Ahukumiwa kifo kwa mauaji ya hawara aliyedai alimvuta nyeti

Mtwara. “Kuna nyakati katika maisha hatima huchukua mkondo usiotarajiwa, ikiacha maumivu na maswali yasiyo na majibu. Rashid Mkumba (shahidi wa kwanza wa Jamhuri) hakuwaza kuwa Aprili 14, 2022 ingekuwa siku ya mwisho kumuona mkewe mpendwa, Mwajuma Lipala (marehemu)”

Ndivyo anavyoianza hukumu Jaji Martha Mpaze wa Mahakama Kuu katika kesi ya mauaji namba nane ya mwaka 2023 inayomkabili Said Ngamila.

Katika hukumu aliyoitoa Machi 13, 2025 katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mtwara na nakala ya hukumu kupatikana kwenye tovuti ya Mahakama, Jaji Mpaze amemhukumu Ngamila, mkazi wa wilayani Mtwara kunyongwa hadi kufa kwa kosa la kumuua Mwajuma katika ugomvi uliosababishwa na wivu wa mapenzi.

Jaji Mpaze akirejea ushahidi uliotolewa mahakamani amesema Mkumba na Mwajuma Aprili 14, 2022 walitoka pamoja kwenda shambani hawakujua iwapo kuna janga litatokea.

Amesema walipofika shambani kila mmoja aliendelea na kazi yake, Mkumba alimucha Mwajuma shambani, yeye akaenda msitu jirani kukusanya fito za kutengeneza kitanda cha kwenye kibanda chao.

Aliporejea hakumkuta Mwajuma akamtafuta pasipo mafanikio, hivyo akatoa taarifa kwa uongozi wa kijiji.

Jaji Mpaze amesema kwa msaada wa wanakijiji walifanya msako wa kina hadi Aprili 16, 2022 walipoukuta mwili wa Mwajuma ukiwa umezikwa nje ya nyumba ya Ngamila (mshtakiwa na shahidi wa kwanza wa utetezi) katika kesi hiyo.

Jaji amesema mwili ulikuwa umekatwa vipande, kichwa na miguu vilikosekana na kwa wakati huo, Ngamila hakuwepo nyumbani.

Baada ya taratibu zote za polisi na uchunguzi wa kitabibu kukamilika, familia ilipewa ruhusa ya kuchukua mabaki kwa ajili ya mazishi.

Dk Benedicta Daudi (shahidi namba nne wa Jamhuri), aliyefanya uchunguzi wa mwili wa marehemu, alieleza chanzo cha kifo kilikuwa kupoteza damu nyingi, jambo lililosababisha moyo kushindwa kufanya kazi. Alitoa ripoti ya uchunguzi wa mwili iliyopokewa kama kielelezo cha kwanza cha upande wa mashitaka.

Amesema msako wa muuaji uliendelea. Hata hivyo, kwa mujibu wa shahidi wa kwanza wa upande wa utetezi, ambaye ni mshtakiwa katika kesi hiyo baada ya muda akiwa mafichoni, aliamua kujisalimisha kwa viongozi wa kijiji.

Baadaye alikabidhiwa kwa Polisi, ambao baada ya kukamilisha uchunguzi walimfikisha mahakamani kwa shitaka la kumuua Mwajuma Aprili 14, 2022.

Akichambua ushahidi wa kesi, Jaji amesema mshtakiwa aliposomewa shitaka la kuua kwa kukusudia na kutakiwa kujibu kama ni kweli au la alisema:

“Mimi ni kweli kabisa nilimuua Mwajuma Ally Lipala, huyu ni mwanamke aliyekuwa ananitaka kimapenzi.”

Katika utetezi, alisema Mwajuma alifika nyumbani kwake akiwa na mundu, akimtuhumu kuwa na mahusiano na wanawake wengine.

Kwa hasira, alisema Mwajuma alimshika sehemu zake za siri huku akiwa bado ameshikilia mundu. Akiwa na hofu, alichukua mkuki aliokuwa akiutumia kujilinda dhidi ya wanyama wakali na kumchoma.

Baada ya kushtushwa na kitendo hicho, hakujua la kufanya. Akifahamu uzito wa jambo hilo, aliamua kumzika marehemu.

Alisema alichimba shimo, akamweka ndani na kufukia kwa udongo. Baadaye, alipojaribu kuhamisha mwili na kuona kuwa ni mzito, aliamua kuukata vipande ili kurahisisha usafirishaji.

Alifafanua kuwa alizika kiwiliwili nje ya nyumba yake, huku kichwa na miguu alivizika msituni alikochimba shimo la kina kifupi.

Akiogopa matokeo ya kitendo alichofanya, hivyo alikimbilia mafichoni ndani ya pango.

Mshtakiwa alisema alikiri kwa baba yake mzazi kufanya mauaji na baadaye alitafuta msaada kutoka kwa wachungaji wa mifugo waliomwelekeza kwa mwenyekiti wa kijiji.

Alisema mwenyekiti alimpeleka kituo cha afya kwa usalama, ambako baadaye alikamatwa na Polisi.

Akiwa kituoni, alikiri kosa na kushirikiana na Polisi kwa kuwaelekeza maeneo aliyozika viungo vya mwili wa marehemu.

Katika utetezi alisema hakukusudia kumuua Mwajuma, akieleza ilikuwa ni ugomvi wa kimapenzi uliozidi mipaka.

Kwa nini anastahili kunyongwa

Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili, Jaji amesema hakuna ubishi kuwa kwa ushahidi uliotolewa, Mwajuma ni marehemu na kifo chake hakikuwa cha kawaida na hii ni kulingana na ushahidi wa mshtakiwa na taarifa ya chanzo cha kifo.

“Ukipitia ushahidi wa upande wa Jamhuri na wa mshtakiwa mwenyewe, hakuna ubishi kuwa mtu pekee anayewajibika na kifo cha Mwajuma Ally Lipala siyo mtu mwingine zaidi ya mshtakiwa,” amesema Jaji Mpaze na kuongeza:

“Ingawa hakuna ushahidi wa moja kwa moja wa mtu aliyeona akifanya mauaji hayo, ushahidi wa mazingira uliotolewa na shahidi wa tatu, Haji Abdallah Ngamila ambaye ni baba wa mshtakiwa unamuhusisha moja kwa moja mshtakiwa.”

Kwa mujibu wa Jaji, shahidi huyo aliieleza mahakama kuwa siku ya mwisho ambayo marehemu (Mwajuma) hakuonekana na mshtakiwa naye hakuonekana nyumbani kwake.

Alisema alipokwenda nyumbani kwake alibaini uwepo wa shimo na udongo mbichi.

Alitoa taarifa polisi ambao baadaye aliongozana nao hadi eneo aliloona uwepo wa shimo lenye udongo mbichi na lilipofukuliwa, mwili wa marehemu ulikutwa na ufukuaji huo ulishuhudiwa pia na mume wa marehemu.

“Hoja hapa ni je, alifanya tendo hilo akiwa na nia ovu? Upande wa mashitaka umeleta ushahidi mzito kuonyesha mshtakiwa alifanya mauaji hayo akiwa na dhamira ovu. Namna mauaji yalivyofanyika ni wazi nia ovu ilikuwepo,” amesema.

Jaji Mpaze amesema: “Mshtakiwa alitumia mkuki kumpiga nao marehemu kabla ya kwenda kutenganisha kichwa, kiwiliwili na miguu kwa kutumia shoka kitendo ambacho huwezi kukataa kuwa hakuwa na dhamira ya kuua.”

“Kukiri kwake kosa kuwa alichukua mwili na kuutenganisha shingo, kiwiliwili na miguu na kuvizika viungo hivyo katika maeneo tofauti  huko msituni inaonyesha zilikuwa ni njama za makusudi za kutaka kupoteza ushahidi,” amesema jaji na kuongeza:

“Katika utetezi wake, mshtakiwa anakiri kumuua Mwajuma kwa madai alimtishia kwa kumvuta sehemu zake za siri akiwa ameshika mundu na kutoa matamshi ya vitisho na kwamba yeye alichokifanya ilikuwa ni kujilinda.”

Amesema: “Sheria ya utetezi wa kujilinda inataka majibu dhidi ya shambulizi lazima yalingane na tishio lenyewe. Lakini tukitizama alivyojibu kwa kumshambulia na mkuki haileti uwiano wa kujilinda kwa kujitetea kama anavyodai mshtakiwa.

“Hakuna ushahidi wa wazi kuwa maisha yake (mshtakiwa) yalikuwa hatarini ili kuhalalisha nguvu ya utetezi aliyoitumia. Pamoja na utetezi wake huo mahakama inaona kumshambulia marehemu kwa mkuki hailingani na kitisho anachosema.”

Amesema mshtakiwa alikuwa na fursa ya kutafakari kile alichokifanya lakini aliamua kuendelea mbele na kukatakata mwili na kuutenganisha.

“Ukichanganya matukio haya yanadhihirisha bila kuacha mashaka kuwa alidhamiria kutenda mauaji,” amesema.

Jaji amesema katika utetezi wake, licha ya kukiri kumuua marehemu (Mwajuma), alisema alimtishia kwa kumvuta sehemu zake za siri, huku akiwa ameshika mundu na kutoa vitisho. Kwamba hilo linatosha kuhalalisha kujitetea.

“Lakini sheria ya kujitetea inapaswa iwe na uwiano na kitisho kilicho mbele yako,” amesema.

Jaji amesema utetezi wa kwamba alifanya hivyo akijitetea hauwezi kusimama kutokana na nguvu ya ziada aliyoitumia kabla na baada ya mauaji.

Ni kutokana na uchambuzi huo, Jaji Mpaze amesema anaona upande wa mashitaka umetimiza wajibu wao kuthibitisha shitaka dhidi ya mshtakiwa pasipo kuacha mashaka, hivyo anamtia hatiani na kumuhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.

Related Posts