Songwe. Wakati kitendo cha kuzuiwa kuingia nchini Angola na mamlaka za nchi hiyo kwa Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman na mwenzake wa Chadema, Tundu Lissu kukizua mjadala, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira amejitosa kwenye sakata hilo.
Othman akiwa na ujumbe wake kutoka ACT Wazalendo na Lissu walizuiwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Quatro de Fevereiro jijini Luanda, Angola jana Machi 13, 2025 walipokuwa wakienda kushiriki mkutano wa Jukwaa la Kidemokrasia Afrika (PAD). Mkutano huo uliandaliwa na Taasisi ya The Brenthurst Foundation ikilenga kuwaleta pamoja wana-demokrasia wa Afrika kutafakari kuhusu demokrasia na kubadilishana uzoefu.
Tayari Othman amerejea nchini huku Lissu akiendelea kuwepo nchini Angola kusubiri taratibu za kurejea.
Hata hivyo, Wasira amesema kuwa kuzuiwa kwa viongozi hao na mamlaka za nchi za Angola, hawapaswi kutafuta mchawi wala kuinyooshea kidole Serikali ya Tanzania.
Akizungumza leo Ijumaa Machi 14, 2025 kwenye mkutano wa ndani uliofanyika Vwawa wilayani Mbozi mkoani Songwe, wakati akianza ziara yake ya siku tatu mkoani humo, Wasira amesema kila nchi ina utaratibu wake ambao ni lazima uheshimiwe.
“Leo nimesoma kuna viongozi walikuwa wanaenda Angola, lakini wamenyang’anywa hati za kusafiria, huko ni Angola sio Tanzania, hapa hakuna aliyenyang’anywa hati yake na hata ikiisha muda wake tunawapa nyingine ili waende wanakotaka na kurudi salama.
“Wanalalamika kwa nini Serikali imekaa kimya sasa kwani, sisi tunasimamia Uwanja wa Ndege wa Angola? Ule uwanja unasimamiwa na watu wa Angola, na huenda walikuwa na jambo ambalo wanalitilia shaka,” amesema Wasira na kuongeza: “Sasa kuwaambia tu msiingie nchini kwetu kuna tatizo gani, si mrudi tu nyumbani?