Rombo waanza kuzalisha unga wa ndizi

Rombo. Wakulima wa ndizi, Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro wamebuni mbinu mpya ya kujipatia kipato baada ya kuanza kuchakata ndizi na kupata unga wa uji na mtori.

Inaelezwa kuwa unga huo huuzwa maeneo mbalimbali nchini na kilo moja huuza kwa hadi Sh10,000.

Wakulima hao  wameanzisha kiwanda kidogo chenye thamani ya Sh100 milioni katika Kijiji Cha Maharo, kata ya Makiidi. Wamesema hivi sasa ndizi zao zina thamani kubwa zaidi kuliko ilivyokuwa awali ambapo zilikuwa zikiivia mashambani na kuharibika kutokana na kukosa wanunuzi, hali hiyo iliyowafanya baadhi yao kulishia mfugo.

Wakizungumza na Mwananchi digital leo Machi14,2025, wakulima hao ambao wameungana na kuanzisha kikundi cha Marsho, wamesema sasa zao la ndizi linawasaidia kupata fedha kwa ajili ya kuendesha shughuli zao za kila siku, ikiwemo kusomesha watoto.

Tedy Kishewa, mmoja wa wakulima na mwanachama wa kikundi cha Marsho, amesema ubunifu huo umeleta mabadiliko makubwa kwa wazalisha na watengenezaji wa bidhaa hizo.

“Sasa hivi tunauza mkungu mmoja wa ndizi kwa Sh15,000 hadi Sh20,000, wakati awali tulikuwa tukiuza kati ya Sh2,000 na Sh5,000, hivyo uwepo wa  kiwanda hiki ni msaada mkubwa kwa wakulima, kwani sasa wanapata faida kubwa na kulinda mazao yao dhidi ya kuharibika,” amesema Mkulima huyo

Dionis Edes, mkulima mwingine, amesema kuwa awali walikuwa wakizalisha ndizi kwa wingi lakini kutokana na kutokuwa na soko la uhakika, mara nyingi walikuwa wakilazimika kuzitumia kama chakula cha mifugo.

Mwenyekiti wa kikundi cha Marsho, Bavon Assenga, amewashukuru wadau mbalimbali kwa kuwashika mkono akiwemo Mbunge wa Rombo, Profesa Adolf Mkenda ambaye amewakabidhi hundi ya Sh5 milioni  kwa ajili ya kuendelea kuboresha huduma mbalimbali katika kiwanda hicho.

“Tulianza mwaka 2022, ambapo tunachakata ndizi  kitarasa na matoke, ambapo tunatoa unga wa mtori na uji, hivi sasa tumeanza kusambaza bidhaa zetu kwenye maeneo mbalimbali na mwitikio ni mkubwa,” amesema Assenga

Naye, Mbunge wa Rombo, Profesa Adolf Mkenda amesema Serikali  ipo bega kwa bega na wakulima hao kuhakikisha wanazalisha kwa wingi na kwa  tija ili kila mkulima anufaike na anachokifanya.

Profesa Mkenda ambaye pia ni Waziri wa Elimu amesema kwa sasa, wilaya hiyo ipo katika hatua za mwisho za kuanzisha  kilimo cha matone katika kata za Ushiri Ikuiini na Mrao Keryo ambapo wakulima wataanza kuzalisha kwa tija na kuongeza thamani ya kile wanachozalisha.

“Kwa mfano unga wa kitarasa tunajua ni mzuri sana, hivyo  kazi yetu kubwa ya kilimo hapa Rombo ni kuhakikisha tunaongeza thamani kilimo chetu na kuwa na matumizi bora ya mbolea (samadi), tutumie chachu ya kuhakikisha tunakwenda mbali zaidi, ndizi nyingi zinazozalishwa hapa Rombo zianze hata kuja hapa kuchakatwa na kuuza nje ya Rombo,” amesema Profesa Mkenda

Related Posts