Unguja. Jeshi la Polisi Mkoa wa Kusini Unguja linawashikilia watu watano kwa tuhuma za kuwazuia watu wasijiandikishe kwenye daftari la wapiga kura na kufanya fujo kwenye kituo cha kuandikisha wapigakura.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Daniel Shillah ametoa taarifa hiyo leo Machi 15, 2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya Polisi ya Mkoa huo. Amesema wanaoshikiliwa wanadaiwa kuwa wanachama wa ACT Wazalendo.
Amesema, kati ya watuhumiwa hao, watatu walisimama kwenye njia ya kuingia kwenye kituo cha kujiandikisha na kuwazuia wananchi wasijiandikishe kwa madai kuwa watu hao wana asili ya Tanzania Bara, huku wakijua kuwa hawana mamlaka ya kufanya hivyo.
“Watuhumiwa hao ni Ramadhan Hassan Rajabu (58), Mohamed Pandu Ameir (43), Ameir Kishaji Ameir (60) wote wakazi wa Jambiani Mzuri na Khamis Haji Juma (56) mkazi wa Muyuni, hao waliwazuia watu wasijiandikishe huko Muyuni A na Jambiani Kibigija,” amesema Shillah
Mwingine, Alli Abdalla Mkwende anadaiwa kufanya vurugu kwa kutoa lugha za vitisho na kuwapiga picha watendaji wa kituo cha Tasani Makunduchi, kitendo ambacho kinadaiwa kililenga kuvuruga uandikishaji.
Vilevile, Kamanda Shillah amesema Jeshi la Polisi linaendelea kuwatafuta watuhumiwa wengine wanaodaiwa kuwanyang’anya wananchi vitambulisho ili wasiweze kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura.
“Watuhumiwa watatu walikamatwa na kuhojiwa na kukiri kufanya hivyo wakiamini kuwa watu waliokuwa wakiwakamata na kuwazuia wasiingie kujiandikisha walikuwa hawana sifa,” amesema Shillah.
Hata hivyo, pamoja na changamoto hizo zilizojitokeza, amesema shughuli ya uandikishaji imemalizika salama na kuwa wananchi ambao ndio walengwa walipewa fursa kwa mujibu wa sheria kujiandikisha na kuhakiki taarifa zao.
Kamanda Shillah ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuwa watulivu na kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili kudhibiti vitendo vya uvunjifu wa amani na watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa.
Akitoa taarifa juu ya mwenendo wa uandikishaji wa wapiga kura kwa awamu ya pili, Wilaya ya Kusini Unguja, Naibu Katibu Mkuu ACT Wazalendo Zanzibar, Omar Ali Sheha amesema mawakala wawili wa Chama hicho na kiongozi mmoja watawi walikamatwa na jeshi la polisi wakidaiwa kujihusisha na uvunjifu wa amani.
Chama hicho kilidai kuwa katika Wilaya hiyo lilijitokeza wimbi kubwa la watu kutoka Tanzania Bara wanaotaka kuingizwa katika daftari hilo.
Amesema kundi hilo lilipewa vitambulisho feki vya Mzanzibari mkazi (ZAN ID) kwa lengo la kujiandikisha wakati Tume ya Uchaguzi ZEC ilishatoa makadirio ya kuandikisha watu.
Pia, chama hicho kimetaka walioshikiliwa waachiliwe huru.
Hassan Fadhila Suleiman ni Sheha wa Shehia ya Nganani amesema ndani ya kituo uandikishaji ulikwenda salama ila changamoto hizo zilijitokeza nje ya kituo kwa Mawakala wa akiba na watu kupokonywa vitambulisho vyao.
“Yupo mtu ambaye ni wakala mwenza wa chama cha ACT Wazalendo amewapokonywa mtu na mkewe vitambulisho vyao wakati wanakuja kujiandikisha,” alisema.
Nao baadhi ya wananchi wanaodaiwa kukutwa na changamoto hiyo walisema wakati wakiwa njiani kuelekea kituo cha kujiandikisha alitokea mtu na baiskeli na kujitambulisha kuwa ni mtu wa serikali na kuwahoji kwamba wanakwenda kituoni na kuwataka kutoa vitambulisho vyao.
Emanuel Kinyaja Sapili alisema mtu huyo alijifanya kama anaongea na simu na mtu na baadaye alikimbia na vitambulisho vyao.
Akitolea ufafanuzi kuhusu watu wanaotilia mashaka uhalali wa kuandikishwa baadhi ya wananchi, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Jaji Joseph Kazi, amesema iwapo kuna watu hawakubaliani na au wanawatilia shaka wanatakiwa kuwawekea pingamizi baada ya daftari hilo kuwekwa wazi lakini hakuna mwenye mamlaka ya kunyang’anya kutambulisha
“Baada ya uandikishaji Tume tutatoa daftari wazi kwa wale wote waliondikishwa hivyo yoyote ambae ataona kuna mtu hana sifa na ameandikishwa basi anaweza kuweka pingamizi na ZEC itasikiliza na kupokea ushahidi basi mtu huyo ataondolewa,” alisisitiza Jaji Kazi
Mwenyekiti huyo alibainisha kuwa Sheria ya uchaguzi imeweka utaratibu wa kuwapinga wale wote ambao wanaonekana kama hawana sifa ya kujiandikisha katika shehia husika,.
“Baada ya uandikishaji tume tutaoa daftari kwa wale wote walioandikishwa hivyo yoyote ambae ataona Kuna mtu Hana sifa na ameandikishwa basi anaweza kuweka pingamizi na ZEC itasikiliza na kupokea ushahidi basi mtu huyo ataondolewa,” alisisitiza.
Hivyo, amewataka wananchi kufuata sheria na kuwaacha wale wote wanaojitokeza na wana sifa za kuandikishwa waweze kupata fursa hiyo.