WINGA wa TP Mazembe, Philip Kinzumbi amezungumzia taarifa za kutakiwa na Yanga akisema kwa mzuka uliopo ndani ya timu hiyo ni vigumu kukataa ofa yao.
Akizungumza na Mwanaspoti kwa simu, Kinzumbi ambaye ana umri wa miaka 25, amesema ingawa bado hajaanza rasmi mazungumzo na Yanga, lakini kama timu hiyo itamalizana na TP Mazembe fasta atajiunga na mabingwa hao wa Tanzania.
Mchezaji huyo ameeleza kuwa tangu alipokutana na Yanga kwenye Kombe la Shirikisho Afrika msimu mmoja uliopita amekuwa akivutiwa na timu hiyo baada ya kuuona ubora wa kikosi na pia mzuka wa mashabiki.
Yanga inatajwa kuvizia saini ya Kinzumbi ambaye ni fundi anayemudu kucheza winga ya kushoto ambapo mashabiki wa mabingwa hao wa Tanzania wanamhusudu kwa ubora wake.
Katika kuelekea dirisha la usajili lijalo, Yanga inapiga hesabu za kusajili winga wa kushoto atakayekuja kuchukua nafasi ya Msauzi Mahalatse Makudubela ‘Skudu’ ambaye anatajwa huenda akaachana na Yanga mwisho wa msimu huu.
“Yanga waliwahi kunifuata muda mrefu, lakini kwa sasa hawajarudi tena ingawa tuna tabia ya kusalimiana na viongozi wao. Mimi ni mchezaji wa Mazembe bado nina mkataba hapa na ninaheshimu mkataba wangu. Lakini kama Yanga watamalizana na Mazembe nitajiunga nayo haraka,” amesema Kinzumbi ambaye amedumu katiak timu hiyo tangu msimu wa 2020-21.
“Yanga ni timu kubwa tangu nilipokutana nao kwenye mechi za Shirikisho tulicheza nao mechi mbili niliona jinsi ilivyo nzuri. Ina kikosi bora na mashabiki wao nawapenda. Wanapenda timu yao sana.
“Tuko na wachezaji hapa walicheza Yanga kama Serge (Mukoko). Kuna mambo mengi mazito mazuri huwa anasema kuhusu Yanga ambayo kama ni mchezaji utapenda kufanya kazi hapo.”
Kinzumbi amekiri kwamba mezani kwake kuna ofa nyingi zikiwamo za kutoka klabu za Afrika Kaskazini, lakini anachosubiri ni timu ipi itamalizana na TP Mazembe.
“Nimekaa sana hapa Mazembe, nina ofa nyingi za nchi za Uarabuni, lakini bado hazijafika mwisho. Kama klabu itakuja na kumalizana na Mazembe nitaweza kuondoka mara moja kwenda kutafuta changamoto mpya,” amesema.