Dar es Salaam. Mtoto akikosea anatakiwa kuadhibiwa au kuadabishwa? Huu ni mjadala ulioshika kasi kwa sasa kukiwa na msukumo mkubwa wa kuondolewa adhabu ya viboko kwa kile kinachoelezwa haina matokeo chanya kwa anayeadhibiwa.
Adhabu hiyo ambayo hutumika zaidi shuleni na wakati mwingine nyumbani inatajwa kuwa si tu huishia kumletea maumivu ya kimwili mtoto husika, bali humuathiri kisaikolojia na kumtengenezea hofu badala ya kumfundisha na hofu hiyo inaweza kwenda hata kwa watoto wengine wanaoshuhudia.
Mjadala huu unakuja kukiwa na matukio ya vifo vya wanafunzi vinavyodaiwa kusababishwa na adhabu kali za viboko ambavyo vinatolewa kinyume na mwongozo wa utoaji adhabu shuleni na matukio mengine ya ukatili wanayofanyiwa watoto nyumbani.
Mfano wa matukio hayo ni lile llilotokea Februari 26, 2025 katika Shule ya Sekondari Mwasamba iliyopo wilaya ya Busega mkoani Simiyu ambapo ambapo inadaiwa kuwa Mduhu alifariki dunia baada ya kuchapwa viboko 10 na kukanyagwa kichwani na mwalimu wake aitwaye Salim Chogogwe.
Mwanafunzi huyo alikumbana na adhabu hiyo baada ya kushindwa kufanya kazi za vikundi iliyotolewa na mwalimu huyo ambapo kwa mujibu wa mmoja wa wanafunzi waliokuwepo eneo la tukio, Mduhu alipigwa fimbo za kichwani na mgongoni kisha kukanyagwa.
Mkurugenzi wa C-Sema Tanzania Michael Mwarwa amesema kutojiamini kwa wanafunzi wengi wa shule za msingi na sekondari ni matokeo ya woga unaosababisha na adhabu ya viboko ana adhabu nyingine zinazotweza utu wao hivyo kuathirika kisaikolojia.
“Hakuna utafiti wowote wa kisayansi ambao unaonesha mtoto akipigwa au akipewa adhabu ya viboko anakuwa na akili, msikivu na mwenye nidhamu, lakini kuna tafiti za kisayansi zinaonesha mtoto akipewa malezi mazuri, akiadabishwa anakuwa mwenye akili, kujitambua na kujiamini,”amesema Michael.
Mkurugenzi huyo ambaye shirika lake linahusika kupokea kesi za ukatili anasema katika kipindi cha Januari na Februari wamepokea malalamiko 52 yanayohusu ukatili kwa watoto.
“Kupitia namba ya bure ya 116 kazi yetu ni kupoke kesi zinazohusu matukio ya ukatili, kwa upande huu wa watoto katika kipindi cha miezi miwili tumepokea malalamiko 52 yanayohusu ukatili dhidi ya watoto. Aina za ukatili zilizoripotiwa ni kupigwa, kung’atwa na kuchomwa moto sehemu mbalimbali.
Ukweli ni kwama adhabu hailengi kumfundisha mtoto zaidi ya kumuumiza, sasa usitegemee kupata matokeo ya kudumu kama utampa maumivu ya kimwili na kihisia lakini ukimuadabisha kwa kumpa kazi za mikono itamsaidia na siku zote itabaki kichwani mwake” anasema Marwa.
Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (Tenmet) Martha Makalla amesema licha ya juhudi mbalimbali za kuhamasisha matumizi ya mbinu mbadala za malezi na nidhamu, vitendo vya ukatili dhidi ya wanafunzi na watoto bado vinaendelea kushuhudiwa ndani ya shule nchini, jambo linaloashiria udhaifu katika utekelezaji wa miongozo na sheria zinazosimamia haki za mtoto ndani ya mfumo wa elimu.
Anasema kuongezeka kwa matukio haya pia kunachangiwa na baadhi ya wazazi kutokuwa na utayari kuyaripoti matukio ya aina hii katika vyombo vya dola ili hatua sitahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa kwa wahusika.
“Wazazi wasio tayari kutoa taarifa wamekuwa wakifanya mazungumzo na familia za watuhumiwa nje na utaratibu uliopo kisheria na wakati mwingine wamekuwa wakipokea fedha zinazodaiwa za matibabu au fidia kinyume cha sheria, tunaomba wanaofanya vitendo hivi waache na badala yake watoe taarifa kwa vyombo vya dola,”amesema Martha.
Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Flugence Masawa amesema adhabu za viboko zimekuwa ni moja ya sababu za kuongezeka kwa utoro shuleni, hivyo ipo haja kwa serikali ikomeshe adhabu hizi ili kuhakikisha wanafunzi wanabaki shuleni, wanandelea na masomo na kukamilisha mzunguko wao wa Elimu katika ngazi husika bila vitisho vyovyote.
Kufuatia hilo ametaka Serikali iwekeze katika adhabu mbadala zisizotweza utu wala kutishia maslahi ya watoto na wanafunzi kwa ujumla.
“Serikali ifuatilie pia adhabu zingine ambazo sio za viboko lakini ni mbaya na zinatweza utu wa watoto na kuwasababishia maumivu ya muda mrefu ya kimwili, kisaikolojia na kiakili.
“Wizara ya Elimu kupitia ofisi ya kamishina wa elimu iviimarishe vitengo vya udhibiti ubora wa elimu ikiwa ni pamoja na kutenga bajeti ya kutosha, upatikanaji wa vitendea kazi na utolewaji wa mafunzo ya mara kwa mara ili kuhakikisha kwamba wanatekeleza majukumu yao kikamilifu” amesema Masawe na kuongeza
“Pia Wizara ya Elimu, Sayansi, na Teknolojia itoe waraka rasmi unaoelekeza walimu wote kuacha matumizi ya adhabu za viboko yaliopitiliza na kuelekeza mbinu mbadala za nidhamu zinazolinda utu na haki za watoto wakati mchakato wa marekebisho ya Sheria ya Elimu ukiendelea”.
Muelimishaji wa afua zinazoleta tija kwenye elimu Neema Kitundu anasema mtoto anapokosea anaweza kuadabishwa kwa kupewa kazi itakayomfanya asirudie kosa alilofanya.
“Kazi utakayompa kulingana na umri wake itamfanya asifikirie kurudia tena kosa alilofanya, mfano kazi ya bustani, usafi na shughuli nyingine zitakazomtofautisha na wenzake na kumfanya ajutie kosa alilolofanya bila kumdhuru mwili,” anasema Neema.
Mshauri kutoka shirika la Hakielimu Dk Wilberforce Meena anasema badala ya kumchapa mwanafunzi viboko kwa sababu hakufanya kazi za darasani mwalimu anaweza kumuongezea kazi zaidi na kuuchukua muda wake wa mapumziko.
“Mfano mtoto hakufanya kazi ya darasani, unaweza ukamzuia asiende mapumziko ule muda wake wanacheza yeye unampa kazi nyingine ya kufanya au muda wenzake wanatoka yeye anabaki darasani kufanya zoezi ulilompa. Hii itamfunza, wakati mwingine akitaka kuacha kufanya kazi aliyopewa atakumbuka kilichomkuta,” anasema.