Unguja. Wakati Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), ikiendelea na uandikishaji katika daftari la kudumu la wapigakura, bado wapo wananchi wanaojiandikisha lakini hawaendi kuchukua vitambulisho.
Kutokana na hilo, ZEC imewataka wafuatilie kwani hiyo ni haki yao na wasipochukua vitambulisho hatawaweza kushiriki kuchagua viongozi wanaowataka wakati wa uchaguzi mkuu Oktoba, mwaka huu.
Mkurugenzi Uchaguzi ZEC, Thabit Idarous Faina, amesema hayo leo Machi 14, 2025 baada ya kutembelea vituo wakati wa kuhitimisha uandikishaji katika Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja.
Faina amesema zaidi ya vitambulisho 3,000 bado havijachukuliwa na wananchi katika wilaya zote 11 za ZEC.
“Kuna changamoto moja, watu wanajiandikisha baadhi hawafuatilii kuchukua vitambulisho vyao, saa kama mtu hajachukua anakuwa ametumia muda wake wa bure na kukosa haki ya msingi, kwa hiyo tunaomba wote wanaojiandikisha wafike ofisi zetu za Tume katika wilaya zote wachukue vitambulisho vyao,” amesema.
Amesema Serikali inatumia gharama kubwa kuandikisha mtu na kuzalisha kitambulisho, hivyo ni busara kujitokeza kwenda kuchukua na baadaye kukitumia kwa matumizi ambayo yamewekwa kwa ajili ya kupiga kura.
Faina amesema wakimaliza kuandikisha hatua inayofuata ni kuweka wazi daftari la wapigakura.
Amesema ZEC inatoa vitambulisho katika ofisi zake zote za wilaya na kutumia maonyesho mbalimbali kwa hiyo kwa ambao wanapata fursa ni vyema wakafuatilia ili kuwarahisishia uchukuaji wake.
Mwenyekiti wa ZEC, Jaji Joseph Kazi, amesema uandikishaji katika Wilaya ya Kusini umefanyika kwa mafanikio makubwa kwani wale wote wenye sifa ya kuandikishwa wameandikishwa.
Amesema katika wilaya hiyo makadirio ya Tume yalikuwa kuandikisha wapigakura wapya 2,081 lakini wameandikisha 3,500.
“Jambo hili ni jema kwani litawawezesha watu wengi kupata fursa ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu unaofanyika mwishoni mwa mwaka huu,” amesema Jaji Kazi.
Amesema kumaliza zoezi hilo kwa wilaya hiyo ni mwanzo wa uandikishaji wa Wilaya ya Mjini ambayo ni ya mwisho, hivyo aliwataka wananchi wote wenye sifa ya kujiandikisha kujitokeza kwa wingi ili kupata haki yao ya msingi.
Hata hivyo, amewasisitiza wananchi kutokubali kutoa vitambulisho vyao vya Mzanzibari Mkaazi kwa watu wengine ambao hawawajui na hawahusiki na zoezi hilo.
Mwakilishi wa Viti Maalumu kundi la Wazazi, Mkoa wa Kusini Unguja, Sabiha Filfil Thani, amesema uandikishaji kwa mkoa huo umekwenda vizuri tangu siku ya kwanza na unaridhisha kwani wananchi wamejitokeza kwa wingi kupata haki hiyo.
Baadhi ya mawakala wa vyama vya siasa wameipongeza ZEC kuweka utaratibu mzuri wa uandikishaji, huku ulinzi na usalama ukiimarishwa bila ya kuwapo na vitisho kama ilivyozoeleka kipindi cha nyuma.
Wakala wa Chama cha ACT-Wazalendo katika kituo cha uandikishaji Mkuyuni A, Suleiman Kudura amesema uandikishaji unaendelea vizuri na hali ya ulinzi na usalama imeimarika.
Amesema ilizoeleka awali inapofika kazi hiyo, askari polisi hutembea na silaha lakini safari hii jambo hilo halikujitokeza.
“Kwa kweli jambo hili nimeridhia na nimefurahika, sijaona hata gari moja la Jeshi la Polisi au kikosi chochote cha SMZ kwamba kina silaha, hii inaonyesha nchi yetu ina amani na utulivu katika uandikishaji huu unaoendelea,” amesema.
Wakala wa Chama cha Mapinduzi, kituo cha uandikishaji Muyuni C, Abdalla Burhan Abdalla, amesema hakuna jambo lolote ambalo linakwenda kinyume cha utaratibu na kila mwenye haki anaipata ya kuandikishwa.
Mohammed Rashid Suleiman, wakala wa ACT-Wazalendo kituo cha uandikishaji Muyuni C, ameomba amani na utulivu viendelee hata siku ya kupiga kura itakapowadia kwani kuipoteza amani kuirudisha ni gharama kubwa.
Sheha wa Shehia ya Kizimkazi Mkunguni, Mwachum Hassan, amesema wananchi wanajitokeza kwa wingi kujiandikisha kwa sababu ya hamasa iliyokuwapo.
Baadhi ya wananchi akiwemo, Raya Rashid amesema hawakupata usumbufu, huku akipongeza utaratibu unaotumika.