Haya ndio yanayojitokeza vituo vya uandikishaji wapigakura Zanzibar

Unguja. Licha ya awamu ya pili ya uandikishaji wapigakura kulenga wananchi ambao wamefikisha umri na hawakuwahi kuandikishwa, imebainika wananchi wengi wanakwenda kwenye vituo vya uandikishaji kubadilisha taarifa zao.

Mbali na kutaka kuhamisha taarifa zao, pia wengine wanakwenda na kopi ya kitambulisho jambo ambalo halikubaliki bali wanatakiwa kuwa na kitambulisho halisi cha Mzanzibari mkaazi.

Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa Zanzibar (ZEC), Aziza Iddi Suwed, akizungumza Machi 16, 2025 baada ya kutembelea vituo vya uandikishaji amesema kazi hiyo kwa sasa hailengi kuhamisha taarifa bali ni kuandika wapigakura wapya, lakini wengi wanakwenda kuhamisha taarifa zao.

“Wananchi wanakuwa hawafahamu wanajua kazi hii inahusisha na mambo mengine ya kuhamisha taarifa au ambao wamepoteza vitambulisho vyao tunawakuta watu wanapanga foleni vituoni, lakini anavyo vitambulisho viwili: cha Mzanzibari na mpigakura anataka kuhamisha taarifa,” amesema.

“Daftari hili linahusisha wapigakura wapya tu ambao hawamo katika daftari la kudumu la wapigakura, kwa wale ambao wanataka kuhamisha taarifa zao waende katika ofisi za tume za wilaya kwa ajili ya kufanyiwa utaratibu na kuelekezwa kuhamisha taarifa zao kutoka shehia moja kwenda nyingine,” amesema.

Hata hivyo, amewasisitiza wananchi wanaokwenda kujiandikisha kuhakikisha wanawasilisha kitambulisho halisi cha Mzanzibari mkaazi na sio kwenda na nakala ya karatasi ama kwenye simu kwani kufanya hivyo hawatoweza kupatiwa huduma.

“Zipo changamoto pia kwa baadhi ya vituo wananchi wanakuja na copy ama kwenye simu na wanafahamishwa kwamba hairuhusiwi na waende wakachukue kitambulisho ili waweze kuandikishwa,” amesema.

Pamoja na changamoto hizo, amesema  wananchi wengi wamejitokeza na wameonesha hamasa kubwa kujiandikisha na wale wanaotimiza sifa za kuandikishwa basi wanapatiwa fursa hiyo bila ya matatizo yoyote.

Hivyo, amewasihi wananchi waendelee kujitokeza ili wasije kupoteza haki yao ya kupiga kura utakapofika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

 Sheha wa Shehia ya Kilimani, Khalid Ali Kombo amesema wananchi wamehamasika kwa wingi kwenda kujiandikisha na matarajio yao kuandikisha wapigakura wapya zaidi ya 150.

Maryam Mwinyi Yussuf ni wakala wa Chama cha TLP, amesema kazi hiyo inakwenda vizuri na wamekuwa wakishirikiana pamoja baina yao mkuu wa kituo na sheha wa shehia husika.

Jokha Issa Muhammed aliipongeza ZEC kwa utaratibu mzuri waliouweka kwa kuwa, hakuna usumbufu wowote wanaoupata, mtu anapata huduma na kuondoka.

Haji Ibrahim Omar, amesema kazi hiyo ni  muhimu kwa kila kijana kujiandikisha kwa sababu kila mtu ana haki ya kumchagua kiongozi anayemtaka kutokana na uamuzi wake.

Hivyo, waliwahamasisha vijana wenzao kujitokeza kujiandikisha kwani kitambulisho hicho kitawawezesha kushiriki katika uchaguzi unaokuja na kuwachagua viongozi wanaowataka.

Related Posts