Dar es Salaam. Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu amesema alishtuka baada ya kuona wanatengwa kwa makundi baada ya kuzuiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Quatro de Fevereiro jijini Luanda, Angola.
Semu, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Othman Masoud ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais, Zanzibar na Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu walizuiwa na mamlaka za Angola kuingia nchini humo jana Machi 13, 2025.
Si hao pekee, bali hata viongozi wengine mashuhuri wakiwemo marais wastaafu kutoka Botswana na Colombia, Waziri Mkuu mstaafu wa Lesotho na baadhi ya wakuu wa vyama vya siasa kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika walikumbwa na kadhia hiyo.
Viongozi hao, pamoja na wanaotoka mataifa mbalimbali yakiwemo ya Uganda, Botswana na Kenya walikwenda Angola kushiriki mazungumzo ya Jukwaa la Demokrasia Afrika (PAD). Mazungumzo hayo yaliandaliwa na Taasisi ya The Brenthurst Foundation.
Lengo la jukwaa hilo ni kuwaleta pamoja wanademokrasia wa Afrika ili kutafakari kuhusu demokrasia na kubadilishana uzoefu na mikakati ya kuimarisha demokrasia.
Semu aliyerejea nchini usiku wa kuamkia leo Ijumaa, Machi 14, 2025 amesema kundi lao liliwasili uwanjani hapo kwa ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia lakini walilazimishwa kurejea nyumbani kwa ndege hiyohiyo.
“Kwanza tulikuwa tumechoka sana, kwa sababu tulisafiri takribani saa nane kutoka Dar es Salaam hadi Addis Ababa, kisha Luanda.
“Kwa uzoefu wa nchi za Afrika, ulipoanza mchakato wa kukusanya hati zetu za kusafiria na kuanza kuitwa wachache pembeni, kisha kuamriwa ‘kaa hapa’, baada ya muda unaona wenzako kwenye msafara wa kueleka Benguela wanaongezwa katika kundi, nilijua kuna tatizo,” amesema.
Semu akizungumza na Mwananchi leo Machi 14, amesema jambo jingine lililowafanya kujua kama kuna tatizo ni viongozi wakiwemo wanasiasa mashuhuri kutopitishwa eneo la VIP (wageni mashuhuri) wala kupokewa na watu wa Serikali na uhamiaji.
“Nilivyoona kundi letu limetangulizwa, hisia zikanijia kuna kitu hakipo sawa, tukajiuliza kwa nini tupo hivi? Mwanzoni tuliitwa kundi la watu watano, akiwemo waziri mkuu mstaafu wa Lessotho.
“Sasa tulipoanza kupitishwa kwenye korido za uwanja wa ndege na kila tukijaribu kuwauliza watuambie kitu gani tumekosea, hatukupewa ushirikiano. Niliamua kuwa mtulivu kwa sababu nipo Afrika na kazi ninayoifanya ni ya siasa na demokrasia,” amesema.
Amesema aliamua kuwa mpole baada ya sintofahamu hiyo, akitambua yupo nchi ya watu na kazi anayoifanya ni kuzungumzia masuala ya wananchi.
“Nilijua kuna shida, sikuwa na wasiwasi kwa sababu tumezoea mambo ya maagizo kutoka juu, kwa sababu kila mtu alikuwa anasema ameagizwa, tulisubiri kuona maagizo yataendelea hadi wapi.
“Ni kama vile walikuwa wanatusubiri na walishapanga, lazima tuondoke,” amesema Semu.
Amesema msafara wa ACT-Wazalendo, ulikuwa na yeye, Othman, Katibu wa Haki za Binadamu na Makundi Maalumu, Pavu Abdallah na Naibu Katibu wa Mambo ya Nje, Dk Nasra Nassor Omar.
“Mimi pamoja na Dk Nasra na Pavu tuliopanda ndege ya Ethiopia, tumesharejea Tanzania. Wakati tunakuwa deported (tunarejeshwa) tuliwaacha wenzetu (Othman na msafara wake) mambo yao yakiendelea, kwa sababu tulilazimishwa kurudi na ndege iliyotupeleka ndani ya saa mbili tulikuwa tayari tumeishaingia kwenye ndege.
“Hatukujua kilichoendelea huko nyuma maana tulikwenda kwanza Addis Ababa kisha Dar es Salaam,” amesema Semu.
Dk Nasra ambaye ni Waziri Kivuli wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa ACT-Wazalendo, amesema kabla ya kufika eneo la uhamiaji baada ya kushuka kwenye ndege, walipanga foleni kusubiri taratibu za ukaguzi, lakini katikati ya eneo la dawati la uhamiaji, palikuwa na ofisa wa Angola.
“Ofisa huyo ndiye aliyekuwa akichukua hati zetu za kusafiria, baada ya kuchukuliwa hati zetu tuliwakuta wenzetu (Othman), pamoja na marais wastaafu kutoka mataifa mbalimbali waliowekwa pembeni.
“Tulijua wamewekwa pembeni ili kusubiria taratibu za kuchukuliwa, kwa sababu ukiona marais au viongozi wengine wamesimamishwa pembeni. Tulifanya mazungumzo nao ya kawaida kwa muda saa mbili, kabla ya kuanza kutenganishwa,” amesema.
Dk Nasra amesema baadaye waliwekwa kwenye ukumbi bila kuelezwa chochote, kisha wakarejeshwa.