RC Chongolo atangaza ‘vita’ kwa wanaovusha wageni kinyemela

KATIKA kulinda usalama wa nchi kupitia mpaka wa Songwe, Mkuu wa mkoa huo, Daniel Chongolo ametangaza ‘vita’ kwa wananchi watakaojihusisha na shughuli za uvushaji na usafirishaji haramu wa binadamu. Anaripoti Ibrahim Yassin, Songwe… (endelea).

Chongolo aliyasema hayo jana Ijumaa wakati akizungumza na wananchi kupitia mikutano alipokuwa akihitimisha ziara yake ya kikazi wilayani Momba.

Amesema zipo nchi nyingi za Afrika zenye hali mbaya ya usalama, hivyo wana-Songwe wanakila sababu ya kulinda usalama uliopo nchini kwa kutowakaribisha wageni kuingia nchini kinyemela kwa ni hatari.

“Raia hao wa kigeni mnapowakaribisha nchini hamjui wamebeba nini, wanaweza kuleta hatari kubwa na madhara kwa nchi, hivyo kila mmoja awe mlinzi wa mwenzie… umuonapo mtu usiyemfahamu toeni taarifa kwenye uongozi uliopo karibu nanyi ikiwemo polisi kata,” amesema Chongolo.

Wananchi Songwe wakimsikiliza Chongolo

Amesema wilaya ya Momba imepakana na nchi za Congo na Zambia hivyo inawezekana raia wa nchi hizo wakaingia Tanzania kinyemela kwenda nchi nyingine.

Hivyo lazima taarifa zitolewe kwa mtu ama watu watakaowaona raia wa kigeni maeneo yao ili wahusika wa biashara hiyo wakama twe na kuchukuliwa hatua.

“Hapa nipo na jeshi la polisi, magereza, uhamiaji, usalama wa Taifa, mshauri wa mgambo na wakuu wa taasisi mbalimbali… nalisema hili na wao wanasikia, atakayekamatwa atashtakiwa na kufikishwa mahakamani, hivyo acheni kujihusisha na kazi hiyo,” amesema.

Naye Kamanda wa Polisi mkoani Songwe, Agustino Senga amesema wamejipanga kuhakikisha wanasimamia na kulinda amani ya nchi iliyopo.

Hivi karibuni baadhi ya wafanyabiashara na viongozi machachari wa kisiasa katika halmashauri ya mji Tunduma wakiwemo wa familia moja walikamatwa na kuwekwa rumande wakituhumiwa kusafirisha raia wa kigeni kutoka Somalia.

Related Posts