Tanga. Imeelezwa kuwa, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga, Bombo, haina daktari bingwa wa magonjwa ya dharura, hali inayosababisha huduma za kibingwa kushindwa kutolewa.
Mkuu wa Idara ya Tiba na Huduma za Magonjwa ya Dharura (EMD), hospitalini hapo, Dk Arafa Kachenje amesema hayo juzi katika mahojiano maalumu na Mwananchi Digital, wakati wa ziara ya mafunzo kwa waandishi wa habari kutembelea mradi wa huduma za dharura nchini katika ngazi ya kijiji, mkoa na Taifa, unaofadhiliwa na Mfuko wa Abbott Fund Tanzania wakishirikiana na Wizara ya Afya.
Amesema kwa sasa idara hiyo ina jumla ya watumishi 34 wakiwamo madaktari wa kawaida 13, manesi 15, wafamasia watatu, wataalamu wa maabara na ofisa Ustawi wa Jamii mmoja, lakini haina daktari bingwa wa magonjwa ya dharura.
Kutokana na changamoto hiyo ameomba wapatiwe madaktari bingwa wanne ili huduma za wagonjwa wa dharura zifanyike kwa ufanisi.
Mbali na kutokuwa na daktari bingwa wa magonjwa ya dhararu, Dk Kachenje amewataka wakazi wa Tanga, kutenga muda na kuwa na utamaduni wa kufanya uchunguzi wa afya zao mara kwa mara ili kujua afya zao na kupata matibabu mapema iwapo watagundulika kuwa na magonjwa.
“Kuchelewa kufanya uchunguzi wa afya zao, kumesababisha wagonjwa wengine wanaofika katika idara yangu kwa ajili ya matibabu wakiwa katika hali mbaya,” amesema Dk Kachenje.
Pia, amewata wagonjwa wenye tatizo la figo, moyo, kisukari na shinikizo la juu la damu, kuzingatia masharti na maelekezo ya madaktari na wataalamu wa afya ikiwamo ulaji unaofaa pamoja na kwenda kliniki kwa wakati ili kuepuka athari zinazoweza kuwapata watakapokiuka masharti waliyopewa.
“Muitikio mdogo wa watu kwenda kufanya uchunguzi wa afya zao, umesababisha kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wanaofika katika Idara yetu kupata matibabu na wengine wakiwa katika hali mbaya, lakini kama jamii ingekuwa na utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara na kujua afya zao, basi wangechukua hatua za haraka wamebainika kuwanna tatizo la afya,” amesena Dk Kachenje.
Pia, amesema kwa siku, idara hiyo iliyoanzishwa mwaka 2019 kwa ufadhili wa Mfuko wa Abbott, inapokea wagonjwa kati ya 60 hadi 80 kwa ajili ya kupatiwa huduma dharura.
Amesema kati ya wagonjwa wanaofika kuhudumiwa kwa siku, nusu ya wagonjwa hao ni wagonjwa wa figo, matatizo ya moyo, kisukari na shinikizo la juu la damu.
Wengine ni wagonjwa wanaotokana na ajali mbalimbali za mvunjiko, moto na upasuaji.
Katika hatua nyingine, Dk Kachenje ameomba Jengo la Idara ya Dharura liongezwe kutokana na lililopo kuwa dogo ili liweze kuhudumia wagonjwa 150 hadi 200 kwa siku.
Awali, Hospitali ya Bombo ilikuwa haina idara ya tiba za dharura lakini mwaka 2019, Serikali ilishirikiana na Mfuko wa Abbott ilianzisha huduma hiyo.
“Kwa sasa idara hiyo ina jumla ya vyumba saba vya kutolea huduma hiyo kwa ajili ya watu wazima, watoto na wale,” amesema Dk Kachenje.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Abbott Tanzania, Profesa Hendry Sawe amesema lengo la mfuko huo ni kushirikiana na Wizara ya Afya kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma bora za afya.
Profesa Sawe amesema kutokana na umuhimu wa huduma hiyo, Abbott ilitoa Sh444 milioni kwa ajili ya ukarabati na usimikaji vifaa tiba katika jengo hilo la EMD Hospitali ya Bombo.
” Huduma ya tiba za dharura ni sehemu muhimu ya huduma za matibabu, lakini maeneo mengi ulimwenguni yana upungufu wa miundombinu ya kutolea huduma hii, ndio maana mfuko huo umeamua kusaidiana na Serikali ili wananchi wapate huduma bora za afya,” amesema Profesa Sawe.
Kwa upande wake, Dk Said Izina ambaye ni Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Bantu iliyopo Kata ya Mapambano Wilaya ya Mkinga, amesema huduma ya dharura iliyopo katika zahanati yake imesaidia kuokoa maisha ya wananchi wanaofika kupata huduma.
Agnes Singano ni mmoja wa wagonjwa wanatibiwa katika zahanati hiyo, amesema kabla ya kuwepo kwa huduma ya dharura, alikuwa anatumia gharama kubwa kufuata huduma Hospitali ya Bombo.
“Nina tatizo la pumu tangu nikiwa darasa la tatu mwaka 2003, hivyo ili nipate matibabu ilikuwa inanigharimu kutumia zaidi ya Sh20,000 kufuata matibabu kwa siku, lakini kuwepo kwa huduma hii kijijini kwetu, imenisaidia kupunguza gharama,” amesema Singano.