Dar es Salaam. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limesema kuna changamoto katika ununuaji wa Luku kupitia mitandao ya simu huku likitoa njia mbadala ya kupata huduma hiyo.
Taarifa ya Tanesco imetolewa leo Jumapili Machi 16, 2025 na Kurugenzi ya Mawasiliano na Huduma kwa Wateja huku ikiahidi kuitatua changamoto hiyo.
“Shirika linawataarifu wateja wake kuwa, kuna changamoto katika ununuzi wa umeme unaosababisha wateja kushindwa kununua umeme kupitia mitandao ya simu na njia za kibenki kuanzia leo majira ya saa tatu asubuhi,”inaeleza taarifa hiyo.
Shirika limewashauri wateja kufanya ununuzi kupitia mawakala wake walioko nchi nzima wakati wataalamu wakiendelea na jitihada za kurekebisha changamoto iliyojitokeza.
Aidha, Tanesco imeomba radhi kwa usumbufu wowote unaojitokeza.