Dodoma. Umoja wa Walimu Wasio na Ajira (Neto) wa kati ya mwaka 2015 hadi 2023 umewasilisha mambo sita katika kikao cha mawaziri wawili, ikiwemo pendekezo la kupunguza umri wa kustaafu kwa walimu kutoka miaka 60 hadi 50 ili kutoa nafasi za ajira kwa vijana serikalini.
Mambo mengine yaliyowasilishwa katika andiko lao lenye kurasa 22 ni masuala ya mtalaa mpya, usaili wa ajira za walimu, uzalishaji wa walimu, hali ya maisha ya walimu wasio na ajira mitaani, na uhaba wa walimu.
Viongozi wa umoja huo walikutana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, pamoja na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda.
Katika kikao hicho kilichofanyika Machi 12, 2025, jijini Dodoma, Serikali ilikubaliana kuunda timu ya wataalamu kutoka wizara tano kushughulikia changamoto za walimu hao, huku wakiombwa kuwa wavumilivu kwa kipindi cha siku 30 hadi 45 ili timu hiyo ifanyie kazi yake.
Katika tovuti ya Utumishi wa Umma, Simbachawene alinukuliwa akisema kuwa timu hiyo itachambua maoni ya Neto ili kuyatumia kama sehemu ya upatikanaji wa suluhisho la tatizo la ajira kwa walimu.
Umoja huo ulizua mjadala katika mitandao ya kijamii baada ya Sekretarieti ya Ajira kuwaita kwenye usaili walimu waliotakiwa kujaza nafasi 14,648 zilizotangazwa na Rais Samia Suluhu Hassan ili kupunguza uhaba wa walimu nchini. Hatua hiyo ilimfanya Simbachawene kuwaita walimu hao ofisini kwake ili kuwasikiliza.
Katibu wa Neto, Daniel Mkinga, alisema katika andiko hilo walitoa pia mapendekezo ya nini kifanyike, na mawaziri hao waliwasikiliza na kuyapokea.
Amesema viongozi wengi wamekuwa wakisisitiza vijana wajiajiri, hivyo wanapendekeza umri wa kustaafu upunguzwe hadi miaka 50 ili waliostaafu warudi kujiajiri, kwani wameshapata mitaji, na vijana nao wapate nafasi ya kulitumikia Taifa.
“Kwa sababu viongozi wengi wamekuwa na kauli za kuchoma mioyo ya vijana kwamba wajiajiri au waendelee na masomo, tunaomba kwa kuwa wameshalitumikia Taifa kwa muda mrefu, warudi kujiajiri kwani wameshapata mitaji. Tunaomba vijana nasi tupewe ajira ili tulitumikie taifa kwa weledi,” ilieleza sehemu ya andiko hilo.
Walimu hao pia wanataka walioajiriwa wapewe mikataba ya miaka 20 ya kufanya kazi serikalini.
Mkinga alisema kuwa Serikali ina nia njema ya kuanzisha mchakato wa kuwafanyia usaili walimu, lakini utaratibu huo mpya una upungufu.
Amesema usaili huo hauna vigezo vya haki kwa kuwa unawahusisha walimu wote waliohitimu kati ya mwaka 2015 hadi 2023 bila kuzingatia muda wa kuhitimu.
“Tunashauri mchakato wa kuajiri urudishwe Ofisi ya Rais – Tamisemi kama ilivyokuwa zamani na uanze kuajiri wahitimu wa miaka ya nyuma kwanza. Kuna watu wamekaa miaka 10 bila ajira na wanakaribia kufikisha miaka 45, hivyo watakosa sifa ya kuajiriwa serikalini kwa mujibu wa sheria,” amesema Mkinga.
Alipendekeza vyuo vikuu vimalize hatua zote za kuthibitisha walimu kwa kutoa mtihani wa mwisho wa usaili unaofanana vyuo vyote nchini, ambapo ufaulu uwe asilimia 50 kwa nadharia na asilimia 50 kwa vitendo. Wataofaulu wapatiwe leseni ya kufundisha kama ilivyo kwa kada zingine kama udaktari na sheria.
Mkinga amesema uzalishaji wa walimu uzingatie uhitaji wa walimu shuleni. Pia, amesisitiza kuwa kada ya ualimu iwe na masharti maalum ili kuinua hadhi ya walimu.
“Kada ya ualimu imeshushwa hadhi hadi baadhi ya watu wanaona aibu kusema kuwa wao ni walimu. Tunaiomba Serikali iangalie upya namna ya kuwaandaa walimu na kuhakikisha kuwa ualimu unasimamiwa na wataalamu wa elimu bila kuingiliwa na siasa,” amesema.
Katika andiko hilo, walimu hao wamesema wengi wao wanatoka katika familia maskini na walitegemea ajira ya Serikali baada ya kumaliza masomo yao.
Walibainisha kuwa asilimia 80 ya walimu wasio na ajira wamekwamisha ndoto za wategemezi wao kutokana na ukosefu wa ajira.
Walimu hao wameiomba Serikali iwaajiri wote waliomaliza masomo kati ya mwaka 2015 na 2023 na kuzingatia mwaka wa kuhitimu na umri wa mwombaji bila masharti yoyote.
Pia, wamependekeza ajira za muda serikalini wapewe kipaumbele vijana wasio na ajira, na Serikali iongeze kima cha chini cha mishahara kwa walimu wa shule binafsi kutoka Sh207,000 hadi Sh450,000 au kushirikiana na shule binafsi kutoa mikataba ya kudumu kwa walimu.
Mkinga amesema kuwa kati ya mwaka 2021 hadi 2024, Serikali imejenga shule mpya za msingi 1,649 na shule mpya za sekondari 1,042, hivyo kuna uhitaji mkubwa wa walimu.
Amesema wanafunzi katika shule nyingi wanalipa fedha kwa ajili ya walimu wa kujitolea, jambo ambalo linakwenda kinyume na sera ya elimu bure.
Wamependekeza Serikali iajiri walimu wote waliomaliza kati ya mwaka 2015 na 2023 na kuongeza nafasi za ajira kutoka 15,000 hadi 60,000 kwa mwaka kutokana na ongezeko la wanafunzi.
Mkinga amesema Serikali itazame upya ajira kwa watu waliosomea usimamizi wa biashara kama walimu na kuhakikisha kuwa walimu waliobobea katika ufundishaji wa biashara ndio wanaoajiriwa.
“Uamuzi huu unatoa picha mbaya kwa jamii. Walimu wa biashara wanapaswa kuajiriwa, na siyo wale waliomaliza masomo ya usimamizi wa biashara. Tunaomba masuala haya yasihusishwe na siasa,” amesema.
Amesema Serikali inapaswa kuweka mfumo mzuri wa ajira kwa walimu na kuhakikisha kuwa ualimu unasimamiwa na wataalamu wa elimu pekee.