BURIANI MAMA YANGU MKUBWA TABITHA SIWALE: WAZIRI WA KWANZA MWANAMKE

Wakati wa harakati za kupigania uhuru, siasa ilirindima vilivyo kwenye ukoo wa Mwambenja kama Prof. Mark Mwandosya alivyosimulia katika kitabu chake “38 Reflections on Mwalimu Nyerere” uk. 250 :

“Our house was nothing but political. For, my father and his colleagues, who included Mzee Wilfred Mwambenja, the father of Tabitha Siwale, would engage in endless political debates”.

Wakati wa harakati hizo, Mwalimu Nyerere, Oscar Kambona & Rashidi Kawawa mara kwa mara walilala nyumbani kwa Mzee William Mwambenja. Keneth Kaunda wa Zambia pia alifika na kulala hapo na hadi leo anakumbukwa na Wanamwambenja kwa usemi wake “I only eat vegetables like an elephant” kwavile kila alipochinjiwa Jogoo, aligoma kula kwakuwa alikuwa “Vegetarian” !

Bi Tabitha alipenda siasa tangu utotoni na alikuwa akihudhuria mikutano ya TANU kwa kificho kwani baba yake alimkataza akimhimiza ajikite kwenye masomo

4. Safari ya Elimu ya Bi Tabitha

4.1 Elimu ya Msingi

Bi Tabitha alianza shule mwaka 1947 katika Native Authority Primary School”. Alikuwa mwanafunzi mwenye akili sana. Alifanya mtihani wa darasa la nne mwaka 1951 na akafaulu na kuchaguliwa kujiunga na Shule ya Kati ya Tosamaganga Girls. Huko ndiko alikoonana kwa mara ya kwanza na Bw. Edmond Siwale aliyekuwa mwanafunzi wa Shule ya Kati ya Tosamaganga Boys, ambaye baadaye alikuja kuwa mume wake.

4.2 Elimu ya Sekondari

Bi Tabitha Siwale alifanya mtihani na kuchaguliwa kujiunga na Tabora Girls “Warsaw” mwaka 1955. Enzi hizo, ni wasichana wachache sana na wenye akili ndio waliofanikiwa kupata fursa ya kusoma shule hii. Bi Tabitha alikuwa miongoni mwao na alihitimu shuleni hapo mwaka 1958.

4.3 Masomo ya Juu

Bi Tabitha alipenda kujiendeleza kielimu hivyo alisomea uchumi wa kijamii katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Geita, akapokea mafunzo ya ualimu katika Chuo cha Ualimu cha Mpwapwa na kisha akaanza kazi ya ualimu mwaka 1961.

Mwaka 1965, Mama Siwale alisafiri hadi Nairobi, Kenya ambako alikwenda kusomea kozi ya “Home Economics” na kutunukiwa shahada mwaka 1968.

5. Mama Siwale: Mwalimu Mkuu

Mama Siwale, aliyekuwa mmoja wa Wanawake Wazalendo wa kwanza nchini kuwa Walimu Wakuu, alihudumu kama Mwalimu Mkuu kwenye shule zifuatazo :

5.1 Shule ya Bwiru

Mama Siwale alihudumu kama Mwalimu Mkuu wa shule ya Bwiru Girls na alihakikisha wasichana wanapata elimu bora ya maisha. Wanawake wengi maarufu waliosoma shule hii walipitia mikononi mwake akiwemo Mama Rachel Nyirabu, mke wa Gavana wa pili wa Benki Kuu, Charles Nyirabu.

Akiwa Bwiru, Mama Siwale alikutana tena na Bw. Edmond Siwale, aliyekuwa mwalimu katika shule ya Bwiru Boys. Baadaye walifunga ndoa na kupata watoto wanne – Fred, Mary, Abel na Maka.

5.2 Shule ya Korogwe

Baada ya mafanikio makubwa Bwiru Girls, Mama Siwale alihamishiwa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Korogwe, Tanga ambako pia alileta mafanikio makubwa. Mama Siwale alijulikana kama Mwalimu Mkuu mkali mwenye kusisisitiza sana nidhamu.

Novemba 2, 2019, Bi Salome Peter, mmoja wa wanafuzi wa zamani wa Korogwe Girls alisimulia mambo yalivyokuwa enzi zao miaka ya 1970s chini ya Mwalimu Mkuu, Mama Siwale:

“Mimi ni mmoja wa wasichana waliobahatika kuchaguliwa kujiunga Korogwe girls. Headmistress alikuwa Mama Tabitha Siwale. Shule ilikuwa ya mchepuo wa kilimo. Mama Siwale alitulimisha mashamba makubwa. Kila mwanafunzi wa Kidato cha 1 hadi 6 alipewa eneo bila kujali alikuwa mtoto wa kiongozi au nani. Pale tulisoma na watoto wa Vigogo. Kulikuwa Anna Watiku, mtoto wa JK Nyerere, Asha Rose Migiro na ndugu zake (mmoja ni Balozi Afrika Kusini) nk. Kilimo kilikubali mno- mahindi, matango, matikiti nk. Kila mwanafunzi alipewa jembe lenye namba, ukipoteza unalipa. Kila tulicholima kilikuwa kwa matumizi yetu. Rais Nyerere alipokuja alishangaa eka na eka zimezaa vizuri. Alivutiwa sana. Mama Siwale alikuwa msimamizi hodari aliyefuatilia sana suala la masomo, nidhamu na shule ilikuwa safi mno ndio maana Rais Nyerere akamteua kuwa Waziri mwaka 1975”.

Mama Siwale, kwa upande wake, aliwahi kuhabarisha 

“Niliongoza shule hizo za Bwiru na Korogwe kwa ufanisi mkubwa. Kwa mfano, Korogwe ilikuwa shule iliyotuma idadi kubwa zaidi ya wasichana kujiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Nilikuwa mkali sana na sikuvumilia uzembe. Sasa ninafurahia matunda ya kazi yangu. Miongoni mwa wanafunzi ni Dr. Asha Rose Migiro na Kejo Bisimba”.

6. Walimu Wakuu Wapelekwa Kivukoni

Mwaka 1975, Walimu Wakuu wote wa shule za sekondari nchini walipelekwa katika Chuo cha Siasa cha Kivukoni kwa mafunzo ya siasa ya Ujamaa kwa mwaka mmoja. Mama Siwale alimchukua mtoto wake wa mwisho, Maka, aliyekuwa mtoto mchanga, katika safari hiyo. Akaenda kusoma akiwa na mwanae huyo.

7. Mama Siwale Aitwa Ikulu

Jioni ya Jumatatu, Novemba 3, 1975, Ofisi ya Rais Ikulu ilimpigia simu Mkuu wa Chuo cha Kivukoni. Bahati mbaya hakupatikana. Ikabidi Bi Peruzi Butiku, mke wa Joseph Nyerere, mdogo wa Mwalimu Nyerere, atumwe kwenda chuoni Kivukoni. Mama Siwale, akiwa darasani, alistukia anatakiwa atoke nje alikokutana na Bi Peruzi aliyempa maagizo kuwa Rais Nyerere anamhitaji Ikulu mara moja.

Mama Siwale alipatwa na hofu kubwa kwani kuitwa Ikulu na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, halikuwa jambo dogo :

“Nilikuwa na wasiwasi mkubwa. Sikuamini Rais angeniita. Nikajiuliza maswali mengi lakini nikakosa majibu!”.

Safari fupi ya kutoka Kivukoni hadi Ikulu ilionekana ndefu kama safari ya kutoka Musoma hadi Mtwara !

8. Mama Siwale Ateuliwa Mbunge

Mama Siwale alifika Ikulu akiwa na hofu kubwa akijaribu kuwaza ni kosa gani ambalo huenda alilifanya. Rais Nyerere alipomweleza kuwa amemteua kuwa Mbunge kupitia nafasi 10 za uteuzi wa Rais, alipigwa butwaa. Hakuamini alichokisikia na akaomba Rais Nyerere arudie taarifa hiyo. Rais Nyerere alicheka sana na akarudia ndipo Mama Siwale alipotambua kuwa ameteuliwa.

Usiku huo Saa 2, Taarifa ya Habari, kupitia RTD, ilitangaza uteuzi wa Mama Siwale pamoja na Bi Hadija Swedi, Bi Anna Kabati na wengine sita kuwa Wabunge.

9. Mama Siwale Ateuliwa Waziri

Jumapili, tarehe 9 Novemba 1975, Rais Nyerere alimwita tena Ikulu Mama Siwale na kumweleza kuwa amemteua kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Miji.

Mama Siwale alishangaa kwa kusema, “Lakini mimi si mtaalamu wa ardhi”. Rais Nyerere alicheka na kumjibu:

“Kama nimekuteua, tayari nimefanya utafiti wa kutosha. Nina imani na wewe; utajifunza kazi ukiwa kazini”.

Baraza la Mawaziri lilipotamgazwa, Mama Julie Manning ni mwanamke mwingine aliyekuwa ameteuliwa. Aliteuliwa kuwa Waziri wa Sheria.

Mama Siwale anatambuliwa kuwa ndiye hasa Waziri wa Kwanza Mwanamke kwavile yeye ndiye alitangulia kuapa.

10. Mama Siwale Ajichana Ugali kwa Mama Sophia kusherehekea!

Mama Siwale alipotoka Ikulu, aliwachukua ndugu na marafiki wachache na breki ya kwanza ikawa Masaki nyumbani kwa mdogo wake, Mama Sophia, (Mama wa “Mzee wa Atikali”). Walisali kumshukuru Mungu na walipomaliza, Mama Sophia alimweka kando kitinda mimba wake, Bi Carol “Manecha” aliyekuwa mtoto mchanga akapika ugali wa nguvu kwaajili ya dada yake, Mama Siwale, Mwanamke wa kwanza kuwa Waziri pamoja na wageni wote !

11. Mama Siwale Aleta Mabadiliko Wizarani

Licha ya kutokuwa na ubobevu kwenye masuala ya ardhi, Mama Siwale alileta Mabadiliko mengi kwenye Wizara ya Ardhi ambayo yameainishwa kwenye makabrasha mbalimbali ya wizara hiyo.

12. Mama Siwale Amkwamua Bibi Titi Mohammed

Serikali ilipopitisha Sheria ya kutaifisha majumba, ilitaifisha nyumba mbili za Bibi Titi Mohammed.

Bibi Titi alihukumiwa kifungo cha maisha mwaka 1970 baada ya kupatikana na hatia ya kutaka kuipindua Serikali na kufungwa jela ya Isanga, Dodoma. Hata hivyo, Rais Nyerere alimpa msamaha mwaka 1972. Aliporejea, akakuta nyumba zake zimetaifishwa. Alijitahidi kwa kadri ya uwezo wake huku akienda kwa Mawaziri lakini akagonga ukuta.

Mama Siwale hakuwa na simile kwenye suala la kutetea haki. Hivyo, mwaka 1976, akiwa amekaa kwenye uwaziri kwa mwaka mmoja tu, aliamua “kumvaa” Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, aliyekuwa akiogopwa sana na kumpiga shule kuhusu haki ya Bibi Titi Mohammed kurudishiwa nyumba. Hatimaye, Baba wa Taifa akaingia kwenye mfumo” na walau Bibi Titi akarudishiwa nyumba moja baada ya Dokezo sabiri la Mama Siwale lililosheheni hoja zenye mashiko kukubaliwa na Rais Nyerere. Bibi Titi alimshukuru sana na akasema kuwa maishani hatakuja kumsahau Mama Siwale kwa wema huo mkubwa aliomfanyia.

13. Mama Siwale Ateuliwa Waziri wa Elimu

Mwaka 1980 baada ya Uchaguzi mkuu, Mama Siwale alihamishiwa Wizara ya Elimu ambako alileta mabadiliko kadhaa. Miongoni mwa Mabadiliko aliyoleta kupitia Waraka ni kuelekeza kuwa shule za seminari haziko kwenye mfumo wa kiserikali hivyo wanaofaulu kidato cha 4 hawawezi kujiunga na Kidato cha 5 shule za serikali.

Mwaka 1982, Mama Siwale alirudishwa tena Wizara ya Ardhi hadi mwaka 1984 uwaziri ulipogota, akaendelea kuwa Mbunge hadi mwaka 2000.

14. Tabitha: Mwanamke Msomi, Mchapakazi na Mwadilifu

Mama Siwale alikuwa Mchapakazi hodari na Mwadilifu wa hali ya juu.

Mama Siwale aliwahi kunena:

“Katika maisha yangu, maneno “Sijui” au “Siwezi ” hayamo kwenye kamusi yangu. Kazi yoyote unayopewa ifanye kwa bidii yako yote ili matokeo yake yaonekane na watu waithamini”.

15. Mama Siwale Ampigania Mwanamke Haki ya Ardhi

Mama Siwale, akiwa Mbunge, alitoa mchango mkubwa kwenye masuala ya haki na usawa wa kijinsia pamoja na umiliki wa ardhi kwa mwanamke. Zamani mwanamke kumiliki ardhi ilikuwa kizungumkuti, sio kama hali ilivyo sasa. Miongoni mwa waliotoa mchango mkubwa ni Mama Siwale.

16. Mama Siwale na G-55

Mwaka 1993, Mama Siwale alikuwa mmoja wa Wabunge 55 waliotaka Serikali ya Tanganyika.

17. Mama Siwale Apewa Tuzo ya “Mwanamke wa Karne”

Mwaka 2000, taasisi maarufu ya Marekani ilimtunuku Mama Siwale tuzo ya “Mwanamke wa Karne” kwa mchango wake mkubwa kwa Taifa lake.

18. Mama Siwale Atumikia Bodi Mbalimbali

Uchapakazi na Uadilifu wa Mama Siwale ulipelekea ateuliwe kuwa Mwenyekiti au M/Mwenyekiti wa Bodi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na PPF, NBC, DAFCO, NMC, Baraza la Taasisi ya Ardhi, na Women’s Advancement Trust.

19. Mama Siwale: Kioo cha Mabinti wa Kikyakyusa

Wazazi wengi Wanyakyusa walipenda kutoa mfano wa Mama Siwale kila walipowahimiza mabinti zao kupenda masomo. Hivyo, mabinti wengi wakapenda kusoma ili nao wawe kama Mama Siwale. Wazazi wengine waliamua kuwaita mabinti zao “Tabitha” !.

20. Mama Siwale: “Mke na Jiko ni Uji na Mgonjwa”

Mama Siwale alikuwa mpigania haki za wanawake mahiri sana. Hata hivyo, daima alisisitiza kuwa mke ni lazma alitambue jukumu lake na aelewe jiko ni sehemu muhimu ya maisha yake. Alipokuwa Waziri, alikuwa akiuvua uwaziri getini na kuvaa cheo chake cha Mke na Mama.

21. Mama Siwale na Kuzaliwa kwa “Mzee wa Atikali”

Baba yake “Mzee wa Atikali” aliwahi kuwa “Area Commissioner” Geita. Siku moja, Mama Siwale alifika Geita kumuona mdogo wake, Mama Sophia, aliyekuwa na ujauzito wa “Mzee wa Atikali” na akamfanyisha mazoezi ya kutembea kwenye kokoto na changarawe. Kesho yake, Ijumaa usiku, Desemba 29, akazaliwa Mzee wa Atikali”. Wakati huo, wadogo wa “Mzee wa Atikali” (Prof. Lucy, Gona, Sr. Angela, Sam & Caro) na mwanae, Attu, walikuwa hawajazaliwa.

22. Mama Siwale Ampa Zawadi “Mzee wa Atikali”

“Mzee wa Atikali” alisoma Shule ya Msingi Oysterbay. Matokeo ya darasa la Saba yalipotoka, Mama Siwale ndiye aliyempa taarifa “Mzee wa Atikali”. Matokeo hayo yalionesha kuwa kati ya Wanafunzi 170, wanafunzi 40 (28 Wasichana na 12 Wavulana) walikuwa wamefaulu. Mama Siwale akampa zawadi ya Mpunga. “Mzee wa Atikali” akapanga na Fred, mtoto mkubwa wa Mama Siwale kwenda “Shamba la Bibi” Desemba 20, ambako kulikuwa na mechi kati ya Taifa Stars na Super Eagles ya Nigeria. Hiyo ndio ilikuwa mara yake ya kwanza kwenda uwanja huo. Siku moja kabla, “Mzee wa Atikali” akapelekwa kwenda kulala kwa Mama Siwale mkabala na ilipo Ikulu. Keshoye, Fred na “Mzee wa Atikali” wakaenda Posta, wakagombea UDA hadi kufika uwanjani ambako walikaa mzunguko na watu walikuwa wengi mno. “Mzee wa Atikali” alikuwa mdogo sana hivyo hata kuona mpira ilikuwa ni shughuli pevu!. Mechi ikaisha 1-1. “Mzee wa Atikali” akapoteana na Fred na mabasi ya UDA yalikuwa machache mno, yasingeuweza umati wote ule.

Ikabidi “Mzee wa Atikali” aunge Azimio la Arusha ! Akiwa na watu wengine, alistukia amefika mjini saa 2 usiku. Hata hivyo, akawa hajui atafikaje Ikulu. Akaulizia na kisha akaweza kwenda “Central Police Station” na kuelezea masaibu yaliyomkuta na kuwa anataka kwenda kwa Waziri Mama Siwale lakini hajui jinsi ya kufika Ikulu. Akaingizwa ndani ya Defender” na kufikishwa! Akamkuta kakaake, Fred, amebanisha nje akiogopa kuingia ndani kwani alijua angeulizwa “Mdogo wako yuko wapi”?.

23. Mama Siwale Ainusuru Familia ya “Mzee wa Atikali”!

Wazazi wa “Mzee wa Atikali” na watoto wao waliwahi kuishi Mbezi kwa Musuguri. Usiku mmoja, “Wazee wa Kazi” waliligeuza eneo hilo kuwa “Ukanda wa Gaza”! Walivamia nyumba zisizopungua 10 na kujeruhi wakaaji vibaya sana. Baba wa “Mzee wa Atikali” aliumizwa hadi akalazwa Muhimbili, “Mzee wa Atikali” akiwa boarding shule ya sekondari ya Malangali. Mama Siwale alienda akamchukua mdogo wake, Mama Sophia na watoto wengine, na kukaa nao kwa mwaka mzima kwake mkabala na Ikulu. Baada ya kutoka hospitali, baba yake “Mzee wa Atikali” aliamua kumuuzia nyumba hiyo Mhe Paul Rupia kwani hiyo ilikuwa ni mara ya pili eneo hilo kuvamiwa.

24. Tamati

Mama Tabitha Siwale alikuwa Mwanamke Mchapakazi na Mwaminifu aliyelifanyia mengi Taifa lake. Alipoteuliwa kuwa Waziri hakuwaangusha wanawake na kupelekea wanawake wengine kuja kupewa nafasi kubwa za uongozi na sasa tunaye Mwanamke, Mama Samia Suluhu Hassan, kama Rais wa nchi.

25. Mama Siwale Ameacha Watoto 2

Mzee Edmond Siwale alifariki 2016, Fred alifariki 1993 na Abel alifariki 2008. Mary na Dr. Maka ndio walio hai.

26. Mazishi

Msiba wa Mama Siwale uko Mikocheni mkabala na nyumba ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere. Mazishi yatafanyika Jumamosi, Machi 15, 2025, Kinondoni.

27. Tafakuri Jadidi:

Wizara ya Wanawake mna mpango wa kumuenzi vipi Mama Siwale ?

28. Picha

28.1 Mama Siwale alivyopenda kuvaa akiwa Waziri

28.2 Baraza la Mawaziri likiwa na Wanawake Wawili (Mama Siwale & Mama Julie Manning)

28.3 Bibi Titi Mohammed akimvulia kofia Mama Siwale

28.4 Mama Siwale akiongoza ujumbe wa Tanzania huku Prof. Mark Mwandosya akiwa nyuma yake, kwenye Mkutano wa 21 wa UNESCO, Belgrade, Yugoslavia 1980/81.

28.5 Mama Siwale, akiwa na mdogo wake, Sophia, Mama yake “Mzee wa Atikali”.

PUMZIKA KWA AMANI MAMA TABITHA IJUMBA SIWALE

Related Posts