Mradi wa jengo la mama na mtoto Geita wasuasua

Geita. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi imeitaka Wizara ya Afya kupeleka fedha za mradi wa jengo la mama na mtoto, njia za watembea kwa miguu na mfumo wa maji taka katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita kwa kuwa ujenzi wake umesimama tangu mwaka 2023 kutokana na changamoto za fedha.

Mradi huo ulioanza kutekelezwa Juni 2022 na kutakiwa kukamilika Juni 2023 unajengwa kwa Sh13 bilioni na hadi sasa Serikali imetoa Sh4.04 bilioni huku mkandarasi anayeutekeleza akidai hati ya malipo ya Sh160.5 milioni.

Kutokana na fedha kutopelekwa kwa wakati mwenyekiti wa kamati hiyo, Hassan Mtenga amemtaka Naibu Waziri wa Afya, Godwin Mollel kuikutanisha kamati hiyo na katibu mkuu Wizara ya Afya ili wajue changamoto na kuitatua.

“Tukae na katibu mkuu wako na waziri tukubaliane tuzungumzie suala la hii hospitali kwa sababu wenzangu wamesema walikuja mwaka jana na waliyoyakuta ni yaleyale, na mimi mwenyekiti sioni sababu ya kukagua kama ni ukuta tumeuona,”amesema.

Amesema Serikali inatoa kazi kwa makandarasi wa ndani lakini malipo yake yanatolewa kwa shida wakati makandarasi wamekopa fedha benki na riba zinaongezeka kila wakati.

Mtanga amesema Wizara ya Fedha inapaswa kutambua afya ni uti wa mgongo wa nchi kwa sababu inagusa maisha ya watu hivyo miradi yake ipewe kipaumbele na ilipwe kwa wakati.

“Rais anatafuta fedha na anatoa fedha kwa kiasi kikubwa akiwa na matarajio wananchi wake wanakwenda kupata huduma, nikuombe tena muite katibu mkuu tukae tuone mwelekeo,” amesema Mtenga.

Hoja ya kusuasua kwa ujenzi huo imeibuliwa na mjumbe wa kamati hiyo, Cecil Mwambe akisema mwaka 2024 walitembelea hospitali hiyo na walichokikuta kipindi ndio kilichopo sasa.

“Mwenyekiti hii inashtua hata fedha iliyopatikana kiasi kikubwa ni fedha kutoka kwa wafadhili. Serikali iliahidi Sh2.3 bilioni na sasa tumebakisha miezi miwili ya kukamiliisha bajeti na kama Bunge tuliiidhinisha hii fedha, hata hivyo wametoa Sh900 milioni kwa hali hii mtiririko wa fedha zinazokuja hapa sio mzuri,” amesema Mwambe ambaye pia ni mbunge wa Ndanda.

Mwambe amesema, Bunge limetekeleza wajibu wa kutenga fedha kwa ajili ya Hospitali ya Geita ili iweze kusaidia wananchi lakini fedha hiyo haijatoka na kuitaka Serikali kutoa fedha hizo kwa wakati ili ujenzi ukamilike.

“Mwaka jana tulipotembelea hapa mkandarasi alikuwa analalamika ana madeni makubwa, ametumia fedha yake amekopa benki kabla ya huyu alikuwa mkandarasi mwingine ambaye ni Wakala wa Majengo wa Serikali (TBA) aliyeshindwa kuendelea kutokana na changamoto hizi hizi za fedha,” amesema Mwambe.

Mhandisi kutoka Wizara ya Afya, Johnson Kamala amekiri uwepo wa mkwamo wa upatikanaji wa fedha akisema iliyolipwa sasa ilitokana na bajeti iliyopita.

Naibu Waziri wa Afya, Godwin Mollel amesema changamoto ya fedha kuchelewa inajulikana na sasa makandarasi wanaogopa kufanya kazi wakihofia  hela zao zitachelewa.

Mganga Mfawidhi wa Hospiitali ya Rufaa Geita, Kibwana Mfaume amesema mradi wa jengo la mama na mtoto ulianza Juni 2022 na ulitarajiwa kukamilika Juni 2023, lakini kutokana na changamoto za upatikanani wa fedha hadi sasa haujakamilika.

Amesema kukamilika kwa mradi huo kutaboresha huduma ya afya kwa wananchi hususan ya mama na mtoto na kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella amesema kwa miaka minne vituo vipya vya afya  84 vimejengwa Geita na kuwapunguzia wananchi adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma.

Related Posts