*Aitaka Bodi kutekeleza majukumu kwa kuzingatia sheria, sera na miongozo inayotolewa na Serikali
*Mkurugenzi
Mkuu asema NSSF inatekeleza azma ya Rais Dkt. Samia ya kuongeza wigo wa
hifadhi ya jamii kwa kuwafikia wananchi waliojiajiri
Na MWANDISHI WETU,
Dar
es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na
Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete, amezindua Bodi ya Wadhamini ya
Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na kuitaka kutekeleza majukumu
yake kwa kusimamia sheria, sera, kanuni na miongozo mbalimbali
inayotolewa na Serikali.
Uzinduzi
wa Bodi hiyo umefanyika tarehe 14 Machi, 2025 jijini Dar es Salaam na
kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Afisa Mtendaji Mkuu wa ATE,
Bi. Suzanne Ndomba, Naibu Katibu Mkuu TALGWU, Bw. Wandiba Ngocho,
Mwakilishi kutoka Benki Kuu ya Tanzania na Mwakilishi kutoka Msajili wa
Hazina pamoja na Menejimenti ya NSSF.
Mhe.
Ridhiwani ameitaka Bodi hiyo pia kusimamia Mpango Mkakakati wa Mfuko
unaozingatia uboreshaji wa huduma ya wanachama, michango, uwekezaji na
kulipa mafao.
Naye,
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba amesema Mfuko unaendelea
kutimiza azma ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais
Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza wigo wa hifadhi ya jamii na
kuwafikia wananchi waliojiajiri waweze kujiunga na kuchangia ili
wanufaike na mafao mbalimbali yanayotolewa na Mfuko.
Amesema
suala la wananchi kujiunga na kuchangia katika mifuko ya hifadhi ya
jamii ni ajenda ya dunia na ya nchi na kuwa lipo kwenye Ilani ya
Uchaguzi ya Chama, ambapo Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe,
Rais Dkt. Samia imelipa umuhimu wa pekee.
“Ninakushukuru
Mhe. Waziri kwa namna ambavyo umelishikia bango jambo hili,
umeshirikiana na sisi tangu tuanze kampeni yetu ya “NSSF Staa wa Mchezo”
kuhakikisha waliojisajili wanakuwa sehemu ya hifadhi ya jamii kama
ambavyo nchi zilizoendelea zimewasajili wananchi waliojiajiri,” amesema
Bw. Mshomba.
Amesema
kwa mujibu wa malengo 17 ya dunia, kila lengo linazungumzia masuala ya
hifadhi ya jamii kwa sababu ili uweze kuondoa umasikini ni hatua ya
kwanza wananchi wa taifa husika wawe ni wanufaika wa hifadhi ya jamii,
kwa sababu kupitia hifadhi ya jamii mwanachama au mwananchi wanakuwa na
uhakika wa maisha na kipato.
“Ndio
maana tunasema “NSSF Staa wa Mchezo” kwa maana ukiwa mwanachama wa NSSF
wewe utang’aa, utakuwa Staa katika maisha yako yote, wakati ukiwa na
nguvu za kufanya kazi na hata baada ya kumaliza kufanya kazi, NSSF
inakuwa Staa wa kukupa pensheni ya uzee, hivyo nawaomba wananchi
waendelee kujiunga na kuchangia ili wawe Mastaa wa Mchezo wa sasa na
baadaye.
Naye,
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye
Ulemavu, Bi. Mary Maganga amewataka wajumbe wa Bodi kusimamia Mfuko kwa
uadilifu na kuzingatia maslahi mapana ya wanachama.
Mwenyekiti
wa Bodi ya Wadhamini ya NSSF, Bi. Mwamini Malemi ameahidi kufanya kazi
kwa kufuata sheria, sera na miongozo iliyopo kwa mustakabali wa Mfuko.