VINARA na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara Yanga, wanatarajiwa kuzindua Uwanja wao mpya wa Singida Black StarsĀ uliopo Mtipa mjini Singida, katika mchezo wa kirafiki utakaochezwa Jumatatu ijayo ya Machi 24, mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Singida Black Stars, Hussein Massanza ilieleza uwanja huo wa kisasa unalenga kuinua maendeleo ya mpira wa miguu nchini, huku ukitarajiwa kuhudhuriwa pia na viongozi wa Serikali.
“Uwanja huu ni sehemu ya dhamira ya Singida ya kuwekeza katika maendeleo ya michezo kwa kutoa mazingira bora kwa wachezaji, mashabiki na jamii kwa ujumla, umejengwa kwa viwango vya mashindano makubwa ya kitaifa na kimataifa pia.”
Massanza alisema anawaalika wadau wa michezo kuhudhuria tukio hilo la kihistoria, ambalo litakuwa na burudani mbalimbali hususani ya mchezo huo wa kirafiki kati ya timu hiyo dhidi ya Yanga ambao ndio wageni waalikwa kwenye uwanja huo mzuri.
Uwanja huo unaelezwa unaingiza mashabiki 7000, huku Singida ambayo mwanzoni ilikuwa inatumia Liti kwa michezo yake mbalimbali ya msimu huu, ikiwa na lengo la kuanza kuhamishia majeshi uwanjani hapo unaoelezwa ni wa kisasa. Singida itaungana na KMC na Azam kuwa timu ambazo zinamiliki viwanja vyao wenyewe.