NYOTA wa Kitanzania, Athuman Masumbuko ‘Makambo’ amesema amesaini mkataba wa mwaka mmoja na klabu ya SC Viktoria inayoshiruiki Ligi ya Ujerumani maarufu Hessenliga.
Awali nyota huyo wa zamani wa Mashujaa na Mtibwa Sugar ya vijana U-20, msimu uliopita alijiunga na 1.FCA Darmstadt ya nchini humo kwa mkataba wa miaka mitatu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Makambo alisema ni kweli amesaini mkataba na timu mpya ingawa hakuweka wazi kama alivunja mkataba na timu ya awali ama ilikuwaje.
“Hii ni timu yangu mpya na nashukuru mechi yangu ya kwanza nimecheza na kufunga bao, watu wafahamu nipo huku na niko tayari kuipambania timu yangu ifanye vizuri kwenye ligi na mashindano mengine,” alisema Makambo.
Makambo kabla ya kujiunga na chama hilo msimu wa 2023/24 aliichezea Mashujaa baada ya kuonyesha kiwango kizuri akiichezea timu ya vijana ya Mtibwa Sugar iliyobeba ubingwa huku akiibuka mfungaji bora kwa kutupia kambani mabao saba akiwa na kikosi hicho.