Wanaume wanaolia balaa kwa mapenzi

Wataalamu wa masuala ya mapenzi wamebaini kuwa wanaume wenye hisia kali kiasi cha kudondokwa na machozi kwa sababu ya wapenzi wao, huishia kuwa na uhusiano thabiti wa kimapenzi.

Hii ni kinyume na dhana ya kipindi kirefu kuwa wanaume wenye misuli na kifua kilichotanuka ndio huwaniwa na wanawake kutokana na maumbile yao ya kupendeza.

“Sasa mambo yamebadilika, imebainika kuwa wanaume wanaodondokwa na machozi hata kwa mambo madogo wana utu, wenye huruma na hunogesha mapenzi,” anasema Marina Lazaris, mtaalamu wa masuala ya mapenzi ambaye pia ni mchapishaji wa jarida la ‘Wanaume Huhitaji Mapenzi’ linalochapishwa nchini Marekani.

“Kutofautisha kati ya hisia ya kumwonea mtu imani, huruma na mwenendo wa zamani ambapo maumbile ndio huzingatiwa kama kigezo cha kupenda, ni jambo ambalo limeanza kuwachanganya wanaume,” anasema mtaalamu mwengine Adam Cohen Aslatei wa shirika la Tawkify nchini humo.

Mtaalamu huyo anatoa ufafanuzi kuwa kumpata mwanaume ambaye hisia zake ni thamani kwake, kutawasaidia wanawake kuwapata wapenzi wa kudumu.

Mara nyingi wanawake wamelalamikia hatua ya baadhi ya wanaume kuwahadaa kwa kuanzisha uhusiano nao kimapenzi kisha kuwahepa.

Hii ni kwa sababu wanaume hao hawathamini hisia zao na hawaingii katika uhusiano huo na roho yote.

Kizazi cha sasa cha Gen Z kinaonekana kubadili utamaduni wa wanaume wazuri kuonekana kuwa ni wale waliojaa misuli na kutanuka kifua maarufu kama ‘six pack’.

Sasa wanawake wanawathamini wanaume ambao wanaweza kudondokwa na machozi kwa sababu yao. 

Ni wale wanaowathamini sana na hutetea haki zao kwa kukemea dhuluma wanazopitia katika jamii.

“Sasa mambo si kujaza misuli na kutanuka kifua au kuwa mwanaume mwenye msimamo mgumu. Sasa ni uaminifu, mwanaume mlinzi, mwenye heshima na yule ambaye hisia zake zinaonyesha wazi mapenzi kwa mwanamke,” anaongeza Lazaris.

Mtaalamu huyo anasema mabadiliko hayo yameanza kushuhudiwa kote ulimwenguni kwa sababu wanaume wengi sasa hawafichi hisia zao kwa hofu ya kuchekwa kama ilivyokuwa zamani.

Amina Abdallah, mkazi wa Kimara jijini Dar es Salaam, anasema kuwa kulia kwa mwanaume ni tendo ambalo ni nadra kutokea au kufanywa na mwanaume.

Hivyo kwake anatafsiri tendo hilo la mwanaume kulia, kama ishara ya kuonyesha uhakika na msisitizo wa jambo analozungumza au kulitenda.

“Mwanaume akizungumza jambo huku akitoa machozi ujue anamaanisha kwa sababu ni jinsi ya watu  wagumu kuonyesha hisia zao iwe ya furaha au huzuni, ”anasema.

Magdalena John mkazi wa Sinza pia jijini humo,  anasema huwa anafurahi na kujiona wa kipekee anapomuona mwanaume akilia kwa ajili yake.

“Kama tumegombana na akaniomba msamaha huku akilia huwa ninatafsiri kuwa amemaanisha msamaha anaoumba,”anaeleza.

Hata hivyo, kwa  Zaruna Ali, kulia kwa mwanaume si kigezo cha kusema ana mapenzi ya dhati kwa mwenza wake.

Anasema wapo baadhi yao hawamaanishi kile wanachokitolea machozi na  aghalabu hutumia machozi yao kama njia ya kuwalaghai wanawake.

“Mwanaume anaweza kulia  yakawa ni maigizo tu ili aweze kupata anachokitaka, hivyo ni muhimu mwanamke kuwa makini,”anasema.

Peter Peter,  mkazi wa Chanika,  anasema kitendo cha mwanaume kulia, kwa sababu ya mapenzi katika jamii nyingi kinatafsiriwa kama kitendo cha udhaifu.

“Katika jamii nyingi, kuna dhana kwamba mwanaume anapaswa kuwa na nguvu; asionyeshe hisia, na adumishe ukakamavu hata katika mazingira ya kihisia, ”anasema.

Naye, Khalid Socha anasema mwanaume anaweza kutoa machozi ili aweze kupata huruma ya mwanamke na asimaanishe kama kweli na mapenzi ya dhati.

“Wanawake wana hulka ya huruma hawapendi kuona mtu anaumia,  hivyo baadhi ya wanaume wakitaka kupata mambo yao kutoka kwa mwanamke,  wanaweza kutumia machozi ili wafanikiwe”anasema. 

Anachosema mtaalamu wa uhusiano

Mtaalam na mshauri wa masuala ya uhusiano, Eva Mrema anasema kitendo cha mwanaume kulia mbele ya mpenzi wake,  kinaweza kumaanisha mapenzi ya dhati kwa upande mmoja  au ulaghai  kwa upande mwingine akisisitiza hayo yote hutegemea  nia pamoja na hisia zake.

Anasema mwanaume anaweza kulia kwa mpenzi wake akiashiria upendo huruma na kuthamini kama nia ndani ya moyo wake ni ya  kweli na yenye uthabiti.

Lakini pia anasema machozi ya mwanaume,  yanaweza kutumika kwa ajili ya kumlaghai mwanamke ili aweze kuaminika na kupata huruma kutoka kwa mpenzi wake.

“Hivyo ni muhimu kwa mwanamke kuwa makini siyo kila mwanaume anayelia anamaanisha hicho anachokililia,”anaeleza.

Related Posts