TIMU ya taifa ya wanawake chini ya miaka 17 ‘Serengeti Girls’ kesho itashuka Uwanja wa Levy Mwanawasa, Zambia kwenye mchezo wa marudiano kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Zambia.
Ni mchezo wa kufa ama kupona kwa timu hiyo ambayo inatafuta tiketi ya kufuzu Kombe la Dunia itakayofanyika mwaka huu Morocco huku Tanzania ikishiriki kwa msimu wa tatu mfululizo.
Mchezo wa kwanza uliopigwa Machi 9 Uwanja wa Azam Complex, Serengeti ilichapwa mabao 3-0 na Copper Princess. Ili Serengeti ivuke raundi ya pili inahitaji kupata ushindi wa kuanzia mabao manne bila ya kuruhusu bao lolote.
Tanzania ilivuka raundi ya pili baada ya Eswatini kujiondoa kwenye raundi ya kwanza na kuipa nafasi Serengeti inayofuata ilipokutana na Zambia.
Tanzania ilipokutana na Zambia mwaka jana kwenye hatua hiyo iliondoshwa kwa jumla ya mabao 5-1.
Serengeti ilianza kupokea kichapo cha mabao 5-0 Uwanja wa Nkoloma, Lusaka Februari 3 kisha kushinda bao 1-0 nyumbani mchezo ambao ulizima matumaini ya kuendelea raundi ya tatu.
Mwaka huu Serengeti haijaanza vyema kampeni hizo ikiwa na mwendelezo mbaya ikichangiwa na vitu mbalimbali ikiwemo uzoefu wa baadhi ya wachezaji.
Katika kikosi kilichoanza mchezo uliopita wachezaji sita pekee wamekuwa na mwendelezo wa kucheza kwenye timu wanazocheza.
Kombe la Dunia 2022 Tanzania ilifika robo fainali na karibu nyota wote waliokuwa wanaanza kikosini walikuwa tegemeo kwenye timu zao. Nyota kama Clara Luvanga wakati huo alikuwa Yanga Princess, Neema Paul alikuwa Fountain Gate, Diana Mnally (Simba Queens) walichangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya Srengeti kutokana na uzoefu.
Msimu huu ni kama mambo yamekuwa magumu kwani baadhi tu ndio wamekuwa na mwendelezo wa kupata nafasi kwenye timu wanazocheza wengine wakichaguliwa kutoka vituoni. Wachezaji kama Lidya Maximilian ndiye beki tegemeo wa JKT Queens, lakini Serengeti Girls alianza kama kiungo wa chini, Winifrida Charles alirejea Fountain baada ya kuwa nje akiuguza majeraha kwa takriban msimu mzima.
Ester Maseke ni kiungo tegemeo wa Bunda Queens huku Yasinta Mitoga, Christer Bazil mara kadhaa wamekuwa wakipata nafasi kwenye kikosi cha JKT.
Licha ya kukaa takribani mwezi mzima kambini ikijiandaa na michezo hiyo, lakini nyota hao wanaonekana hawajapata muunganiko mzuri wa kiuchezaji.
Changamoto kubwa iliyoonekana kwenye mchezo wa kwanza ni kushindwa kuelewana hasa eneo la kiungo mshambuliaji.
Eneo hilo lilikosa ubunifu wa kutengeneza nafasi za kushambulia jambo lililowapa changamoto washambuliaji kupata nafasi.
Copper walionekana kufanya baadhi ya vitu kwa usahihi kuanzia eneo la ulinzi na hata mwisho kwenye kushambulia.
Tanzania inakwenda ikiwa na uhitaji zaidi wa mabao ili iweze kuvuka hatua hiyo.
Lakini inapaswa kuwa na mpango mkakati wa kuimaliza mechi kipindi cha kwanza.
Kupoteza mchezo wa kwanza haimaanishi kuwa Serengeti imeaga mashindano hayo kwani kuna dakika nyingine za kujirekebisha ingawa ina mlima mrefu wa kupanda.
Kwa mara ya kwanza Tanzania ilishiriki michuano hiyo 2020 ikianzia hatua za awali kwa kuichapa Burundi mabao 6-1, ikishinda 5-1 nyumbani na ushindi wa bao 1-0 ugenini.
Matokeo hayo yaliipa nafasi ya kutinga raundi ya kwanza ikakutana na Uganda, Tanzania ikipata ushindi wa mabao 2-1 nyumbani na kupokea kichapo cha mabao 5-0 ugenini na kuondolewa raundi ya pili. Uganda ilitinga raundi ya pili ikakutana na Cameroon raundi ya pili. Hata hivyo mashindano hayo hayakuendelea kutokana na ugonjwa wa Uviko 19.
Msimu huo ulikuwa bora kwa baadhi ya nyota wa Tanzania akiwamo Aisha Masaka anayekipiga Brighton ya England akiibuka mfungaji bora kwa kufunga mabao matano sawa na Juliet Nalukenge wa Uganda na Ophelia Amponsah wa Ghana.
Akizungumzia nini inachopaswa kufanya Serengeti Girls katika mchezo huo, kocha wa Ceasiaa Queens, Ezekiel Chobanka alisema huo utakuwa ni mchezo mgumu akiamini kocha Bakari Shime anaweza kubadili matokeo ugenini kama akipanga mbinu mbadala.
“Mpira sasa umebadilika timu inaweza kushinda ugenini na ina uwezo wa kupoteza nyumbani pia. Tumeruhusu mabao mengi lakini tuna uwezo wa kurekebisha (ugenini),” alisema Chobanka.
Naye kocha wa Alliance Girls, Sultan Juma alisema makocha wa Serengeti wanapaswa kuwapa moyo wachezaji wao wadogo ili wasitoke mchezoni.
“Ni wachezaji wanaochipukia, makocha wa timu wanapaswa kuwapa moyo na motisha kuelekea mchezo wa maruadiano ili usiwatoe mchezoni… naamini wana uwezo mkubwa wa kubadili matokeo ugenini kama wataamua,” alisema.