Unguja. Ili kuleta mapinduzi katika somo la hisabati nchini, limependekezwa kuwa kigezo mojawapo cha ufaulu kwa daraja la kwanza na pili katika matokeo ya kitaifa ya kidato cha nne, jambo litakalosaidia wanafunzi kufanya juhudi na kujituma zaidi.
Hayo yamebainishwa katika kilele cha maadhimisho siku ya hisabati duniani (IDM) yaliyofanyika kitaifa leo Machi 14, 2025 kisiwani Zanzibar.
Mwenyekiti wa Mat/ Chahita Taifa, Dk Said Sima amesema pia zitolewe fursa za mafunzo za mara kwa mara kwa walimu wa hisabati na kila wilaya itenge fungu katika bajeti, au kuwapo na mfuko maalumu kwa ajili ya kuwezesha mafunzo hayo.
“Kigezo cha ufaulu wa hisabati pia kitumike kwa wanafunzi wanaoingia kidato cha kwanza,” amesema na kuongeza
“Ili kupunguza tatizo la ushiriki hafifu katika mafunzo ya kitaifa tunaiomba Serikali kupitia kila halmashauri au wilaya kila mwaka wagharamie washiriki 10, kati ya hao washiriki saba wa sekondari na washiriki watatu wa shule za msingi na wengine walipiwe na shule zao,” amesema.
Mtihani mwaka jana 2024 ufaulu wa hisabati kwa kidato cha nne ulikuwa wastani wa asilimia 25 wakati mahitaji ya chini kwa dunia ni asilimia 31 sababu kubwa ikiwa ni upungufu wa walimu, ubunifu mdogo kwa walimu na kukatishwa tamaa kwa kauli kuwa hesabu ni ngumu.
Maadhimisho hayo yanalenga kuboresha miundombinu ya kujifunza na kufundishia kuongeza hamasa kwa walimu wa hisabati hata katika changamoto za uhaba wa walimu wa kujitolea, kufundisha, kuwatambua na kuwapa zawadi waliofanya vizuri katika mitihani ya mashindano ya kitaifa.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Muhamed Mussa katika risala yake iliyosomwa na Mkuu wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume (Kist), Dk Mahmoud Abduwahab aliyemwakilisha, amesema kujua hesabu ni moja ya somo linalosaidia katika kunoa mbinu za kupambana na changamoto nyingi za maisha kila siku katika jamii ikiwemo tatizo la ajira.
“Kujifunza na kuelewa hisabati sio tu itasaidia kuzalisha wahandisi na wanasayansi, lakini pia itazalisha raia wengi wenye uwezo wa kujifunza, kufikiri na kutatua matatizo ya kijamii bila kujali taaluma watakazokuwa wamesomea,” amesema Lela
Ameongeza “ndio kusema Taifa ambalo watu wake hawajui hisabati ni Taifa la watu wasiofikiri na ambao hawawezi kutatua matatizo yao ya kijamii kirahisi,”
Naye Mhadhiri mwandamizi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Sylvester Rugeihyamu amesema bado kuna ushiriki mdogo kwa upande wa Zanzibar ikilinganishwa na Tanzania bara, hivyo wanatamani washirikiane katika kukuza somo hilo kisiwani humo.
Baadhi ya wanafunzi waliopata zawadi katika mashindano ya kitaifa yaliyofanyika Agosti mwaka jana, wamesema hatua hiyo inaongeza hamasa na kuwafanya walete ushindani na kupenda somo hilo
“Nashukuru sana kwa hatua hii, nimepata zawadi ya ushindi, wasichana tumekuwa tukionekana kuwa nyuma lakini tukiamua tunaweza kwa hiyo niwahamasishe wenzangu walipende somo hili na sio gumu kama ambavyo watu wanasema kikubwa ni kujiwekea mikakati,” amesema Rahma Abubakr mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Benjamini Mkapa