Dar es Salaam. Benki ya NMB kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – Tamisemi, imezindua mfumo wa kidijitali wenye lengo la kupunguza mianya ya ufisadi na matumizi mabaya ya rasilimali za Serikali katika mamlaka za Serikali za mitaa.
Mfumo huo umelenga kuboresha usimamizi wa fedha za umma, kuongeza uwazi, na kuboresha ufanisi katika matumizi ya fedha za Serikali.
Pia, utasaidia kuimarisha huduma kwa wananchi na kuongeza uwajibikaji, huku ukitoa uwezo kwa mamlaka za Serikali za mitaa kufuatilia na kudhibiti matumizi ya fedha kwa haraka na kwa usahihi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Idara ya Biashara ya Serikali, Vicky Bishubo, amebainisha kuwa mfumo huo ni sehemu ya juhudi za pamoja kati ya NMB na Serikali katika kuboresha huduma za kifedha, kuongeza uwazi kiutendaji, na kuimarisha usimamizi wa fedha za umma.
Bishubo amesisitiza kuwa mfumo huu utasaidia kuhakikisha mifumo ya kifedha inaendana na teknolojia za kisasa, kwa manufaa ya Taifa.
Ametaja faida nyingine ya mfumo huo kuwa ni kupunguza upotevu wa fedha za umma, kuimarisha uwajibikaji, na kurahisisha ukaguzi wa fedha kwa haraka.
Bishubo amefafanua kuwa mfumo huo utaondoa haja ya kusafiri kwenda benki kwa ajili ya kupata taarifa za akaunti, kwani taarifa zote zitapatikana kwa mtandao.
Amesema mfumo huo utawezesha malipo ya posho na huduma mbalimbali kwa watumishi wa Serikali za mitaa kwa njia ya mtandao.
Uzinduzi wa mfumo huo unatokana na majaribio ya miezi tisa, ambayo yameonyesha matokeo chanya na uwezo wa kubadilisha mfumo wa usimamizi wa fedha za umma nchini.
Katika uzinduzi huo, Katibu Mkuu wa Tamisemi, Adolf Ndunguru, amesema uboreshaji wa mifumo hiyo ni hatua muhimu katika kuboresha usimamizi wa fedha kwenye ngazi za Serikali za mitaa, na linachagiza ufanisi na uwazi katika sekta ya umma.
Kwa upande mwingine, Mkurugenzi wa Serikali za Mitaa, Angelista Kihaga, amesisitiza kuwa utekelezaji wa sera ya benki mtandao ni jambo lisilopingika katika zama hizi za mageuzi ya kidijitali.