Kimbembe cha mikopo kausha damu mitaani

Dar es Salaam. Ndani ya kipindi cha takribani miezi mitatu kumeibuka wimbi la malalamiko kuhusu mikopo umiza maarufu kausha damu, huku baadhi ya viongozi wa serikali za mitaa wakisema mengi yanaibuka baada ya wananchi kushindwa kulipa madeni.

Malalamiko hayo kwa mujibu wa wenyeviti wa mitaa, yanatokana na wakopeshaji kuchukua mali za watu wanaoshindwa kulipa mikopo, zikiwamo samani za ndani ambazo mara nyingi thamani yake inazidi kiasi cha fedha zilizokopwa.

Wakati kukiwa na malalamiko hayo, tayari Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imekataza taasisi za fedha na watu binafsi kukopesha bila kuwa na vibali, ikitangaza taasisi zaidi ya 20 ilizozifungia kutoa huduma ya mikopo mitandaoni.

Katika kukabiliana na hilo, BoT na Wizara ya Fedha inatoa elimu kwa wananchi kuwapa uelewa wa masuala ya fedha, kujitambua na kuziripoti taasisi zinazotoa mikopo bila vibali stahiki.

Hatua hiyo ya Serikali ni matokeo ya mijadala mbalimbali ikiwemo iliyoibuka bungeni kuitaka BoT kudhibiti mikopo ya aina hiyo inayoumiza wananchi na kuwaingiza katika umaskini.

Akichangia mjadala wa Mwananchi X Space ulioandaliwa na Mwananchi Communications Limited (MCL) wiki hii, Marius Alphonce, Mwenyekiti wa Mtaa wa Tabata Kimanga Darajani, jijini Dar es Salaam alisema katika kipindi cha miezi mitatu ya uongozi wake tangu Novemba mwaka jana, amepokea malalamiko 40 kuhusu mikopo ‘kaushadamu.’

Alisema malalamiko hayo yanatokana na baadhi ya wakopaji kushindwa kutekeleza masharti ya mikopo waliyochukua, huku wengine wakifilisiwa na kudaiwa katika hali inayoibua kero.

“Mikopo hii imekuwa rahisi kwa sababu ya upatikanaji wake ndiyo maana wananchi wanaikimbilia, japokuwa kwa uhalisia kampuni au taasisi zinazoitoa masharti yake ni magumu na riba yake ni kubwa na inatakiwa kuanza kulipwa kwa muda mfupi baada ya kukopeshwa,” alisema Alphonce.

Alisema amekaa kikao na wakopeshaji mtaani kwake ili kupata suluhisho la changamoto inayowakabili wakopaji, lakini hawakufikia muafaka kwa sababu watu hao hawana leseni wala vibali vya kufanya biashara hiyo.

Katika Mtaa wa Yangeyange, Kata ya Msongola, wilayani Ilala, mwenyekiti wa mtaa huo, Mrisho Goha amesema amepokea malalamiko zaidi ya 60 kuhusu mikopo hiyo.

Licha ya idadi ya malalamiko anayopokea, amesema ni vigumu kuyatatua, kwa kuwa baadhi yanahusisha jinai, hivyo hulishirikisha Jeshi la Polisi.

“Wanapokopeshana hawashirikishi ofisi za mtaa, kwenye kudaiana anakuja mdaiwa analalamika kachukuliwa vitu usiku,” anasema.

Katika tukio moja anasema mdaiwa mali zake zilichukuliwa saa nane usiku, lakini akadai ameibiwa.

Anasema mkopeshaji alishindwa katika tukio hilo kwa kuwa alikwenda kuchukua mali za mdaiwa bila kibali wala taarifa kufikishwa ofisi ya serikali ya mtaa husika.

“Niliwauliza waliochukua vitu vya mwananchi kama walikuwa na kibali, jibu likawa hapana. Nilitaka kujua kama walipita kwenye ofisi zetu jibu likawa hapana, niliwahesabu kama wametenda kosa la jinai,” anasema.

Anasema malalamiko hufika ofisini baada ya mali za mdaiwa kuchukuliwa kwa kushindwa kulipa deni.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mjimwema wilayani Kigamboni, Daruesh Mohamed amesema ndani ya miezi mitatu aliyokaa madarakani amepokea malalamiko mawili kuhusu mikopo hiyo.

“Malalamiko yanakuwa mengi kwenye jamii kwa sababu mtu anapokuwa na shida ya haraka hafikirii kuangalia masharti ya mkopo anaochukua hata inapotokea ameshalipa asilimia 80 na kushindwa, kilichobaki wanataka kuchukua kitu cha thamani kubwa kuliko deni,” anasema.

Anasema ili kutatua changamoto, wakopaji wanapofika ofisini kwake kuomba barua, huwauliza iwapo wamesoma masharti ya mkopo na kama hawajafanya hivyo huwarudisha wakasome.

Anasema wanaoathiriwa zaidi na aina hiyo ya mikopo ni wajasiriamali wanaotafuta mtaji kwa ajili ya kuanza biashara, ilhali wenyewe hawana kianzio.

“Nimekuwa nikitoa darasa kwa wajasiriamali wasichukue mkopo kama hawana vya kuanzia, haiwezekani mtu anachukua mkopo wa Sh100, 000 akaanzishe biashara ya mihogo, hana hata karai wala jiko, hiyo pesa ni wazi hawezi kufanyia kitu,” anasema Mohamed.

Mwenyekiti wa wenyeviti wa mitaa ya Dar es Salaam, Juma Mwingamno amesema tangu alipoingia madarakani kwa awamu hii, amepokea malalamiko 15 kuhusu mikopo hiyo.

Miongoni mwa aliyoshuhudia anasema ni mwananchi kufungua malalamiko ya wizi wa kuaminiwa kwa sababu alikuwa anadaiwa mkopo.

“Nilikwenda hadi kituo cha polisi ambacho mwananchi alikuwa amewekwa mahabusu, nikamhoji ofisa mikopo aeleze kama kweli mwananchi aliiba au walikopeshana kinyume cha utaratibu,” amesema.

Katika tukio hilo, amesema mwananchi huyo alikopa Sh120,000 akitakiwa kulipa riba ya Sh70,000 kwa muda mfupi na inakuwa mara tatu ya fedha aliyochukua.

Mwingamno amesema mwingine alichukuliwa mtungi wa gesi ambao hadi leo upo ofisini kwake baada ya muhusika kusafiri, akimpa onyo mkopeshaji kutorudia kuchukua vitu kwa kuwa haifanani na fedha alizokopesha.

Amesema mwingine alikopeshwa Sh150,000, aliposhindwa kulipa alitakiwa kuchukuliwa mali yenye thamani ya Sh500,000.

“Kilichowakuta hao watu wameona wapite mitaani kimya kimya kwa sababu wanaogopa kuja kwangu,” amesema.

Sababu wingi wa malalamiko

Ofisa Mkuu Msimamizi wa Fedha, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha katika Wizara ya Fedha, Salim Kimaro amesema ongezeko la wananchi wanaolalamikia mikopo hiyo ni matokeo ya juhudi za Serikali kutoa elimu.

Anasema kwa sasa Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na BoT, ipo katika mkoa wa 15 kutoa elimu kwa wananchi kuhusu athari za mikopo hiyo na taasisi zinazokopesha bila kuwa na vibali stahiki.

Katika elimu hiyo, anasema wanawafundisha wananchi namna ya kuripoti, wanawajengea uelewa kuhusu sekta ya fedha na utambuzi wa taasisi zinazokopesha kinyume cha utaratibu.

“Hawa kaushadamu na wengine, Serikali kwa sasa inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhakikisha wanawaepuka wakopeshaji wasio na vigezo stahiki na tunawaelekeza namna ya kuwaripoti katika serikali za mitaa na maeneo mengine,” anasema.

Katika mazingira hayo, anasema lazima uelewa wa wananchi uongezeke, lakini hata idadi ya malalamiko itaongezeka.

Mwajuma Mwinyimkuu anayeishi Mjimwema, Dar es Salaam, alijikuta akiangukia kwenye maombi kutafuta nafuu ya deni la kaushadamu aliloshindwa kulipa.

Kwa mujibu wa Mwajuma, alikopa Sh200,000 kumtunza rafiki yake aliyekuwa na sherehe na mkopeshaji alimpa masharti ya dhamana inayozidi thamani ya alichokopa na aliweka kabati la nguo na televisheni.

Katika mkopo huo, anasema alitakiwa kulipa Sh3,000 kila siku na wakati anakopa aliamini isingepita siku atakayokosa kiasi hicho kwani alikiona kidogo.

Hata hivyo, anasema ulifika wakati alishindwa kupata rejesho la siku na mateso ndipo yalipoanzia.

“Kila nikilipa naona deni haliishi na ile kero ya kufuatwa kila siku, kuna wakati nilikuwa nakimbia,” anasema.

Anasema alijaribu kila mbinu kutafuta huruma ya mkopeshaji, ikiwemo kuandika tangazo mlangoni kwake kuwa amefiwa, anaugua na hatua ya mwisho alikwenda kwa mchungaji kufanyiwa maombi.

Mbinu hizo kwa mujibu wa Mwajuma, zililenga kumsahaulisha mdeni, lakini kila kitu alichoweka kama dhamana kilichukuliwa.

Luck Andrew anayeishi Mabibo, Dar es Salaam anasema mikopo imemaliza samani zake za ndani.

Mkasa wa Luck unahusisha mikopo ya kausha damu aliyoichukua kwa vipindi vitatu tofauti, hakuna hata mmoja kati ya hiyo aliofanikiwa kuulipa zaidi ya samani zake kuchukuliwa.

“Nilikopa Sh150,000 nikiwatambia jirani zangu kwa kula vizuri na kumpa pesa ya shule mwanangu nikitakiwa kulipa Sh2,500 kila siku nilifanikiwa kulipa Sh70,000 hiyo nyingine nilikuwa nawasumbua wakachukua friji niliyopewa zawadi kwenye harusi,” anasema.

Baadaye, anasema aliingia deni lingine la Sh250,000 kwa masharti ya kulipa Sh5,000 kila siku, kama ilivyokuwa awali alishindwa kulipa wakachukua kitanda na godoro.

Hakuishia hapo, anasema alikopa mkopo mwingine akaweka dhamana televisheni na hadi sasa anaendelea kudaiwa na analipa kwa fedha ya kula anayopewa na mwenza wake.

“Ukopaji kama ugonjwa halafu wanaotukopesha wanakuja na lugha nzuri ya ushawishi hata kama hutaki unajikuta unaingia mkenge tena wanasema mkopo hauna riba kubwa kama wengine lakini tukishakopa tu mambo yanabadilika,” anasema.

Uamuzi wa kukopa, Luck anasema unafikiwa baada ya kukumbwa na shida, hata hivyo hapati muda wa kusoma vigezo na masharti kutokana na haraka aliyonayo.

Related Posts