BEKI wa Simba Chamou Karaboue amewashusha presha mashabiki wa klabu hiyo, hata kama Che Malone Fondoh hatakuwepo lakini amejipanga vizuri kuhakikisha anaendeleza ubora kwenye ukuta wa timu hiyo.
Chamou ambaye alitua Simba msimu huu, amekuwa miongoni mwa mabeki ambao hawapati muda mwingi wa kucheza, baada ya kukuta mastaa wanaokiwasha zaidi yake katika maeneo hayo.
Simba ambayo imecheza mechi 22 za ligi chini ya Kocha Fadlu Davids, kati ya hizo ni michezo tisa tu ambayo beki huyo alianza, huku zilizobakia akianzia benchi.

Hapo awali Mwanaspoti iliandika kuhusu beki wa kati tegemeo wa Simba, Che Fondoh Malone ambaye alipata majeraha katika mechi dhidi ya Azam FC na taarifa ya muda gani atakuwa nje ikiwa bado haijajulikana.
Akizungumza na Mwanaspoti, Chamou ambaye inadaiwa kuwa mrithi wa Che Malone, alisema kwa sasa ameshazijua timu nyingi na namna ya kucheza nazo.
Alisema, maelewano na Abdulrazack Hamza ni mazuri kwani muda mwingi aliokuwa akipata nafasi alicheza nae na hata Che Malone, hivyo alihitaji muda wa kumuelewa zaidi na ameupata.
“Ukuta wetu upo imara kuhakikisha hatutoki kwenye njia ya malengo yetu tuliyojiwekea, nacheza kwa maelewano mazuri na mabeki wenzangu kwa sababu nimeshawasoma.

“Ukizingatia viungo wetu wa juu ni watu wanaojua kutupunguzia presha kama Kagoma na Ngoma, hivyo nataka kutumia mechi hizi ambazo Che Malone hatakuwepo uwanjani kuthibitisha kwamba mimi ni beki sahihi kuitumikia Simba,” alisema Chamou ambaye bado hajafanikiwa kufunga wala kutoa pasi ya bao kwenye kikosi cha Simba msimu huu.