye majibu sahihi ni kwa nini uwe huo.

Lipo swali jingine kwenye hilo, je, malipo ya siku kwenye nyumba hizo yanahesabiwa mgeni anapoingia chumbani au anapokabidhi chumba?

Wadau, wamiliki wa nyumba za wageni na wanasheria waliozungumza na Mwananchi wametoa mitazamo tofauti, lakini mawili wameweka msingi wa hoja kuhusu muda huo wa kuachia chumba ikielezwa mosi, ni utaratibu na pili ni kwa ajili ya usafi.

Julius Chacha, ni miongoni mwa waliokabiliwa na sintofahamu ya muda wa kuachia chumba, iliyosababisha zogo kati yake na mhudumu wa nyumba moja ya kulala wageni jijini Dar es Salaam.

Chacha amesema alijikuta kwenye mgogoro na mhudumu baada ya “kugongewa mlango kwa nguvu” saa nne asubuhi akitakiwa kukabidhi chumba kwa maelezo kuwa muda wake umekwisha, hivyo kama angetaka kuendelea kulala alipaswa kulipia fedha kwa ajili ya siku nyingine, ambazo ni Sh35, 000.

“Mhudumu aligonga mlango kwa nguvu, ile hali ilinikwaza kwa kuwa nilikuwa nimechoka, nilihitaji angalau saa sita hadi saba za kupumzika, hivyo sikuamka.

“Niliingia pale saa 11 alfajiri Machi 7, 2025 lakini ilipofika saa 4:00 asubuhi siku hiyohiyo mhudumu alinigongea mlango akitaka nikabidhi chumba akidai muda umekwisha, sikuamka hadi saa sita mchana, ndipo nilitoka ili nikafanye kazi iliyonileta Dar es Salaam na siku hiyo nilipaswa nisafiri kurudi Mwanza,” anasema akieleza alikataa kulipa fedha za nyongeza.

Japo baadhi ya nyumba za wageni masharti hayo na mengine kuhusu huduma yanawekwa mapokezi, lakini wageni wengi hukutana nayo ndani ya vyumba wanavyokabidhiwa.

Agnes Julius, anatoa ushuhuda kuwa alikabiliana na adha hiyo alipokwenda Dodoma kikazi ambako naye aliingia nyumba ya wageni alfajiri.

“Ilikuwa saa tisa usiku nikachukua lodge (nyumba ya wageni) ili nipumzike, asubuhi saa nne nikagongewa mlango nikiambiwa muda umeisha nitoke, nilikasirika lakini sikuwa na namna ya kufanya,” anasema Agnes.

Juma Ramdhani na Edwin Stephen, kwa nyakati tofauti wanasema hawajui ni kwa nini wanalazimishwa kukabidhi vyumba saa nne asubuhi licha ya ukweli kwamba siku moja inajulikana ina saa 24 na wanaamini unapoingia ndipo muda huanza kuhesabiwa.

Hata hivyo, Paschal Matimbwi, yeye anasema muda siyo shida kwake, lakini kinachomuumiza ni kero ya ugongaji wa milango wanapotolewa au kukumbushwa kuwa muda wa kuwa ndani umekwisha.

“Mtu umeamua kwenda kupumzika na mwenzako inafika muda mhudumu anagonga mlango hata kama unamwambia nimekusikia, dakika kidogo anagonga tena, yaani ni usumbufu mkubwa,” amesema Matimbwi mkazi wa mkoani Njombe.

Mmiliki wa nyumba maarufu ya kulala wageni jijini Arusha, Mohammed Said anasema hafahamu utaratibu wa kukabidhi chumba saa nne ulitoka wapi na kuwa hata yeye ameukuta na hivyo ni kama sheria.

Lakini, Boniface Shaurimoyo, mmiliki wa nyumba ya wageni mkoani Shinyanga anasema kwa kadri ya uelewa wake anaona lengo la kuwatoa wageni muda huo ni kutoa mwanya wa kufanya usafi.

“Hapa kitu kikubwa ni suala zima la kufanya usafi ili kuweka mazingira rafiki kwa mteja lakini kwa kweli ni kama vile hakuna sheria kabisa, ila tunaishi na kufanya biashara kwa mazoea,” amesema.

Kuhusu usafi kwa wanaoendelea kuwa wapangaji, anasema hakuna sharti gumu kwani vyumba vyao hufanyiwa usafi muda wowote watakaoamka na wakipenda kutosafishwa vyumba vyao wanaruhusiwa.

Kwa mtazamo wake, ipo tofauti kati ya nyumba ya kulala wageni na nyumba ya mapumziko, ingawa wao humkirimu mteja kama kaingia saa 10 alfajiri humuacha hadi saa sita mchana badala ya kumwondoa saa nne asubuhi.

Frank Raphael, kwa mtazamo wake anasema muda huo ulitengwa maalumu kwa ajili ya kutoa nafasi kwa wahudumu kufanya usafi.

Anasema kila mteja akitoka kwa muda wake kulingana na saa aliyoingia, itakuwa vigumu kufanya usafi.

Katibu wa wamiliki wa nyumba za kulala wageni Manispaa ya Kigoma Ujiji, Robert Kayaga, amesema imekuwa ni utaratibu wanaopewa kutoka mamlaka za serikali kuwa ifikapo saa nne mteja akabidhi chumba.

Kayaga anasema endapo mteja atafikisha muda bila kutoa taarifa kwa mhudumu kama anaendelea, hulazimika kugongewa mlango ili aulizwe kama anaendelea kutumia chumba husika.

Hamida Sulleiman, mhudumu katika nyumba ya wageni Nyegezi, jijini Mwanza anasema kuachia chumba muda huo ni utaratibu uliowekwa ili kutoa fursa ya kufanya usafi.

“Utakuta ndani ya guest (nyumba ya wageni) watu wanaingia na kutoka mara kwa mara, hivyo usipotengwa muda wa kufanya usafi, tafsiri yake uchafu unaweza kuzidi ikaleta madhara kwa wageni,” amesema.

Diana Ndelwa, anasema anasimamia muda huo kutokana na kufuata maelekezo ya mmiliki wa nyumba, ingawa hajui ni kwa nini muda wa kuwapokea wageni haujawekwa maalumu, kwani wanaruhusiwa kuwafungulia hata ingekuwa usiku wa manani.

Doto Kilasi, yeye amesema wanalazimika kuwagongea wateja wao kwa sababu katika nyumba hizo kuanzia saa tano asubuhi inahesabika ni siku mpya.

Wanavyolitazama kibiashara

Mtaalamu wa masuala ya uchumi, Oscar Mkude anasema biashara ya nyumba za kulala wageni inabidi kueleweka, kwamba wao wanapohesabu hutumia utaratibu wa kuhesabu kwa usiku.

Mkude anasema chimbuko la biashara hiyo ilianzishwa ili wageni wanapofika eneo hilo wapate mahali pa kulala na asubuhi kuondoka, hivyo muda wa kuanza safari unapaswa kuanzia saa 12:00 alfajiri hadi saa nne asubuhi.

Mchambuzi huyo wa masuala ya biashara na uchumi anasema, wengi ni waathiriwa wa muda wa saa nne licha ya kuwa baadhi huingia asubuhi na kulipia fedha ya siku nzima lakini hujikuta wamepumzika hata saa moja au mbili.

Wakili wa kujitegemea Jebra Kambole anasema sheria inataka kuwe na makubaliano ya kimkataba kati ya mmiliki na mpangaji wa chumba kabla ya kulipia na kupewa huduma.

Kambole ameshauri mtu anapokwenda kukodi chumba katika nyumba za kulala wageni, apewe taarifa mwanzoni kabla ya kulipia ili ajue nini cha kufanya katika haki zake.

“Inabidi uambiwe kama unataka kukaa hapa, utaratibu wetu ni huu au uko hivi, ikifika saa nne asubuhi unatakiwa ukabidhi chumba, si ulipie halafu masharti hayo uyakute ndani ya chumba, huo siyo utaratibu ni mazoea,” anasema.

Kambole anasema mkataba wa mtu anayekodi chumba hicho anaweza kupewa kwa maandishi au kwa mdomo na akubaliane na utaratibu wa kukabidhi chumba saa nne asubuhi ndipo alipie na si vinginevyo.

“Siyo kila nchi au kila mahali kuna utaratibu wa saa nne asubuhi, hata hapa Tanzania si takwa la kisheria ni makubaliano ya mpangaji na mmiliki, mkubaliane hiyo siku moja inaanza kuhesabiwa vipi?” amesema.

Imeandikwa na Imani Makongoro (Dar), Habel Chidawali (Dodoma), Mgongo Kaitira (Mwanza), Hellen Mdinda (Shinyanga), Seif Jumanne (Njombe), Neema Mtuka (Rukwa) na Godfrey Chubwa (Kigoma)

Related Posts