Watoa mbinu kuongeza watalii kutoka maeneo mapya

Unguja. Wakati wageni 82,750 wameingia Zanzibar Februari ikiwa ni sawa na upungufu wa asilimia 1.6 ikilinganishwa na walioingia visiwani humo Januari mwaka huu, sekta husika zimeshauriwa kuongeza vivutio na kuitangaza Zanzibar katika mataifa ambayo hayajavutika kuitembelea.

Mtakwimu kitengo cha takwimu za utalii kutoka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Fatma Hilali amesema hayo akiwasilisha taarifa ya uingiaji wageni Machi 13, 2025.

Amesema Bara la Ulaya linaongoza kwa wageni walioingia Zanzibar.

“Wageni 63,726 waliingia nchini kutoka Bara la Ulaya sawa na asilimia 77.1 ya wageni wote wa Februari 2025, huku Bara la Afrika likiwa la pili kwa kuingiza wageni 8,680 sawa na asilimia 10.5 ya wageni wote wa Februari 2025,” amesema.

Bara la Amerika lilikuwa la tatu kwa kuwa na jumla ya wageni 5,272 sawa na asilimia 6.4 na Bara la Oceania lilikuwa la mwisho kwa kuwa na jumla ya wageni 534 sawa na asilimia 0.6 ya wageni wote.

Taifa lililoongoza ni Italia kwa kuleta wageni 10,977 sawa na asimilia 13.3 ya wageni wote, likifuatiwa na Ufaransa 9,340 (asilimia 11.3) Poland ni ya tatu kwa kuingiza wageni 8,242 (asilimia 10.0).

Katika mpangilio huo Ujerumani ni ya nne kwa kuingiza wageni 6,544 sawa na asilimia 7.9, ikifuatiwa na Scandinavia kwa kuingiza wageni 5,004 (asilimia 6.0).

Katika idadi hiyo, wageni 75,548 sawa na asilimia 91.3 ya wageni wote waliingia Zanzibar kupitia viwanja vya ndege na wageni 7,202 sawa na asilimia 8.7 waliingia kupitia bandari.

Mchumi mbobezi kutoka Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (Suza), Dk Estela Ngoma Hassan amesema bado kuna changamoto ya wageni kuingia Zanzibar kwa kufuata misimu, hivyo wanatakiwa kuondoa zana hiyo.

Ameshauri wizara na taasisi zinazohusika na utalii kuhakikisha zinaendelea kuitangaza Zanzibar na kuongeza vivutio vyake kupata watalii wengi zaidi.

Mchuni huyo ameshauri kuwe na vivutio vingi zaidi ili kuwafanya watalii wengi watembelee visiwa hivyo badala ya kuishia kwenye vichache.

“Bado wageni wanaingia Zanzibar kufuata msimu, inapaswa kuondokana na hii, wanatakiwa kuja wakati wote na hili litafanikiwa ikiwa kuna vivutio vingi ambavyo vitamfanya mtalii aendelee kuvutiwa na kukaa,” amesema.

Ofisa Takwimu kutoka Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Mabadi Jaffar Ramadhani amesema kamisheni imejipanga kuanzisha utalii wa aina mbalimbali, ukiwemo wa vyakula na michezo ili kuongeza wigo.

“Kutakuwa na maonyesho ya vyakula vya asili vya Kizanzibari, kwa hiyo watu watakuwa wakija na kujionea namna utamaduni ulivyo na utaongeza idadi ya wageni,” amesema.

Amesema hilo litaongeza idadi ya watalii kama ambavyo wameanza kufanya katika kuendesha makongamano na maonyesho ya kitaifa na kimataifa.

Moja ya sababu ambazo zinatajwa watalii wengi kutorejea Zanzibar ni kukosekana vivutio vingi.

Hili limekuwa likielezwa na Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrick Ramadhan Soraga, akisema wana kila sababu ya kujipanga kuongeza vitu vya kumuhamasisha mtalii apate kurejea kutalii.

Licha ya sekta ya utalii kuchangia kwa zaidi ya asilimia 30 ya pato la Taifa, bado Zanzibar ilikuwa imejikita kwenye utalii wa fukwe, historia na utamaduni. Sasa inabadili mwelekeo huo na kuanza utalii wa mikutano, Halal maadili na michezo.

Kwa mara ya kwanza Oktoba, mwaka jana ulianza utalii wa Halal ambao ilifanyika mikutano na maonyesho na kuhudhuriwa na Mufti maarufu duniani, Sheikh Ismail Menk.

Kwa mujibu Rais, Dk Hussein Mwinyi, Zanzibar inapaswa kuwa na utalii wa afya kwa kutengeneza miundombinu ya matibabu kwa hiyo watu wanapokwenda kutibiwa inakuwa sehemu ya kufanya utalii.

Katika mipango hiyo, inajengwa hospitali kubwa ya Binguni, kukiwa na mkakati wa kujenga kitengo cha maradhi ya moyo ambacho wagonjwa wengi wakienda kutibiwa inakuwa sehemu ya kuendeleza utalii.

Related Posts