Ndanga, mzee anayetembelea kilomita mbili kila siku kufuata gazeti la Mwananchi

Iringa. Mzee Pascal Ndanga, (90), ambaye ni mkazi wa mtaa wa Kijiweni, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, ameendelea kuwa mfano wa kupenda habari, akitembea kila siku umbali wa kilomita 2 ili kufuata nakala za gazeti la Mwananchi.

Kwa miaka mingi, Mzee Ndanga amejiwekea utaratibu wa kufuatilia habari za ndani na nje, akisema anapenda zaidi kusoma habari za kihistoria.

Akizungumza na Mwananchi Leo Machi 14, 2025, Ndanga alizaliwa Februari 18, 1935 katika Kata ya Mgama wilayani Iringa, anapenda sana kusoma gazeti la Mwananchi kwa sababu ya habari zake mchanganyiko na za uhakika.

Amesema amekuwa mfuatiliaji wa gazeti hilo tangu kuanzishwa kwake (2000) na hupenda zaidi sehemu za kihistoria zinazozungumzia matukio ya zamani na ya sasa, kama historia za makabila mbalimbali. 

Amewaomba wazalisha wa Mwananchi kuendeleza usimamizi wake na kuboresha magazeti yake kwa manufaa ya jamii.

“Nashukuru kwa kupata nakala za Mwananchi kila siku na niwaombe waendelee na utawala bora ili kuboresha magazeti yao. Hii inahitajika sana ili kuongeza uwazi na kuendeleza habari za ukweli,” amesema. 

Aidha, Mzee Ndanga amegusia changamoto ya vijana kutopenda kusoma magazeti kama ilivyokuwa kwa wazee wa zamani ambapo ameeleza kuwa wengi hutumia muda wao kwa shughuli nyingine tofauti na kusoma magazeti, jambo ambalo linapaswa kubadilika ili kuendeleza utamaduni wa kusoma kujua kinachoendelea katika jamii.

Amesema ikitokea amesafiri na yupo nje ya Iringa na kakosa nakala ya gazeti la Mwananchi, akirejea Iringa hufika katika ofisi za Mwananchi mkoani humo na kununua nakala za alizozikosa.

Mzee Ndanga baada ya kuhitimu elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari ya Tosamaganga baadaye alipata elimu ya biashara, uhasibu na uchumi katika Chuo cha British Tutorial Collage Nairobi, Kenya kutoka 1960 mpaka 1965. Anasema elimu hiyo ilimsaidia katika kazi zake za baadaye.

“Nilimaliza shule yangu ya sekondari huko Tosamaganga na baada ya hapo nilijikita kwenye uhasibu, ambao ulinisaidia sana katika kazi zangu,” amesema. 

Mzee huyo amesema alifanya kazi muda mrefu katika Wizara ya Fedha, mhasibu wa Ofisi za Bunge kuanzia mwaka 1966 hadi 1977 na baadaye aliendelea kufanya kazi katika mashirika mbalimbali ya umma hadi mwaka 2015 alipostaafu.

Priva Kassian ambaye ni muuzaji wa magazeti kutoka Samora, mkoani Iringa, anasema Mzee Ndanga ni mteja wake wa mara nyingi huonekana akifurahia kupata gazeti la Mwananchi.

“Mzee huyu kila anapofika kununua nakala yake, huwa ni mwenye kufurahia kupata habari za kila siku,” amesema Priva.

Kwa upande mwingine, Hamza Gwandi, Wakala wa Kampuni ya Mwananchi Communications mkoani Iringa, amesema kuwa amemfahamu Mzee Ndanga kwa muda mrefu kama msomaji maarufu wa gazeti hilo.

 “Mzee Ndanga ni mteja wetu wa muda mrefu. Haipiti wiki moja bila kutufikia hapa ofisini na kuchukua nakala za gazeti. Yeye ni mfano mzuri wa mtu anayejua umuhimu wa kusoma magazeti,” amesema Gwandi.

Related Posts