Dar es Salaam. Ukiacha kurahisisha usafiri katika maeneo yenye msongamano na kuokoa muda, usafiri wa pikipiki maarufu bodaboda katika Jiji la Dar es Salaam umekuwa nyenzo hatari kwa matukio ya uhalifu.
Ni bodaboda hizo hizo zinazotumika katika ukwapuaji na unyang’anyi wa mali za raia katika jiji hilo, jambo linalozua hofu kwa wakazi wake.
Unyang’anyi huo hufanywa na watu wanaojulikana vishandu, ambao mara nyingi hutumia bodaboda kukwapua na kutokomea kwa kasi kwenda kusikojulikana.
Kwa mujibu wa wakazi wa jiji hilo, unapokuwa mitaani unalazimika kushika simu, pochi au mabegi kwa tahadhari ili kujiepusha na vishandu, ambao aghalabu hawajulikani wanapotokea.
Kutoka Kinondoni hadi Kariakoo, Ilala, Buguruni, Kigogo, Temeke, Mbagala, Mwenge, Tandale, Gongo la Mboto, Tegeta, Bunju na maeneo mengine, simulizi za uporaji wa ghafla kwa kutumia pikipiki zimekuwa jambo la kawaida.
Omary Hussein (25), mkazi wa Vingunguti, Dar es Salaam, ni miongoni mwa vijana waliowahi kujihusisha na uhalifu huo. Amesema ushawishi wa rafiki yake ulimuingiza kwenye wimbi hilo.
Amesema rafiki yake huyo alikuwa dereva bodaboda, na walipoona hesabu ya bosi haijakamilika, waliamua kwenda kuiba.
“Rafiki yangu alinifundisha udereva wa pikipiki na kisha kuingia naye mtaani. Aliniambia niwe najifunza kuendesha kwa haraka, lakini sikuwa najua lengo lake kwa kipindi hicho,” amesema Omary.
Tukio lake la kwanza lilifanyika Kipawa, alipokwapua pochi yenye simu, kiasi kidogo cha fedha na vitambulisho ambavyo walivitelekeza relini.
Baada ya kufanikiwa, alirudia tukio hilo Kimara, alipomnyang’anya simu binti aliyekuwa akiongea barabarani.
Hata hivyo, ameeleza kuwa wizi huo unaota mizizi kwa sababu madereva wa bodaboda huwakingia kifua wenzao wanapobainika, bila kuhoji chochote.
“Leo hii mtu anaporwa, akienda kijiweni kulalamika anaambiwa alibebwa na hajalipa pesa. Wakishikamana, mambo yanakuwa magumu,” amesema.
Mbali na hilo, anasema baadhi ya bodaboda hujifanya polisi ili kuficha pikipiki ya mhalifu.
Omary anasema wachache wanafanya wizi mchana, lakini wengi wao hutumia usiku kwa sababu hakuna msongamano wa watu na vyombo vya moto.
Ametoa wito kwa wananchi kuwa makini wanapotembea au kusimama vituoni, hata wale wanaopandishwa mishikaki wasiwaamini wenzao kwani wanaweza kuwa kundi moja.
Waathirika wa ‘vishandu’
Mwajuma Khalfani, mkazi wa Kinondoni, ni mmoja wa waathirika wa wizi wa vishandu.
Akisimulia tukio lililomtokea Mwananyamala, amesema aliporwa pochi yake na mtu aliyekuwa kwenye bodaboda.
“Nilikuwa natembea, bodaboda moja iliponikaribia kwa kasi, dereva akaninyang’anya pochi yangu. Nilipoteza simu, pesa za mauzo ya dukani na kadi za benki,” amesema Mwajuma.
Halima Said, mwanafunzi wa chuo, naye alikutana na kundi la bodaboda lililokuwa limetoka Mabibo kwa madai ya kupeleka bondia wao.
“Walinivamia ghafla na kunipokonya mkoba wangu uliokuwa na vifaa vyangu vya kujifunzia. Hata nilipopiga kelele, nilionekana kama mshabiki wao, hivyo hakuna aliyejali,” amesema Halima.
Leornad Njiru, mkazi wa Ukonga, alipoteza fedha zake zote baada ya waendesha bodaboda wawili kumvamia alipokuwa akitoka kwenye huduma ya kifedha.
“Nilikuwa nimepaki gari kando ya barabara. Nikiwa natoka kibanda cha huduma ya pesa, bodaboda moja ilikuja kwa kasi na kunipora bahasha yenye fedha,” amesema Njiru.
Amesema tukio hilo limemfanya awachukie madereva wote wa bodaboda.
Mwenyekiti wa chama cha waendesha bodaboda eneo la Temeke, Abasi Omary, amesema vitendo vya uhalifu wa vishandu vimeharibu sifa ya waendesha bodaboda.
“Wengi tunafanya kazi kwa uaminifu na kutegemea bodaboda kama njia ya kujipatia riziki. Hawa wachache wanaoharibu jina letu wanatufanya sisi waaminifu kuonekana vibaya,” amesema Abasi.
Ameeleza kuwa wanachama wa vyama vya bodaboda wamekuwa wakishirikiana na polisi kuwabaini wahalifu wanaotumia pikipiki kufanya uhalifu.
“Tuna mikutano ya mara kwa mara na polisi na tunawashauri wanachama wetu kuzingatia maadili. Tumewasisitiza wajiunge na vikundi vya bodaboda ili waweze kusaidiana na kupeana taarifa kuhusu vitendo vya uhalifu,” amesema Abasi.
Akizungumza na Mwananchi hivi karibuni, aliyekuwa Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Faustine Mafwele, alisema wameanza kupandikiza watu wao katika maeneo mbalimbali ili kuwatambua wanaojihusisha na wizi kwa kutumia pikipiki.
“Hili jambo ni gumu kufuatilia kwa haraka kwa sababu hawa jamaa hukunja namba za pikipiki zao na hawaweki taa za nyuma. Akifanya uhalifu, ni ngumu kumtambua kwa haraka,” alisema Mafwele.
Alisema pia kuwa masoko yanayonunua simu za mkononi ni chanzo cha wizi huu, na wameanza kufuatilia kwa umakini upatikanaji wa simu hizo.
“Kinachochochea wizi huu ni wanunuzi wa simu za wizi. Natoa angalizo, yeyote atakayekutwa na simu ya wizi atahesabiwa kuwa muhalifu kama mwizi mwenyewe. Sheria inasema aliyeiba na aliyeuziwa wote wanakosa,” alisema.
Pia aliwataka wananchi kuripoti polisi haraka wanapokumbwa na tukio la wizi badala ya kusubiri siku kadhaa, kwani wanapowakamata wezi, wanakosa ushahidi kwa kukosekana mlalamikaji.