Kesi tuhuma za ulawiti nje ya nchi yakwaa kisiki kortini

Dodoma. Mahakama Kuu, masjala Kuu ya Dodoma, imeyatupa maombi ya Watanzania wawili, waliokuwa wanataka kurejeshwa nchini kwa raia wa Oman, Tariq Ahmed Alismail anayeshukiwa kumlawiti mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka saba.

Uamuzi huo umetolewa Machi 14, 2025 na Jaji Fredrick Manyanda akisema Mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza shauri hilo kwa kuwa limefunguliwa nje ya muda wa siku 14 ambao waombaji walipewa kibali cha kufungua maombi.

Kwa mujibu wa maombi hayo ya mapitio ya Mahakama, wanaomba Mahakama ifute amri iliyotolewa na mdaiwa wa kwanza na wa pili, ya kumkabidhi mtoto huyo mikononi kwa mama yake mzazi pamoja na mtuhumiwa.

Waombaji katika shauri hilo, Raawya Hermohamed Jalal na Saifa Ally, walidai Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), alitoa maoni batili kuwa Mahakama nchini hazina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo kwa kosa linalodaiwa kutendeka Oman.

Wajibu maombi katika shauri hilo namba 199227 la mwaka 2024 ni Waziri Nashiri ambaye ni Ofisa Maendeleo ya Jamii kama mjibu maombi wa kwanza na mtu aliyetajwa kwa jina la Water Amandus Kayombo kama mjibu maombi wa pili.

Pia, aliunganishwa askari mwenye cheo cha Sajini, WP Diana mwenye namba WP.8726 kama mjibu maombi wa tatu na Mkuu wa Kituo (OCS), Kituo cha Kati cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kama mjibu maombi wa shauri hilo.

Wengine waliokuwa wameunganishwa ni Mkuu wa Upelelezi (RCO) na Kamanda wa Polisi (RPC) Kanda maalumu ya Dar es Salaam, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Mkurugenzi wa Upelelezi nchini (DCI), DPP na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo, waombaji wote 10 waliwakilishwa na mawakili Werema Kibaha na Eric Akaro wakati wajibu maombi wakiwalishwa na mawakili wa Serikali, Omary Ngatanda, Agnes Makuba na Dunsan Mkisa.

Nini walichokuwa wanaomba

Waombaji katika shauri hilo walikuwa wakiiomba Mahakama itoe amri kuwa kitendo cha mdaiwa wa 1,2,3,4,5,6 na 7 cha kusimamisha na kufunga upelelezi uliokuwa ukiendelea wa tukio hilo ni kinyume cha sheria na taratibu za kiupelelezi.

Walikuwa wanadai kitendo cha wajibu maombi hao kumkabidhi mtoto (mwathirika) kwa mama yake mzazi ilikuwa kinyume na amri iliyotolewa na Mahakama ya watoto Kisutu jijini Dar es Salaam kiliathiri haki ya mtoto huyo.

Katika kiapo chao cha pamoja, walikuwa wakiomba Mahakama iamuru mwenendo wa uchunguzi ufufuliwe na kuendelea na mtoto anayedaiwa kufanyiwa vitendo hivyo arudishwe Tanzania pamoja na mtuhumiwa.

Pia, walitaka Mahakama itoe amri kuwaelekeza wajibu maombi namba 3,4,5,6,7,8 na 9 kufufua upya jalada la uchunguzi huo na kuamuru kukamatwa kwa mtuhumiwa ambaye ni raia wa Oman na hakuna jitihada za kumrejesha nchini.

Mbali na maombo hayo, lakini waleta maombi wanataka wajibu maombi hayo kwa pamoja, waamriwe kumrejesha nchini mtoto aliyefanyiwa vitendo hivyo vya ulawiti, ambaye alichukuliwa kwa nguvu akiwa chini ya waombaji hao wawili.

Kabla ya Jaji Manyanda kuanza kusikiliza shauri la msingi, mawakili wa wajibu maombi waliwasilisha hoja ya kisheria kuwa, shauri hilo limefunguliwa nje ya muda hivyo Mahakama hiyo haikuwa na mamlaka ya kisheria ya kulisikiliza.

Hoja hiyo iliibuliwa kupitia aya ya 15 ya kiapo cha wajibu maombi wa kwanza na wa pili na katika aya ya 20 ya kiapo cha wajibu maombi wa tatu hadi 10.

Akijibu hoja hiyo, wakili Werehema alijibu kwa kifupi kuwa maombi hayo hayakufunguliwa nje ya muda kwani ilifunguliwa ndani ya siku 14 tangu waleta maombi wapewe kibali Julai 24, 2024 cha kufungua maombi hayo ya mapitio.

Wakili Werehema alifafanua kuwa maombi ya msingi yaliwekwa kwenye mfumo wa Mahakama Agosti 6, 2024 na malipo yakafanyika Agosti 8, 2024 ambayo ilikuwa siku ya mwisho, hivyo maombi hayo yalifunguliwa ndani ya muda.

Wakili Werehema alisema hakuna ubishi kuwa mwathirika (jina la mtoto linahifadhiwa) ana umri wa miaka saba na ni Mtanzania wa kuzaliwa na alifanyiwa ukatili wa kingono akiwa mikononi mwa mama yake mzazi huko nchini Oman.

Alieleza pia kuwa ni jambo lisilobishaniwa pia suala hilo lilitolewa taarifa Kituo cha Kati cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na kupewa jalada namba CD/IR/209/2024 na mjibu maombi wa tatu (WP Diana) akapangiwa kupeleleza.

Wakili huyo akaeleza kuwa mjibu maombi wa pili (Kayombo) alifungua maombi namba 4038 ya 2024 katika Mahakama ya Watoto Kisutu na alipewa amri ya muda na baadaye akapewa haki kabisa ya kumtunza hadi Julai 28, 2024.

Kwamba tuhuma za kulawitiwa zilifanyiwa uchunguzi wa kitabibu na taarifa mbili zilizojazwa katika fomu ya polisi (PF3) zote zilithibitisha kuwa mtoto alilawitiwa au kosa la kuingiliwa kinyume cha maumbile lilithibitishwa na uchunguzi huo.

Hoja zinazobishaniwa kwa mujibu wa wakili ni kwamba, WP Diana alimhoji mtoto akiwa peke yake bila Ofisa Ustawi wa Jamii na alimtaja mshukiwa kuwa ni fundi bomba wa kihindi na hakutaja jina la baba yake wa kambo.

Pamoja na kwamba hakuwataja, lakini katika maelezo yao waliyoaandika polisi, waombaji walitoa taarifa za kutosha kuwa mshukiwa wa tukio hilo ni Tariq Ahmed Alismail, ambaye ni baba wa kambo wa mtoto huyo anaishi naye huko Oman.

Alieleza kuwa mjibu maombi wa 3- 10 hawakuwahi kutoa maelekezo ya kufunga jalada la uchunguzi au kufunga jalada hilo Machi 8, 2024 lakini sasa upelelezi umekamilika na DPP ameeleza Mahakama nchini haiwezi kusikiliza kesi hiyo.

Wakili huyo alieleza kuwa, wajibu maombi hao walishindwa kueleza ni kwa namna gani walifanyia kazi maoni ya DPP katika kuchunguza suala hilo kupitia polisi wa kimataifa kwa vile hakuna ripoti inayoonyesha ushiriki wao.

Akijibu hoja hizo, wakili wa Serikali, Agnes Makubi alisema kulingana na kanuni ya tatu ya GN namba 324/2014, amri zinazoombwa haziangukii chini ya mapitio ya Mahakama bali amri za kiutawala au prerogative orders.

Wakili huyo alisema kwa kupitia kiapo cha pamoja cha waombaji, hakuna maamuzi ambayo yanatakiwa kufutwa au kubatilishwa kwa sababu mjibu maombi wa tano (ZCO) hakuwahi kufunga jalada la upelelezi wa tuhuma hizo.

Kwa mujibu wa wakili huyo, hata kibali cha kufungua shauri hilo kilitolewa kimakosa kwa kuwa kulikuwa hakuna uamuzi uliokuwa umetolewa huku wakili Ngatanda akisema wajibu maombi walitekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria.

Wakili alisema ni jambo la kufikirika kuwa kulikuwa na uamuzi ulifanyika na kueleza Mahakama hiyo haiwezi kutoa amri zinazoombwa kwa kuwa ushahidi unaonyesha kosa la ulawiti lilitendeka nje ya nchi na “fundi bomba wa kihindi.”

Kuhusu ombi la kuamuru upelelezi uendelee na kumkamata mshukiwa wa kosa hilo, wakili Ngatanda alisema tayari wajibu maombi walishatimiza wajibu wao kwani walichunguza taarifa zilizotolewa na waleta maombi na jalada kufungwa.

Wakili huyo aliunga mkono kitendo cha maofisa wa Polisi kutomkamata Tariq Ahmed Alismaili akisema kulingana na Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) na Kanuni ya 24 ya PGO, mshukiwa anachukuliwa hana hatia.

Kuhusu hoja ya kuiomba Mahakama iamuru mtoto anayedaiwa kulawitiwa  kurejeshwa nchini, wakili huyo alisema mtoto alikabidhiwa kwa mama yake na mjibu maombi wa 1 na 2 hivyo ilikuwa si sahihi kushitaki wajibu maombi wengine.

Wakili Makubi akarudi tena na kuunga mkono hoja kuwa shauri hilo limefunguliwa nje ya muda akifafanua kuwa kibali kilitolewa Julai 24,2024 na maombi yakafunguliwa Agosti 6,2024 na ada ya maombi hayo kulipwa Agosti 7,2024.

Kulingana na wakili huyo, alisema kwa mujibu wa kanuni za ufunguaji mashauri kwa njia ya kielektroniki, shauri litahesabiwa limefunguliwa pale ada stahiki zinapokuwa zimelipwa na shauri hilo linahesabika lilifunguliwa Agosti 7, 2024.

Katika hukumu yake, Jaji alisema kwa kuwa kuna hoja ya kisheria imeibuka kuwa maombi hayo yamefunguliwa nje ya muda wa kisheria, Mahakama hiyo inawajibu wa kutoa majibu ya hoja hiyo kabla ya kushughulikia maombi ya msingi.

Jaji alisema hakuna ubishi kuwa Mahakama hiyo kupitia maombi namba 13565 ya 2024, ilitoa uamuzi wake Julai 24,2024 na haibishaniwi na mawakili wa pande mbili kuwa nyaraka zilipakiwa Agosti 6,2024 na kulipiwa ada Agosti 7,2024.

Kulingana na Jaji Manyanda, sheria iko wazi kuwa shauri litahesabika limefunguliwa kuanzia siku ambayo malipo ya ada yamefanyika na kwamba siku 14 ambazo waombaji walipewa kufungua maombi zilimalizika Agosti 6,2024.

Jaji alisema angeweza kushughulikia maombi ya msingi lakini kwa vile Mahakama inaona haina mamlaka ya kushughulikia maombi yaliyowasilishwa nje ya muda, Mahakama hiyo haina njia nyingine ya kufanya zaidi ya kuyatupa.

Related Posts