Ujenzi daraja la Pangani wafikia asilimia 38

Tanga. Ujenzi wa daraja la Pangani linalounganisha barabara ya Tanga-Pangani-Bagamoyo umekamilika kwa asilimia 38 imeelezwa.

Mhandisi wa mradi huo, Gladson Yohana amebainisha hayo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu iliyotembelea na kukagua maendeleo ya  mradi huo leo Machi 14, 2025.

Amesema ujenzi wa daraja hilo lenye urefu wa mita 525 linalogharimu  Sh88.2 bilioni hadi kukamilika umefikia asilimia 38.

Wakati akibainisha hayo, Kamati ya Bunge ya miundombinu imetaka kasi ya ujenzi huo iendane na ujenzi wa barabara ya Tanga-Pangani- Bagamoyo ya kilomita 256.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Seleman Moshi Kakoso amesema kazi iliyofanywa kwenye daraja hilo ni kubwa hivyo Wizara ya Ujenzi na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), wahakikishe linakamilika kwa wakati ili kukuza fursa za uwekezaji katika ushoroba wa fukwe za mikoa ya Tanga na Pwani.

“Hakikisheni kasi ya ujenzi wa daraja iendane na ujenzi wa barabara ili vikamilike na kutoa huduma mara moja,” amesema Kakoso.

Kamati hiyo inayoendelea na ukaguzi wa miradi ya kimkakati, katika mkoa wa Tanga  pia imekagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Tanga-Pangani- Bagamoyo ya kilomita 256 ambayo ujenzi wake unaendelea.

Kilomita 15.8 za ujenzi wa barabara ya Tanga-Pangani umekamilika.

Naibu Waziri wa  Ujenzi, mhandisi Godfrey Kasekenya amesema  barabara ya Tanga-Pangani  itakamilika Juni mwaka huu.

“Tumejipanga kuhakikisha sehemu hii ya kwanza ya Tanga-Pangani inakamilika ifikapo Juni wakati daraja likitarajiwa kukamilika Disemba mwaka huu”, amesema Kasekenya.

Awali mhandisi wa mradi huo, Gladson Yohana alisema mkandarasi anafanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha ujenzi ifikapo Juni 16, 2025 kama mkataba unavyoelekeza.

Mtendaji Mkuu wa Tanroads, mhandisi Mohamed Besta amesema ujenzi huo umegawanywa katika sehemu nne ili kuharakisha ujenzi wake.

Amezitaja sehemu hizo kuwa ni Tanga-Pangani kilomita 50, daraja la Pangani kilomita 525 na barabara unganishi kilomita 25.6, barabara ya Mkange-Mkwaja-Tungamaa kilomita 95.2 na sehemu ya Mkange-Bagamoyo Makurunge kilomita 73.25 ambayo usanifu wake umekamilika.

Kukamilika kwa barabara hii  kutachochea ukuaji wa uchumi, kupunguza gharama na muda wa safari, kuwezesha kufikika kwa urahisi vivutio vya utalii na kuunganisha kwa njia fupi bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mombasa.

Kamati hiyo pia ilikagua kivuko cha Pangani na kukiri kwamba kinahitaji kuboreshwa kama ambavyo wizara ya ujenzi imeomba ili kuwapa unafuu wananchi wa Pangani, ambao kwa sasa wanakutana na changamoto kwa kuwa kilichopo kinahitaji ukarabati.

Awali Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dk Charles Msonde amesema wanahitaji Sh2 bilioni ili kuboresha kivuko hicho.

Alipoulizwa endapo uhitaji wa kivuko hicho utakuwepo hata baada ya daraja kukamilika, Dk Msonde amesema daraja litakapokamilika kivuko hicho kitahamishiwa eneo Lingine lenye uhitaji.

Kamati hiyo imehitimisha ziara yake ya siku mbili mkoani Tanga ambapo imekagua miradi mitano ikiwamo bandari ya Tanga, uwanja wa ndege na reli.

Related Posts