Nafasi ya elimuhisia kwa wazazi na walimu

Katika miaka ya hivi karibuni, pameanza kuwepo msisitizo mkubwa kwenye elimu ya hisia.

Nchi nyingi zilizoendelea, kwa mfano, zimetenga bajeti kubwa katika tafiti kwa mamia zinazoangazia ukuaji wa hisia na kusaili uhusiano wake na ujifunzaji.

Miaka ya nyuma, tunafahamu, wataalamu wengi wa elimu waliweka uzito mkubwa kwenye kukuza uelewa wa mtoto na namna ya kumsaidia mtoto kufikiri vizuri.

Pamoja na umuhimu wake, msisitizo huu haukutambua umuhimu wa utimamu wa hisia za mtoto katika ujifunzaji.

Tafiti, hata hivyo, zinaonesha kuwa mtoto mwenye utimamu wa hisia anakuwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kufanya vizuri kwenye masomo kuliko mtoto mwenye changamoto ya hisia.

Uwezo mkubwa wa kudadisi, kufikiri, kuelewa, kukumbuka na kujifunza katika upana wake, unategemea namna gani mtoto anajisikia salama, ana furaha, amani na utulivu.

Elimu hisia ni maarifa anayokuwa nayo mtoto yanayomwezesha kuelewa hisia zake, kumudu hisia zake, kuelewa athari ya hisia zake kwa wengine, kushirikiana na wengine na hivyo kuwa na uwezo mzuri wa kushughulikia changamoto za mahusiano yake na watu.

Elimu hii huanza kupatikana nyumbani anamokulia mtoto kupitia namna wazazi wanavyohusiana naye.

Tafiti zinaonesha kuwa mzazi mwenye upendo kwa mtoto, anayemfanya mtoto ajisikie kupendwa na kujaliwa, hujenga msingi mzuri wa mtoto kuwa na uwezo mkubwa wa kumudu hisia zake.

Kadhalika, elimu hii hupatikana kupitia michezo ya mtoto na wenzake. Kadri anavyojichanganya na wenzake na kucheza, mtoto hupata mazingira wezeshi yanayomsaidia kujifunza vizuri namna ya kuelewa hisia za wenzake, kuziheshimu na kujifunza namna ya kumudu hisia zake zisiharibu mahusiano yake na wenzake. Hapa ndipo ulipo umuhimu mkubwa wa michezo kwa watoto.

Ndio kusema, elimu ya hisia si elimu rasmi inayopatikana kupitia mtaala unaofundishwa darasani bali maarifa anayoyapata mtoto kupitia mahusiano yake na watu wanaomzunguka yanayomfanya ajisikie salama, mwenye uhuru wa kuchunguza mazingira yake bila kujisikia wasiwasi wala hofu.

Katika utafiti mmoja iligundulika kuwa mtoto wa miaka minne hadi sita hujifunza kwa ufanisi kuhusu hisia zake kuliko hata mtu mzima.

Kupitia ukaribu wake na mzazi, kwa mfano, mtoto hujifunza kuelewa hisia zake, kuelewa hisia za mzazi wake na kuzitumia kwenye mahusiano yake na mzazi.

Kwa msingi huo, elimuhisia huanza mapema mtoto angali akiwa mikononi mwa wazazi. Malezi yanayozingatia hisia za mtoto, tafiti zinasema, yanakuwa mfano wa chanjo ya dhidi ya hatari za afya ya akili kwa mtoto, kwa maana ya kumkinga na tishio la hofu, sonona na msongo wa mawazo.

Kwa upande mwingine, malezi yanaweza kuwa mwiba mkali dhidi ya elimu ya hisia. Matukio ya watu kujiua, kwa mfano, yanahusishwa na changamoto za afya ya akili zinazotokana na kujisikia wapweke, kukata tamaa, kushindwa kushughulikia hali zinazoathiri hisia zao kwa wakati. Matatizo haya mara nyingi huanzia pale wazazi wanaposhindwa kuwafanya watoto wasione sababu ya kuwa na wasiwasi na usalama wao.

Mtoto, baada ya kuanza shule, hutumia muda mwingi akiwa shuleni. Huko shuleni anakutana na watoto wanaotoka kwenye familia tofauti tofauti wenye maadili na tabia ambazo wakati mwingine hukinzana na kile alichojifunza kwao.

Pia anakutana na watu wazima, walimu na walezi wengine, ambao kwa kuzingatia uwezo wao kwenye safari ya mtoto kitaaluma, hugeuka kuwa na nguvu kubwa ya kuamua afanye nini.

Katika mazingira kama ambayo taaluma na ufaulu vinabeba matarajio makubwa ya walimu na wazazi, upo uwezekano mkubwa wa nguvu hii kukandamiza hisia za mtoto.

Kwa kuzingatia hali kama hii, nchi mbalimbali zilizotambua umuhimu wa hisia za mtoto zimebuni miradi mbalimbali yenye kuhakikisha kuwa hisia za mtoto zinakuzwa na pale ambapo mtoto anaonekana kuwa na changamoto anasaidiwa kupata elimuhisia.

Mfano wa mipango hii ni ule unaotwa SEL (Social-Emotional Learning) ambao, pamoja na mambo mengine, unalenga kuwasaidia watoto kujitambua kwa maana ya kutambua na kumudu hisia zao, kubaini na kumudu hisia za wenzao, kufanya uamuzi, na kuishi vizuri na wenzao na kadhalika. Tafiti zinaonesha kuwa miradi kama hii ina mchango mkubwa katika kuwasaidia watoto kuwa na utulivu, uchangamfu na uwezo wa kushirikiana na wenzao, na matokeo yake ni kufanya vizuri kwenye masomo yao.

Ingawa miradi muhimu kama hii haijashika kasi hapa nchini, bado tuna nafasi ya kuangalia uwezekano wa kujenga mazingira yanayowawezesha wataalam wetu wa eneo hili kuwawezesha walimu kuangazia elimu hii ya hisia kwa watoto.

Ufaulu mkubwa usioendana na elimuhisia, tafiti zinasema, hauwezi kumsaidia mtoto kufanya vizuri kwenye maisha yake baada ya elimu. Pengine umefika wakati watunga sera na wasimamizi wa elimu kulizingatia hili.

Related Posts