Julio atua Kiluvya United | Mwanaspoti

Kiluvya United imefikia makubaliano na aliyekuwa Kocha wa Ruvu Shooting, Julio Elieza kwa ajili ya kukiongoza kikosi hicho hadi mwisho wa msimu huu, akichukua nafasi ya Zulkifri Iddi ‘Mahdi’ aliyejiunga na timu ya Cosmopolitan.

Akizungumza na Mwanaspoti, Julio alisema amefikia uamuzi huo baada ya kupata ofa nzuri ndani ya kikosi hicho, huku lengo kubwa analopambana nalo ni kuhakikisha timu hiyo inaendelea kusalia tena katika Ligi ya Championship kwa msimu ujao.

“Nashukuru kwa nafasi hii niliyoipata japo natambua wazi haitokuwa kazi nyepesi kutokana na ushindani mkubwa uliokuwepo hapa, jambo kubwa tunalopambania kwa sasa katika michezo minane iliyobaki ni kuhakikisha tunabaki tena Championship tu.”

Kocha huyo wa zamani wa Lipuli FC ya Iringa, alisema ili kufikia malengo hayo ni lazima apate ushirikiano mzuri kutoka kwa viongozi na wachezaji kiujumla, kwani hiyo ndio itakayokuwa silaha kubwa ya kufikia na kutimiza kule wanapopahitaji.

Julio anakuwa ni kocha wa tatu msimu huu kuiongoza timu hiyo baada ya awali kufundishwa na Twaha Beimbaya aliyetimuliwa kutokana na matokeo mabaya, kisha nafasi yake kuchukuliwa na Zulkifri Iddi ‘Mahdi’ ambaye pia ameondoka kikosini humo.

Related Posts