Mwanza. Ujenzi wa kituo kikuu cha utafutaji na uokozi ndani ya Ziwa Victoria umefikia asilimia 80, ukitoa matumaini ya kuokoa maisha wakati vyombo vya majini vinapozama ziwani humo.
Kwa mujibu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac) zaidi ya watu 5,000 hufariki dunia kwa ajali zinazotokea ndani ya Ziwa Victoria kila mwaka katika kwa nchi zinazochangia ziwa hilo ikiwamo Tanzania, Kenya na Uganda.
Kutokana na vifo vitokanavyo na ajali majini, nchi za Afrika Mashariki (Tanzania, Uganda na Kenya) zimekubaliana kwa pamoja kutekeleza mradi huo, unaoratibiwa na Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC).

Akizungumza jana Machi 14, 2025 kwenye kikao maalumu cha makubaliano ya nchi ya Kenya kuingia tena kwenye mradi huo baada ya kujitoa mwaka 2021, Katibu Mtendaji wa LVBC, Dk Masinde Bwire amesema mradi huo utakuwa mwarubaini wa vifo ndani ya Ziwa Victoria, vinavyotokana na vifaa hafifu vya uokozi na mawasiliano.
Ametaja baadhi ya ajali zilizotokea ndani ya ziwa hilo na kusababisha vifo vya watu wengi kutokana na uokozi na vifaa hafifu ni ya MV Bukoba iliyotokea Mei, 1996 na kuua zaidi ya abiria 800, ajali ya Mv Nyerere iliyotokea Septemba 20, 2018 na kuua abiria 228 na watu wengine 19 kufariki dunia kwa ajali ya ndege ya shirika la Precision iliyoanguka katika Ziwa Victoria ikiwa inajiandaa kutua mjini Bukoba, zote za nchini Tanzania.
Ajali nyingine ni ya Novemba 24, 2018 ambapo MV Templar ilipinduka nchini Uganda na kuua zaidi ya abiria 30, ajali ya boti iliyoua watu zaidi ya 20 Agosti 2, 2023 baada ya boti yao kupinduka walipokuwa wakisafiri kando ya Ziwa Victoria kutoka Wilaya ya Kalanga kuelekea Kasenyi nchini Uganda.
Ameeleza pia Septemba, 2021 watu 10 walifariki kutokana na ajali ya boti kwenye ufukwe wa Pier Beach Homabay nchini Kenya.
“Hata uokoaji na nyenzo ulikuwa hafifu kama kamisheni iliyoaminiwa na nchi zetu kuratibu kupitia jumuiya tumeamua kuwekeza na kuondoa hiyo changamoto. Kwa sasa hivi mradi umekamilika kwa asilimia 80, vifaa vya uokoaji na boti ya kisasa vimeshawekwa,” amesema Dk Bwire

Muonekano wa kituo kikuu cha uokoaji na ufuatiliaji kinachojengwa Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza na nchi ya Tanzania, Uganda na Kenya kwa uratibu wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC).
Dk Bwire amesema pamoja na vifaa vya kisasa vitakavyowekwa, pia minara na vifaa vya mawasiliano vitasimikwa katika kituo hicho kinachojengwa Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.
Amesema kitakapokamilika kituo hicho kama Jumuiya ya Afrika Mashariki na Kamisheni watakuwa wamepiga hatua kubwa katika kuimarisha mifumo ya uokoaji, uchukuzi na usafirishaji ndani ya ziwa hilo.
“Mradi umegharimu Dola za Marekani milioni 1.9 kama Sh4 bilioni za Kitanzania … hivyo ukikamilika hizo zitakuwa gharama za uwekezaji, kutakuwa na gharama pia za uendeshaji,” ameongeza.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi nchini Tanzania, Ludovick Nduhiye amesema mradi huo utakuwa na mfumo wa haraka wa kupeana taarifa pamoja na vyombo vya kufanya uokozi.
“Mradi unalenga kutengeneza miundombinu ya mawasiliano na namna ya kupeana taarifa zaidi katika kufanya uokozi yanapotokea majanga, wote tunafahamu ziwa letu limekuwa likikumbwa na majanga mengi na watu wengi wanakufa,” amesema
Kenya kujitoa, kurudi kwenye mradi
Awali mradi huo ulikuwa ukitekelezwa na nchi tatu za Tanzania, Kenya na Uganda kwa miaka minne kuanzia mwaka 2018 ulipozinduliwa.
Kenya ilijitoa mwaka 2021 baada ya mapitio ya mradi huo yaliyofanyika kati ya Mei 2020 na Septemba 2021, na hivyo kubaki ukitekelezwa na nchi mbili ya Uganda na Tanzania.
“Hapo awali nchi ya Kenya ilijiondoa kwenye ujenzi wa kituo hiki na uwekezaji lakini kama mnavyojua Ziwa ni kubwa hakuna namna yoyote nchi ya Kenya inaweza kujitoa kwenye utekelezaji wa mfumo wa pamoja, hivyo mabaraza ya mawaziri wa kisekta zinazoshughulikia Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria liliilekeza Kenya ijumuishwe na tunashukuru Mungu ilikubali,” amesema Dk Bwire
Mwenyekiti wa makatibu wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambaye pia ni Katibu Mkuu wa sekta ya Usafirishaji na Uchukuzi nchini Kenya, Geoffrey Kaituko amesema awali walijitoa kwenye mradi huo kwa kuwa nao walikuwa wanatekeleza mradi kama huo Kisumu, lakini sasa wameungana na nchi ya Tanzania na Uganda kuukamilisha.