Mfanyakazi wa ndani ahukumiwa kunyongwa kwa kumuua dada wa mwajiri wake

Arusha. Mahakama ya Rufani imebariki adhabu ya kunyongwa hadi kufa aliyohukumiwa aliyekuwa mfanyakazi wa ndani wa kiume (houseboy), Robert Steven, kwa kumuua kwa kumnyonga mdogo wa mwajiri wake, Theopista Laurent, kisha kuiba vitu vya ndani na kukimbia.

Tukio hilo lilitokea Oktoba 15, 2021, katika Kijiji cha Rukabuye, wilayani Missenyi, mkoani Kagera, ambapo inadaiwa mrufani alikuwa akiishi na mke na mtoto wake nyumbani kwa Kagirwa Laurent.

Inadaiwa Oktoba 13, 2021, Kagirwa na mkewe walisafiri kwenda Chato, ambapo siku ya tukio, Robert aliingia ndani ya chumba alichokuwa amelala marehemu, akamyonga na kumfunika kitandani kwa shuka.

Baada ya kutenda kosa hilo, alipekua nyumba hiyo na kuiba vitu kadhaa, ikiwemo simu ya mkononi ya marehemu, mali nyingine za Kagirwa kama nguo, kamera, spika, simu za mkononi, na baadhi ya picha za familia ya Kagirwa, kisha kukimbilia Kijiji cha Kiluluma, wilayani Karagwe.

Kagirwa na mkewe waliporejea, walikuta nyumba yao imevurugika huku baadhi ya vitu vikiwa havipo. Walipoingia chumbani kwa marehemu, walimkuta amelala kwenye dimbwi la damu akiwa na kipande cha kitambaa shingoni.

Msako ulifanyika, na Oktoba 31, 2021, Robert alikamatwa katika Kijiji cha Kiluluma akiwa na baadhi ya mali hizo, alikiri kumuua marehemu na kuiba mali za mwajiri wake.

Robert alifikishwa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba na kushtakiwa kwa mauaji, ambapo baada ya Mahakama hiyo kusikiliza kesi hiyo, ilimkuta na hatia ya mauaji na kumhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.

Baada ya kutoridhishwa na adhabu hiyo, Robert alikata rufaa, ambapo rufaa hiyo ya jinai namba 742/2023 ilisikilizwa na jopo la majaji watatu wa Mahakama hiyo—Stella Mugasha, Abraham Mwampashi, na Paul Ngwembe. Majaji hao waliketi Bukoba na kutoa hukumu hiyo Machi 14, 2025.

Mahakama ya Rufani ilitupilia mbali rufaa hiyo baada ya kuona haina mashiko na kwamba adhabu iliyotolewa ilikuwa sahihi, hivyo kujiridhisha kuwa upande wa mashtaka umethibitisha kosa bila kuacha shaka yoyote.

Jaji Ngwembe alisema baada ya kukagua kumbukumbu za rufaa, kanuni za ushahidi wa kimazingira, na ushahidi wa ungamo pamoja na mawasilisho ya pande zote mbili katika rufaa hiyo, suala waliloangalia ni kanuni ya ushahidi wa kimazingira, hasa ikizingatiwa kuwa katika kesi hiyo, moja ya ushahidi uliowasilishwa ni wa kimazingira.

Alisema mojawapo ya kanuni nne zilizowekwa kisheria kuhusu ushahidi wa kimazingira ni kuwa ushahidi huo unaweza kumtia hatiani mshtakiwa ikiwa Mahakama itaridhika kuwa ushahidi huo, bila kupingwa, unaelekeza kwenye hatia ya mshtakiwa na kumtenga na mtu mwingine yeyote.

Jaji Ngwembe alisema katika rufaa hiyo, Kagirwa alidai kusafiri kwenda Chato na kumuacha mrufani (akiwa na mke na mtoto wao mmoja). Hata hivyo, aliporejea hakuwakuta, na badala yake alikuta mwili wa marehemu kwenye dimbwi la damu. Uchunguzi wa mwili wa marehemu ulionyesha kuwa kifo chake kilitokana na kunyongwa, na pia alipigwa na kitu kizito kichwani.

“Kama ilivyoonyeshwa awali, wakati mrufani akitoa utetezi wake, alijinasibu kuwa alishiriki kumuua marehemu na kuiba mali za Kagirwa, ambazo alikutwa nazo katika Kijiji cha Kiluluma, wilayani Karagwe. Tunaona ushuhuda kama huo ulikuwa ushahidi bora juu ya hatia yake,” alisema.

Jaji Ngwembe alisema katika rufaa ya jinai namba 110/2007 ya Paulo Maduka na wengine dhidi ya Jamhuri, Mahakama ilitamka kwamba shahidi bora zaidi katika kesi yoyote ya jinai ni mshtakiwa ambaye anakiri hatia yake.

Alisema kuwa Mahakama imejiridhisha kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha kesi hiyo bila kuacha shaka yoyote.

Katika utetezi wake katika Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Robert hakupinga kushiriki katika mauaji hayo, ila alidai alilipwa Sh1.5 milioni kutoka kwa Laurian Rukiza ili amuue marehemu. Baada ya kupokea kiasi hicho cha fedha, alishirikiana na Laurian kumuua Theopista.

Aidha, alikiri chini ya kiapo kuwa alikusanya mali za mwajiri wake na kutoroka, ambapo alikamatwa akiwa nazo.

Katika rufaa hiyo, Robert alikuwa na sababu saba, lakini wakati wa usikilizaji alibaki na sababu mbili ambazo ni jaji alikosea kisheria kwa kumtia hatiani mrufani kwa kosa la mauaji, huku upande wa mashtaka ukiwa umeshindwa kuthibitisha kesi hiyo bila kuacha shaka yoyote, kama inavyotakiwa na sheria.

Hukumu ya mrufani ilitokana na kukiri kosa bila ushahidi wowote huru unaomhusisha moja kwa moja na uhalifu huo.

Hata hivyo, baada ya Mahakama ya Rufani kupitia ushahidi uliowasilishwa, iliridhika kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha kesi hiyo kwa kiwango kinachotakiwa, hivyo kuthibitisha kuwa hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba ilikuwa sahihi.

Related Posts